Maisha ya Maria na Consolata

Baada ya kuwapo sintofahamu juu ya nini hasa kilichowua watoto mapacha Maria na Consolata, Gazeti la Uchunguzi la JAMHURI limeamua kutafuta ukweli wa chimbuko la kifo cha mapacha hawa, ambao hatimaye sasa umefahamika.

Mapacha hao Maria na Consolata, walifariki dunia Jumamosi, Juni 2, 2018, saa 02:00 usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa baada ya kuugua kitambo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI  umebaini kuwa sababu kubwa iliyochangia kifo cha Maria na Consolata ni upungufu wa oxgen kwenye damu tatizo ambalo lilikuwa likimpata Maria.

JAMHURI limefanya mahojiano maalumu na Daktari Bingwa wa Upasuaji, ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk. Mseleto Nyakiloto, aliyekuwa anaongoza jopo la madaktari kuwapatia tiba mapacha hao.

JAMHURI: Dk. Nyakiloto jamii inajiuliza kwanini Maria na Consolata wamefariki sasa na si miaka 10 iliyopita. Nini hasa kimechangia kifo chao?

Dk. Nyakiloto: Maria ndiye aliyekuwa mgonjwa, Consolata hakuwa mgonjwa kabisa na hata vipimo vilivyofanyika Muhimbili vilikuja na majibu ya Maria peke yake.

Kifo chao kimetokana na kupungua, hatimaye kukosekana kwa hewa safi mwilini (Oxgen) ambako kulisababishwa na mwili wa Maria.

Kuna kipindi Maria alikuwa akishindwa kupumua Consolata naye baada ya muda alikuwa analalamika kupata maumivu mwilini. Hii ninatokana na wao kuchangia mshipa mkubwa wa damu [mapacha hawa wawili walikuwa wanatumia mshipa mmoja mkubwa wa damu. Kila ninadamu anao mshipa mkubwa mmoja wa damu hivyo wangekuwa na mishipa miwili hali hiyo isingetokea kwa wote kwa wakati mmoja].

Kulikuwa na upungufu wa oxgen kwenye damu ya Maria na kusababisha maumivu kwa mwenzake hivyo hata Maria mwili wake ulipokuwa ukibadilika rangi kutokana na oxgen kuwa ndogo baada ya muda na Consolatha alikuwa akipata tatizo kama la mwenzake.

Wamekufa kutokana na maumbile yao kwani yalipokuwa yamefikia maumbile ya mwili wa Maria yalikuwa tayari yamechoka hasa mapafu.

JAMHURI: Kwanini hawakufa mapema?

Dk. Nyakiloto: Hawakufa mapema kutokana na viungo vyao vilikuwa bado vina uwezo wa kusaidia ‘kusupport’ mwili kwa ujumla ambavyo ni mapafu, moyo na ubongo.

Sasa kilichotokea ni mapafu ya Maria kutofanya kazi tena kutokana na maumbile yake ya kuwa chini siku zote [Kati ya mapacha hawa Maria alikuwa anakaa chini na Consolata alikuwa juu yake siku zote. Dk. alisema yalifanyika makosa ya kimalezitangu wakiwa watoto kwani wangekuwa wanabadilishana mkao siku hadi siku, lakini hilo halikutokea hali iliyofanya mapafu ya Maria kukandamizwa na Consolata miaka yote waliyoishi]. Pia ni vyema ukafahamu kuwa mapafu ndiyo yanayoingiza hewa mwilini na yasipopata hewa kwa zaidi ya dakika tatu huwezi kuishi tena.

JAMHURI: Baada ya kugundua tatizo kupungukiwa hewa kwenye damu ndiyo mliamua kuwahamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?

Dk. Nyakiloto: Hapana, mara ya kwanza walifika hapa mwishoni mwa mwaka jana wakiwa na tatizo jingine kabisa. Walipofika hapa walimuona daktari ambaye aliwaunganisha na daktari wa magonjwa ya kike aliyeanza kuwahudumia.

[Tatizo la mwaka jana kwa mujibu wa uchunguzi ilikuwa ni kuwa Maria na Consolata walipokuwa wanapata hedhi ilikuwa inachukua muda mrefu hadi wiki mbili na zaidi (overbreeding)] Kutokana na tatizo walilokuja nalo ilibidi waongezewe damu pia waendelee kuwa chini ya uangalizi.

