‘Majangili’ 3 mbaroni Arusha

Watu watatu, wamekamatwa mkoani Arusha wakiwa na vipande 16 vya pembe za tembo. Wawili kati yao wanatoka jamii ya Kimaasai ambayo kwa miaka mingi ilijulikana kuwa ni wahifadhi wazuri.

Taarifa kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha zimewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jeremiah Slaa (45), mkazi wa Kijiji cha Elekepusi, Ngorongoro mkoani Arusha.

Mwingine ni Nayayi Kiyapi (30) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kemenokla kilichoko ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. 

Polisi wamesema watuhumiwa hao wamekamatwa Karatu wakiwa na vipande 10 vya pembe za tembo, siku ambayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wafanyakazi na viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mtuhumiwa mwingine aliyetiwa mbaroni akiwa na vipande sita vya pembe za tembo ni Simon Shauri, mkazi wa Kijiji cha Majimoto mkoani Rukwa. 

Polisi wamethibitisha kuwa watuhumiwa wote wamekamatwa na Kikosi Maalumu kinachopambana na ujangili katika Kanda ya Kaskazini.

“Watuhumiwa wawili wa kwanza walipohojiwa walikiri kuhusika na matukio ya ujangili kuanzia mwaka 2014. Walisema wanaua tembo kwa kutumia sumu na mikuki.

“Hii ni hatari kwa sababu Wamaasai ndiyo walioheshimika kwa uhifadhi, lakini sasa ni miongoni kwa watuhumiwa wakuu wa ujangili,” kimesema chanzo chetu kutoka Polisi.

Mtuhumiwa Shauri, mwenye umri wa miaka 65, inasemekana alikuwa na bunduki mbili aina ya Rifle 375 na Rifle 458, lakini akazisalimisha polisi.

“Hizo bunduki alizisalimisha, lakini akawa anatumia bunduki za mtuhumiwa mwingine aitwaye Ojuku, ambaye sasa yuko rumande akikabiliwa na kesi za ujangili lakini bunduki zake zinatumiwa na mdogo wake. Huyu Shauri amekuwa akipewa bunduki kutoka kwa mdogo wake Ojuku na kwenda kuua tembo,” kimesema chanzo chetu.

Katika hatua nyingine, imebainika kuwa polisi walio kwenye Kikosi Kazi kinachopambana na ujangili, wamekuwa wakinyimwa ushirikiano kutoka kwa wakuu wa vituo vya polisi wa maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.

Uchunguzi umebaini kuwa kikosi hicho kinapowakamata watuhumiwa na kuwafikisha polisi, wamekuwa ‘wakinyanyapaliwa’ kwa kuambiwa vituo hivyo haviwajibiki na watuhumiwa wa ujangili.

“Inashangaza kusikia hivyo maana hawa ni polisi wanaofanya kazi za hatari za kulinda rasilimali za nchi yetu. Tumepokea malalamiko kutoka kwao na tunatoa maagizo kwa wakuu wote wa vituo na askari kuwapa ushirikiano wanapofikisha watuhumiwa vituoni.

“Hatutasita kuchukua hatua kali za kinidhamu endapo tutapata ushahidi wa baadhi ya wakuu wa polisi wa vituo kukataa kupokea watuhumiwa wa ujangili, au kufanya njama za kuvuruga kesi,” amesema mmoja wa maofisa wa juu wa Polisi mkoani Arusha.

Wakati huo huo, uhaba wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuwawezesha askari kwenye Kikosi Kazi umetajwa kuwa kikwazo kingine katika mapambano dhidi ya ujangili.

“Tuna taarifa nyingi ambazo ni viporo na nyingine nyingi ambazo zinapaswa kufuatiliwa, lakini fedha zimekuwa tatizo kubwa. Tunawasiliana na wakuu wetu ili kuona namna ya kutuwezesha,” amesema ofisa huyo.