Kama unahitaji njia rahisi na ya asili ya kuepukana na maisha yenye hasira au yaliyojaa msongo wa mawazo, basi jenga utamaduni wa kunywa maji kwa wingi. Ogani zote kwenye miili yetu zikiwamo ubongo, zinahitaji maji kwa wingi ili kufanya kazi kwa ufasaha.
Hivyo kukosa kiwango stahiki cha maji kunaathiri afya ya ubongo moja kwa moja na hivyo kusababisha msongo wa mawazo. Kiafya, imethibitika kuwa, ukosefu wa maji kwa kiasi cha nusu lita kwa siku kunasisimua na kupandisha kiwango cha homoni inayoratibu mapokeo ya hasira na msongo wa mawazo mwilini. Homoni hii kwa kitaalamu inaitwa cortisol.

Hii haina maana kuwa, kunywa kiwango kikubwa cha maji mfululizo kwa muda wa siku nzima kutaondoa matatizo unayokutana nayo kila siku ya kimaisha kama vile ya kifedha, ya kifamilia au hata mengineyo,hapana! Lakini kama tayari matatizo haya yameshakusababishia msongo wa mawazo, haupaswi kuendelea kuathirika na msongo wa mawazo kwa kukosa na kiwango stahiki cha maji mwilini na kuleta madhara zaidi ya kiafya.
Pia unakuwa hatarini zaidi kukaukiwa na maji mwilini ukiwa na msongo wa mawazo kwa sababu wakati wa msongo wa mawazo mapigo ya moyo huongezeka kasi na pumzi inakua nzito kuliko kawaida. Vitendo hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa sana upungufu wa vimiminika vya mwili hivyo kunywa maji kwa wingi kunasaidia kutunza vimiminika vilivyopo mwilini hasa wakati ambapo mtu anakua na msongo wa mawazo.

Ieleweke kuwa msongo wa mawazo unaweza kusababisha upotevu wa maji mwilini, na upotevu wa maji mwilini pia unasababisha msongo wa mawazo. Ni matatizo yanayotegemeana. Haya yanaepukika kwa kunywa kiwango cha kutosha cha maji. Baadhi ya matatizo yanayotokana na msongo wa mawazo ni yale yale yanatokana na upungufu wa maji mwilini. Matatizo haya ni kama vile kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo,maumivu ya kichwa, kichefuchefu na hata uchovu. Kwa hiyo, unywaji maji kwa wingi unapunguza madhara ya kisaikolojia yakiwamo msongo wa mawazo na hasira.

Nitajuaje kama nina upungufu wa maji mwilini? Hili ni swali ambalo wengi linawasumbua ili kujua ni wakati gani mwili unaashiria kuhitaji maji. Kiu ni ishara ya kwanza kabisa inayoashiria kuwa mwili unahitaji maji. Hivyo kama unahisi kiu, tayari una upungufu wa maji. Pili fuatilia kwa makini unapoenda haja ndogo. Sote tunaifahamu rangi halisi ya mkojo. Lakini ile rangi ya mkojo ikionekana kuwa nzito zaidi kuliko ya kawaida, basi ni dhahiri una upungufu wa maji mwilini. Lakini pia mkojo ukitoa harufu kali sana unaashiria upungufu wa maji mwilini. Kadri mkojo unavyozidi kubadilika rangi kuwa iliyoiva zaidi na kuwa na harufu nzito zaidi, ndivyo inavyoashiria upungufu wa maji mwilini.
Unywaji wa maji kwa wingi ni changamoto kwa walio wengi. Pamoja na umuhimu wake kwa afya lakini bado wengi hawana utamaduni wa kunywa kiwango cha kutosha cha maji kila siku. Hivyo kutambua wakati sahihi hasa wa kunywa maji kutasaidia kunywa maji ya kutosha.

Usisubiri hadi uhisi kiu, unashauriwa kunywa angalau lita moja asubuhi baada ya kuamka na kabla ya kula chochote kile. Haijalishi yawe ya moto au ya baridi ilimradi yawe safi na salama.
Pia kwa kuwa wengi wanapenda kunywa maji wakati chakula, inashauriwa maji yanywewe angalau kuanzia nusu saa baada ya mlo ili kupisha mmeng’enyo wa chakula. Kwa kufanya hivyo, utakunywa maji mengi zaidi kuliko kunywa ukiwa unakula chakula.

Na Chris Peterson
Barua pepe: sonchrispeter@gmail.com
Simu: 0755-060 788

1851 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!