Lakini wakati akiwahudumia kutokana na tatizo walilokuja nalo, aligundua ya kuwa wana tatizo kwenye mfumo wa upumuaji hivyo tulidhani kuwa wana tatizo la moyo hivyo tukaona ni vyema wakapata matibabu kwenye hospitali ya Jakaya Kikwete iliyopo Muhimbili.

Walipofika Muhimbili huko ndiyo wakagundulika kuwa sio moyo kama tulivyodhani bali ni matatizo mengine ambayo alikuwa nayo Maria.

JAMHURI: Walikuwa na tatizo gani hasa lililosababisha mpaka wakaongezewa damu?

Dk. Nyakiloto: Naomba nisizungumzie hili kwa sasa.

JAMHURI: Umesema Maria pekee ndiye alikuwa mgonjwa, ni kwanini ugonjwa wake ulikuwa unamuathiri Consolata?

Dk. Nyakiloto: Consolata alikuwa anapata damu yenye oxgen nyingi ambayo husambaa mpaka kwenye ubongo kama inavyohitajika kwa binadamu yeyote.

Pia njia yake ya upumuaji ilikuwa haijaathirika kabisa ndio maana hakufa mapema [walipishana kufariki dakika 10 na Maria].

Lakini damu ya Maria iliyokuwa inaenda kwenye ubongo ilikuwa haina oxgen.

JAMHURI: Waliporudishwa katika hospitali yenu kutoka Muhimbili walikuwa katika hali gani?

Dk. Nyakiloto: Muhimbili walipatiwa huduma zinazohitajika, kutokana na tatizo lao walifikia hatua ya kufanya mawasiliano na hospitali za nje hasa India ili kuwapeleka kwa matibabu zaidi. Walifikiria suala la kuwatenganisha, lakini baada ya mawasiliano ya kitabibu haikuwezekana.

Walirudishwa hapa moja kwa moja na kupelekwa kwenye Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) kwani walikuja wanapumulia mashine.

Waliletwa kwa ajili ya kuwa karibu na familia huku wakiendelea na matibabu pamoja na kufuatiliwa na wataalamu wa hospitali [huku mambo mengine yakiachwa mikononi mwa Mungu].

JAMHURI: Mliwaza nini baada ya mmoja wao kufariki na mwingine kuwa hai?

Dk. Nyakiloto: Ukweli ni kwamba tulikuwa na hofu iwapo Maria atakufa wakati Consolata yupo hai. Tulipata hofu kwa vile sisi ni binadamu pia.

Jambo la kushukuru ni kwamba Maria alipofariki Consolata hakujua, lakini baada ya dakika 10-15 naye akafariki. Lilikuwa si jambo rahisi hata kidogo.

Mmoja wa Madaktari katika hospitali hiyo (jina linahifadhiwa), amelieleza JAMHURI kwamba Maria na Consolata walifika hospitali ya Mkoa wa Iringa wakiwa na tatizo la hedhi ambalo lilisababisha kuongezewa damu huku vipimo vingine vikiendelea.

Pia ameeleza kuwa katika vipimo vilivyofanywa kwa Maria vilibaini kuwa alikuwa na uchafu (damu iliyotakiwa kutoka wakati wa hedhi ilikuwa haitoki bali ilikuwa ikitunzwa kwenye mfuko na kama ilikuwa inatoka basi ilikuwa inatoka kidogo na nyingine kuendelea kuwa kwenye kizazi) katika mfuko wa kizazi.

Madaktari walifanya kila linalowezekana kutibu tatizo hili, ila kwa kuwa walichelewa kulibaini na baadhi ya viungo vya Maria vilikwishaanza kulegea, hawakuwa na jinsi zaidi ya kuwashuri wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kuwaweka katika maombi na kuwaombea huruma ya Mungu, hadi mauti yalipowakuta.

 

Marafiki wa Maria na Consolata

 

JAMHURI limefanya mahojiano na marafiki wa Maria na Consolata ambao ni Happy Lucas (21) na Aisha Bakari (21) ambao wanasema katika darasa lao walizoea kuwaona mapacha hao wakiwa wenye furaha na kamwe hawakuwahi kuona wakiwa wametofautiana.

“Masister walituambia kuwa kuna wakati Maria na Consolata huwa wanachoka hivyo tuwe karibu nao, ikitokea tukahisi au kuwaona wanalala wakati wa kipindi tuwe tunawagusa taratibu kwenye mabega wataamka,” anasema Aisha.

Wanasema kuna kipindi walikuwa wanapitiwa na usingizi wakati wa masomo.

Wameeleza kuwa katika mtihani chuoni hapo walipata alama kubwa kuliko darasa zima jambo ambalo liliwaumiza wanafunzi wenzao walipofariki na kuona vipaji vimepotea.

“Walipata 11/15 na 10.5/15 kwenye somo la Kiswahili huku sisi wengine tukiishia kupata 5/15 na wengine wakipata 0. Mwalimu alitusema sana kuwa sisi ni wazembe inakuwaje tunapata alama ndogo hivyo wakati wote tunasoma darasa moja,” amesema Aisha.

Aisha anasema walikuwa katika kundi moja la masomo ya Kiswahili na Kingereza na kwamba walikuwa wanamtegemea sana Consolata katika kuandika kazi za kundi lao.

“Consolata alikuwa na spidi ya kuandika kwa kutumia kompyuta yake, alikuwa anasaidia kuokoa pesa kwani kazi alizokuwa akizifanya kwenye kundi letu zingetugharimu zaidi ya Sh 10,000, lakini yeye alikuwa anafanya bure alafu tunalipia kupiga copy Sh 2,000 tu,” anasema.

Alipoulizwa iwapo waliwahi kuwa kwenye mahusiano (mapenzi) hapo chuoni, walisema kwamba waliwahi kuwasikia wakisema kuwa kuna kijana mmoja ambaye wanampenda wanatamani kuwa na familia.

“Waliwahi kusema kuwa ‘wana-crush,’ lakini hawakutaka kusema zaidi maana walikuwa watu wa utani, hivyo hatukuendelea kuwauliza na ukizingatia tulikuwa kwenye mazungumzo ya kundi (group),” amesema Happy.

Pia wamebainisha kuwa kabla ya kulazwa hospitalini, Maria na Consolata waliwaeleza kuwa pindi watakaporudi semester ya pili walikuwa na mpango wa kuhama kozi kutoka ualimu na kuhamia IT.

“Tuliwaeleza kuwa hata wakihama tutaendelea kuwa rafiki zao kwani kuhama kwao hakutaondoa urafiki wetu,” amesema Aisha.

JAMHURI limefanya mahojiano na Prisca Luvigo (23) na Nuru Mfikwa (18) waliokuwa wakiishi na Maria na Consolata ambao wamesema mabinti hao kila mmoja alikuwa akiwaasa kuishi vizuri na watu.

Wanasema wameishi na Maria na Consolata tangu walipojiunga na chuo kikuu na kwamba Consolata alikuwa anapenda kaungalia bongo movie, hasa zilizochezwa na marehemu Steven Kanumba na tamthilia za Kinaijeria. Huku Maria akielezwa kuwa alikuwa anapenda kuchat.

Wamesema kwamba kuna kipindi walikuwa wanatofautiana wanapoulizwa nini watakula kwa siku, lakini baada ya majadiliano ya muda mfupi walikuwa wanafanya uamuzi wa pamoja.

 

 

“Unaweza kuwauliza siku hiyo watapenda kula nini, kila mmoja akatamka chakula anachojisikia kula, hivyo mabishano yanaanza. Lakini utasikia wanaamua kula chakula kimojawapo na kingine watakula baadaye,” amesema Prisca.

Marafiki hao walimeliambia JAMHURI kuwa vifo vya mapacha hao vimewaumiza mno na kwamba ni jambo ambalo hawataki kulikumbuka kwani walikuwa familia yao.

JAMHURI limefanya mahojiano na Sister Jane Nugi ambaye alikuwa mlezi wa mapacha Maria na Consolata;

JAMHURI: Ndoto za Maria na Consolata zilikuwa zipi?

Sister Jane: Mabinti hawa walikuwa na ndoto nyingi, hasa kuja kuwasaidia yatima kama walivyosaidiwa wao, ikiwa ni pamoja na kufungua kituo cha kutoa misaada.

Pia walikuwa na ndoto ya kuwa na familia hapo baadaye.

JAMHURI: Kuna taarifa kuwa wamewahi kuvutiwa na kijana mmoja, je, unalifahamu hili?

Sister Jane: Hili suala nalifahamu na kijana mwenyewe namfahamu. Ni kijana ambaye alikuwa akiwatangulia darasa wakati wanasoma sekondari. Walivutiwa naye kutokana na ukaribu wao.

Huyu kijana siku zote alionekana kuwapenda na kuwajali. Alikuwa akiwasukuma kwenye baiskeli yao kila mara pindi wanapotaka kwenda sehemu, [lakini] nilipoongea nao wakasema kwamba wanataka kuwa na familia ambayo wata-adopt (kuasili). Lakini sipendi kuzungumzia hili naomba tuliache.

JAMHURI: Maria na Consolata walipenda nini?

Sister Jane: Kwanza walipenda kusoma Biblia na vitabu vya mithali, ingawa mara nyingi walipenda kusali.Kuhusu chakula walikuwa wanapenda kula ndizi na samaki.

JAMHURI: Kuna taarifa kuwa walikuwa na mpango wa kutoendelea na masomo ya ualimu, walikueleza hili?

Sister Jane: Ni kweli, waliniambia kuwa wanajisikia kuwa ualimu unahitaji nguvu zaidi na changamoto zake ni kubwa ambazo ni vigumu kwao kuzimudu kutokana na hali yao.

Wakanieleza kuwa wanataka kwenda kusoma IT na wangehamia huko muhula wa pili wa masomo. Niliwakubalia hivyo nikaenda kuongea na mtawala wa chuo kuhusiana na hilo ili aelewe.

JAMHURI: Umesema ulizungumza na madakatari wa Mhimbili, mlizungumza nini?

Sister Jane: Madakatari walinambia kuwa mapafu ya Maria hayafanyi kazi tena, yaliacha kufanya kazi sababu ya position [mkao] yake.

Nilizungumza na jopo la madaktari watano Muhimbili ambao walinieleza ukweli, hivyo tukaanza kuwapatia ushauri wa kisaikolojia kwa kutumia madaktari waliopo hospitali.

Na walipoletwa tena Iringa tuliendelea na matibabu hayo kwani si kawaida kwa binadamu kukubali kifo. Tulitaka waelewe hali yao ilivyokuwa.

[Anasema walipowajulisha hali yao walishituka, ila mwisho wa siku kutokana na tiba ya kisaikolojia walielewa na kubali ukweli kuwa hakukuwapo namna zaidi ya kukubali matokeo, ila wakaendelea kusali sala nyingi kadri ilivyowezekana].

JAMHURI: Nini unachojivunia kwa Maria na Consolata?

Sister Jane: Walikuwa na shukrani. Na kipindi chao cha mwisho walituomba tuwaombee msamaha pale walipokosea.

Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya maisha yao, tumetimiza wajibu wetu. Mungu ni mwema. Nilikuwa na hamu ya kuwaona wakitimiza ndoto zao.

Walikuwa wanataka wakimaliza masomo watumie taaluma yao watakayopata kuingiza kipato na kusaidia wenye mahitaji hasa yatima.

 

Historia

Kifo chao kimewagusa wengi Tanzania, wengi wakituma salamu zao za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.

Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli, ambaye miezi kadha alikutana na pacha hao, ameeleza kusikitishwa kwake na kifo vyao.

“Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa,” ameandika Rais Magufuli kwenye ukurasa wake wa twitter.

Pacha hao waliokuwa na umri wa miaka 22 wamekuwa wakitunzwa na watawa wa Kanisa Katoliki baada ya kuzaliwa.

Mwaka jana, walijiunga na Chuo Kikuu cha Ruaha Catholic University na kuanza na masomo ya kompyuta kabla ya kuanza masomo kamili.

Oktoba mwaka jana, walianza masomo yao katika chuo hicho wakisomea Shahada ya Kwanza ya Ualimu. Maria na Consolata walikuwa wamefanya mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa.

Maisha ya Maria na Consolata

Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa mwaka 1996, katika eneo la Ikonda, Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe .

Walisoma shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye wakasoma hadi kidato cha sita katika shule ya Udzungwa iliyoko Wilaya ya Kilolo.

Septemba mwaka jana, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walijiunga na chuo kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Iringa (RUCU).

Walianza kuugua Desemba, mwaka jana wakahamishiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili. Baadaye walirejeshwa Iringa, kama ilivyoelezwa hapo juu hadi mauti yalipowakuta.

 

 

 

Mama yao alikuwa anaitwa Naomi Mshumbusi Mwakikuti, alifariki Juni 24, 2004 akazikwa nyumbani kwao Bukoba, mkoani Kagera.

Baba yao alikuwa anaitwa Wilfred Juma Mwakikuti, alikuwa mwenyeji wa Mbeya. Alifariki Desemba, 2001.

Mahojiano aliyofanya daktari na BBC

Awali Dk. Nyakiloto alikuwa amezungumza na BBC. Yafuatayo ni mahojiano kati ya daktari huyona BBC kuhusiana na mapacha hao kama ifuatavyo:-

“Maumbile ya Maria na Consolta ndio sababu kubwa iliyochangia kifo chao” Daktari Mseleto Nyakiloto ameeleza hayo alipozungumza na BBC.

Mseleto Nyakiloto ambaye ni Daktari Bingwa wa Upasuaji na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Iringa ameeleza chanzo kilichosababisha wasichana hao kufariki ni tatizo la njia ya hewa.

“Mmoja alitangulia na mwingine alifariki baada ya dakika kumi, Maria ndio alikuwa ana tatizo la kiafya kwa kuwa mapafu yake yalishindwa kufanya kazi na huyu mwingine alikufa kutokana na viungo vingi katika mwili wao wanavitumia kwa pamoja,”Dk. Nyakiloto anaeleza.

Daktari huyo aliongeza kwa kwamba mzunguko wa hewa na damu ndio umesababisha kifo cha mwingine hivyo matarajio ya mmoja kupona yasingewezekana.

Aidha daktari Nyakiloto amesema mapacha wa aina hii wapo wa aina nyingi ingawa muda wa maisha yao huwa unatofautina kutokana mazingira pia; kuna wale ambao hata hawafikii hatua ya kuzaliwa, wengine wanakaa muda mfupi wanafariki na wengine ndio wanajitahidi wanafikia umri mkubwa kama ya kina Maria na Consolata wameweza kufika miaka 21.

Mwaka 2004, BBC iliandika juu ya watoto hawa mapacha ambao walikuwa na miaka minane kuwa maisha yao yakiwa kwenye mashaka.

Tatizo kubwa ambalo lilikuwa linawasumbua ilikuwa mapafu yao yana uzito mkubwa kuliko mwili wao.

Madaktari walikuwa na hofu juu ya tatizo la mmoja linaweza kusababisha mwingine kuathirika na kuwafanyia upasuaji, kutaongeza tatizo kuwa kubwa zaidi.

Maria aliwahi kula kwa ajili ya mwenzake kwa miaka mitano. Miguu yao ilikuwa imechukua sehemu kubwa ya mwili,

Kwa Maria mguu wake wa kulia ndio ulikuwa na nguvu wakati Consolatha ulikuwa wa kushoto na miguu yao mengine ilikuwa haifanyi kazi. Walikuwa na vichwa viwili, mioyo miwili na mikono minne.

Na walikuwa wanatumia viongo vingine kwa pamoja kama tumbo, ini, sehemu ya uke na haja.

Maria alikuwa na matatizo ya kiafya tangu alipozaliwa, alikuwa na shida ya kupumua, licha ya kuwa alikuwa na uwezo wa kula chakula zaidi ya mwenzie.

Maria alikuwa akila kwa niaba ya ndugu yake kwa takribani miaka mitano na nusu ndipo Consolata na yeye alipoanza kula mwenyewe.

Dk. Rainer Brandl aliiambia BBC Network Africa mwaka 2004, kuwa mapafu yao yalikuwa hayako sawa kwa namna ambavyo hawawezi kuhimili miili yao na hayawezi kuongezeka zaidi. Na kilichobaki ni kuwaombea ili waendelee kuishi kwa matumaini.

Katika maisha yao kutegemeana ndio jambo kubwa na la kawaida, kwa mfano Maria akitaka kwenda chooni atamjulisha mwenzie na vivyo hivyo kwa Consolata.

Maisha yao yalijawa na ndoto nyingi

Maria na Consolata walikuwa katika maisha yenye matumani na walitamani siku moja kuwa walimu na waliweza kuingia chuo kikuu kusomea masomo ya ualimu.

Licha ya kuwa zamani walikuwa ndoto tofauti, lakini baadaye waliweza kuwa na nia moja ya kuwa walimu.

Walikuwa wanatofautiana pia katika tabia, fikra na hata kuongea. Awali mmoja alipenda kuwa daktari na mwingine kuwa sista, lakini badae wote wakapenda kuwa walimu.

Wanapenda vitu tofauti pia kuna ambaye alikuwa anapenda muziki wa bongo fleva na mwingine injili. Watoto hao pia walikuwa wanagombana na kupatana.

Maisha yao yalikuwa ya neema kutokana na mazingira waliyokulia na wanafunzi wenzao waliona kuwa watoto hao walikuwa chachu katika jamii kutowatenga watoto walemavu.

Ndoto yao pia ambayo waliibainisha walipozungumza na BBC ni kwamba walikuwa wanamatumaini kuolewa na mume mwerevu na watayeweza kumsaidia na asione kuwa wao ni tegemezi.

Mapacha walioungana wakoje?

Mapacha walioungana huwa ni wachache sana kutokea au kuwepo, katika watoto 200,000 wanaozaliwa kila mwaka anazaliwa mtoto mmoja tu wa aina hiyo.

Watoto wengi huwa hawawezi kuishi, hufa mara baada ya kuzaliwa au mimba huharibika.

Watoto hawa huzaliwa katika uzao wa yai moja, hufanana na huwa na jinsia moja.

Kuzaliwa kwa watoto hawa huwa kuna hali ya kustaajabisha, kwa ujumla watoto hao wanaweza kuishi wakizaliwa katika hali hiyo huwa ni kati ya asilimia 5 mpaka asilimia 25.

Katika rekodi za historia zinasema kwamba mapacha wa kuungana wengi wanaoweza kuishi kwa muda mrefu ni wa kike, kwa asilimia 70

Mapacha walioungana wamegawanyika katika sehemu tatu

  • Asilimia 73 wameunganika kuanzia kwenye kifua na tumbo
  • Asilimia 23 wanakuwa wameunganika katika sehemu ya chini ya mapaja na miguu
  • Asilimia 4 wanakuwa wameunganika kichwa

Mapacha walioungana waliowahi kuwa maarufu duniani

Kwa miaka mingi mapacha walioungana wameendelea kuishi kutokana na matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa na majaribio mengi ya upasuaji yaliyofanyika.

Mapacha wa kwanza wa kuungana waliojipatia umaarufu mkubwa duniani walijulikana kama ‘Siamese’ majina yao yalikuwa ni Eng na Chang.

Mapacha hao walizaliwa mwaka 1811, waliweza kuishi kwa miaka 63 na kufanikiwa kupata watoto 22 kutoka kwa wadada wawili ndugu waliowaoa wakiwa na umri wa miaka 21.Chang alikuwa na watoto 12 na Eng watoto 10.

Walipozaliwa jamii ilitaka kuwauwa, lakini kwa kudhaniwa kuwa wataleta mikosi na walioneka kuwa ni viumbe wa ajabu.

Mapacha wa kuungana na maisha yao ya ndoa

Katika karne ya 20, mapacha wa kuungana walikuwa wanazuiwa kuoa au kuolewa nchini Marekani

Na hii iliibua hisia za wengi pale ambapo wanamuziki ambao ni wacheza filamu wa nchi hiyo Daisy na Violet walipotaka kuolewa.

Watu wengi waliwaona kuwa maumbile yao hayawezi kuwaruhusu kuolewa au kupata wenza ingawa mapacha wenyewe wanajiona wamekamilika.

Kwa upande wa Chang na Eng ambao walifanikiwa kuoa, maisha yao ya ndoa yalikuwa na changamoto nyingi hasa pale ambapo wake zao walipoanza kugombana na kusababisha wake hao kuishi kwenye nyumba mbili tofauti.

Kwa maisha yao yote mapacha hao walikuwa wanaishi kwa mke mmoja siku tatu na mwingine siku tatu.

Vilevile mapacha kutoka Tanzania, Consolata na Maria ndoto yao kubwa baada ya shule ni kuolewa na mume mmoja.

Habari za Maria na Consolata zimeandikwa na mashirika yote makubwa ya habari duniani zikiwamo CNN, BBC, Aljazeera na mashirika mengine makubwa.

Habari hii imeandikwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Wakfu wa vyombo vya habari nchini Tanzania (TMF) 

 SOMA GAZETI LOTE LA JAMHURI HAPA

1307 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons