Na Aziza Nangwa

DAR E S SALAAM

Zaidi ya wakazi 1,000 wa Kijiji cha Pugu Kinyamwezi wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia jirani yao, Frida Keysi, kuishi kwa amani baada ya eneo lake kuvamiwa mara kwa mara na watu wenye silaha. 

Ombi hilo wamelitoa baada ya mtu mmoja anayedaiwa kuvamia eneo hilo kuwatishia watu walionunua viwanja kwa Frida wahame na kuwavunjia kwa nguvu.

Mmoja wa majirani wa eneo hilo, Rashidi  Kirumbi, amesema anamfahamu Frida kwa muda mrefu tangu mwaka 1990 alipokuwa akiishi na watoto wake kama mmiliki wa eneo hilo.

“Nakumbuka nikiwa ninasoma niko shule ya msingi miaka ya ‘90 mama huyo alikwenda kwa baba yangu mzazi na kumuomba amuuzie sehemu ya eneo letu, mzee alifanya hivyo, akamuuzia  kihalali hata serikali ya kijiji na mtaa inamjua,” amesema Kirumbi.

Amesema eneo hilo ni la Frida tangu akiwa mdogo kwa sababu baba yake alishiriki kumuuzia baadhi ya eneo katika sehemu ya ekari 20.

“Nimezaliwa hapa mwaka 1961, nimesoma eneo hili na ninawajua watu wengi, akiwamo mama Frida kama mjane, amekuwa akiwalea watoto wake kwa kutumia kipato cha kazi na biashara za kuku na zingine, kwa kweli serikali ilione hilo imsaidie kupata haki yake,” amesema Kirumbi.

Salma Mohamed ambaye naye ni jirani wa Frida anasema yuko katika eneo hilo tangu miaka 20 iliyopita na alipofika katika eneo hilo akamtambua kwamba ndiye mmiliki halali wa sehemu hiyo na Shabani hamjui. 

“Kwa kweli mama huyo anataka kudhulumiwa  eneo lake na hakuna hata mtu mmoja ambaye hamjui Frida kuwa ndiye mmiliki halali wa sehemu hiyo.  Watoto kwa wakubwa wanamjua,” amesema Salma.

Mchungaji wa kwanza wa kanisa hilo, Lazaro Samweli, amesema eneo hilo ni la Frida na aliligawa kwa ajili ya Mungu ili lijengwe kanisa. 

Amesema Frida alitoa eneo hilo la sehemu ya shamba lake kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na akawajulisha waumini wote ndipo wakaanza ujenzi huku shamba lake likiwa na miche mbalimbali.  

“Wakati nikiendelea kuishi katika eneo hilo huyu mama bado alikuwa ana eneo kubwa tu, mimi nikamshauri alizungushie uzio kwa sababu watu walikuwa wakivamia mara kwa mara kutafuta kuni,” amesema Samweli. 

Kuhusu eneo la Frida kuvamiwa, amesema yeye kama mtumishi wa Mungu anayelijua kwa miaka mingi ni kwamba Shabani alikuwa ni mmoja wa wavulana waliokuwa wakipitapita kuomba kuokota kuni. 

Amesema anashangaa kuona Shabani anadai hilo eneo la Frida ni lake na yuko tayari kumtetea popote akihitajika. 

“Nikiwa mchungaji kipindi cha nyuma walikuja watu kutaka niuze eneo hilo, niliwatoa mbio, sikupenda kufanya hivyo, kwa sababu yule mama ni mwema kwangu na kwa waumini wote wa kanisa kutokana na kujitoa kwake kwa Mungu na kwetu,” amesema Samweli.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Kata ya Pugu, John Malima, amesema suala la Frida analifahamu kuwa ndiye mwenye sehemu hiyo, lakini alitokea Shabani kulalalamika katika ofisi yao kuwa amevamiwa.  

“Baada ya kuja hapa Serikali ya Mtaa alipotoka alikwenda moja kwa moja Kituo cha  Polisi Chanika kushitaki kwamba shamba lake limevamiwa,” amesema.

Malima amesema polisi walimkamata Shabani kisha wao wakaahirisha kesi baada ya mtuhumiwa kuwa kizuizini.

Amesema baadaye Shabani alitolewa kwa dhamana na tukaendelea na kesi  na Frida aliitwa mara mbili kuja ofisini lakini hakuja. 

Kutokana na Frida kutokwenda wakasikiliza kesi upande mmoja na waligundua Shabani ana haki ya kumiliki sehemu ya eneo hilo kwa sababu hawakupata ushirikiano.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Pugu Kinyamwezi, Kassim Mfinanga, amesema anaufahamu mgogoro huo kwa kuwa ulianzia ofisini kwake baada ya Shabani kwenda kudai kuna sehemu katika shamba analomiliki limevamiwa na Frida.

Amesema kwa sababu ofisi yao haina mamlaka makubwa ndipo wakaenda moja kwa moja eneo la tukio kuona jinsi anavyodai Shabani.

“Mimi kiukweli nalijua eneo lile kwa miaka mingi kwamba ni la Frida kwa sababu ofisi yangu hata nilipokuwa sipo ilishiriki kuhakikisha mama yule ananunua eneo lile kihalali.

“Nilipokuja kushika madaraka nilimtambua Frida kama mmiliki wa eneo hilo na nilishiriki pia katika kuhusishwa katika mauzo aliyokuwa akiyafanya kuuzia watu vipande katika shamba lake,” amesema.

Mfinanga amesema anachoshangaa ni kwamba kuna mmiliki mpya anaitwa Shabani ambaye anamiliki baadhi ya viwanja katika shamba la Frida.

“Sisi kama viongozi tuliwaita watu wote walete  vielelezo vyao lakini mwishowe tuliona eneo lile mmiliki halali ni Frida kutokana na nyaraka na ushahidi wa watu walioko katika maeneo hayo na nyaraka halali za leseni,” amesema.

Mfinanga amesema baada ya hapo aliona kuna umuhimu wa kesi hiyo kusonga mbele kutokana na pande zote mbili kutoelewana na waliipeleka kata na wao wana hati ya hukumu ya kata inayodai kwamba Frida hakuhudhuria katika wito kwa hiyo walitoa uamuzi upande mmoja.

Pia amesema baada ya kuletewa nakala ya hukumu kutoka kata yenye kutoa uamuzi kuwa katika ekari 20, mbili na nusu ni za Shabani, siku hiyo hiyo akampigia simu Frida kumweleza ikiwezekana akate rufaa kwa kuwa hazikuwa zimefika siku 40.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni, Frida, amesema alikwenda katika kijiji hicho mwaka 1982 na ilipofika mwaka 1986 alibahatika kununua eneo la shamba la ekari 20.

Amesema alinunua eneo hilo ili ajiendeleze kiuchumi na kumudu kuwasomesha watoto wake na wakati huo alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Kilitex na kuanza ufugaji.

Frida amesema aliwekeza katika kilimo na ufugaji baada ya kununua eneo hilo na majirani zake walikuwa wakimjua kwa biashara hiyo. 

“Niliponunua eneo langu sikuliacha hivi hivi, niliamua kulisajili ili kuliendeleza kwa kujenga nyumba zaidi ya moja, huku nikijishughulisha na kilimo katika eneo langu. Niliweka wafanyakazi  waweze kunisaidia katika kulifanyia usafi na kilimo, nilifanikiwa kufanya hivyo,” amesema.

Frida amesema eneo hilo analimiliki kwa miaka yote bila kuwa na shida hadi ikafikia hatua ya kuligawia kanisa na kuanza kujenga kanisa.

“Ilipofika Januari mwaka 2021 ndipo alipotokea  kijana anaiyeitwa Shabani Kapelele na timu yake. Walivamia kiwanja changu namba 458, kitalu ‘B’ chenye ukubwa wa mita za mraba 42,054 kilichopo Kata ya Pugu Mwakanga,” amesema.

Pia amesema eneo hilo alilinunua kwa Rashid Mmbonde mwaka 1986, ambaye ametoa ushirikiano katika mgogoro huo na alipoitwa Kituo cha Polisi Chanika akaenda kutoa maelezo yake na hata kwa Takukuru alitoa ushirikiano.

Amesema kadiri miaka ilipokuwa inazidi kuongezeka na mahitaji ya ardhi kuwa makubwa kwa watu, aliamua kuuza baadhi ya eneo lake kwa kukata vipande.

“Katika kuvikata viwanja na kuviuza kihalali nilikuwa nawashirikisha mamlaka husika za serikali,” amesema. 

Katika ukataji wa viwanja hivyo, amesema alifanikiwa kukata eneo lake na kuligawa kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Shekemu Ministry Pugu mwaka 2012.

Frida amesema kwa sasa uvamizi huo unamkosesha usingizi kwa kuwa amekuwa akitishiwa amani na Shabani na walionunua eneo lake wanabomolewa.

“Niliitwa Baraza la Ardhi la Kata ya Pugu Kajiungeni, baada ya Shabani kufungua kesi huko lakini kabla ya kwenda tulikwenda kwa Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wizara ya Ardhi ili kuomba ushauri na kutoa malalamiko ya uvamizi wa eneo langu.

“Kamishna alitushauri tuombe Baraza la Kata litupe barua inayotuhamisha kwenda Baraza la Wilaya ya Ilala, maana ndio wenye mamlaka ya kusikiliza kesi yetu kisheria. Tulipopeleka maombi katika baraza hilo na maelekezo ya kamishna tuliambiwa tusubiri tutapewa barua,” amesema.

Frida amesema: “Kilichokuja kutokea si barua tena, bali hukumu iliyompa Shabani eneo nililokuwa nimewapa kanisa mwaka 2012 na robo tatu ya ekari moja ambayo tayari nilishauza kama viwanja kwa watu akaivamia.” 

Amesema alimjulisha kamishina wa ardhi kilichotokea na akamshauri akate rufaa katika Baraza la Wilaya ya Ilala.

“Nilifanya hivyo kupitia wakili wangu na Septemba 22, mwaka jana uamuzi ya Baraza la Kata ulifutwa rasmi. Kipindi tulipokuwa tunaendelea na taratibu za uendeshaji wa kesi ya rufaa katika hali isiyokuwa ya kawaida Shabani akaanza kukata viwanja katika eneo langu na kuanza kuviuza,” amesema. 

Pia amesema uvamizi huo umesababisha baadhi ya waumini wa kanisa hilo kuanza kupigwa na Shabani na kikundi chake hasa pale anapopeleka wateja na waumini wanakwenda kuwaambia wateja kwamba eneo hilo haliuzwi.  

“Kwa sasa sina raha kwa sababu niliowauzia wameshambuliwa na kukatwa mapanga na katika kanisa walipoweka uzio wa nguzo katika eneo lao, Shabani alikuja usiku akazing’oa zote na kuondoka nazo,” amesema.

Frida amesema kutokana na hofu ya usalama, waumini wengi wamekimbia kanisani hapo baada ya kukosa msaada kwa kuwa mamlaka husika inamwogopa mvamizi huyo.

Pia amesema Shabani anaendelea kumtolea vitisho vya mauaji mtoto wake hata baada ya zuio kuwekwa.

“Kwa sasa watu waliopo katika eneo langu wamekuwa wakikutana na vurugu isiyo ya kawaida, inayosababisha watu kushikiana mapanga.

“Eneo la awali alilodai Shabani ni la kwake wengi wametishiwa maisha na waliovunjiwa na waliopata usumbufu wameripoti matatizo haya Polisi Chanika lakini hawajapata msaada.

“Tuliwahi kupeleka malalamiko yetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, maelekezo yake yalikuwa ni kuitwa Takukuru na kutoa maelezo yetu juu ya kadhia hii. Lakini pamoja na hayo kufanyika  hatuoni hatua zikichukuliwa kwa sababu usumbufu ndiyo umezidi maradufu,” amesema.

Kwa upande wake, Shabani, akizungumza na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni amesema alimpeleka Frida Serikali ya Mtaa kisha akamshinda.

“Eneo ambalo Frida anasema ni la kwake na mimi nasema ni la kwangu, maelekezo ya Serikali ya Mtaa yalitutaka twende baraza la kata, nako nikaenda – nikamshinda, kwa sababu wao hawakuja, walikaidi, nikapewa ushindi.

“Tulipofika baraza la kata aliitwa akakaidi kuja na mwishowe akaniitia polisi eti sababu nimemtapeli shilingi milioni kumi kwa kigezo nimemuuzia yeye, lakini kuna mtu ametokea anasema ni eneo lake,” amesema.

Shabani amesema polisi walimwambia alete hati ndani ya siku mbili kama amemuuzia lakini hakutokea tena hadi akatolewa kwa dhamana.

“Nilikaa polisi baada ya siku tatu nikatolewa nikarudi baraza la kata nikapewa wito mwingine mara nne kumpelekea Frida lakini hakuja, kwa hiyo walisikiliza kesi upande mmoja, likanipa ushindi,” amesema.

Shabani amesema baada ya hapo wakakata rufaa kwenda Baraza la Kata la Wilaya na wakatakiwa kuzungumza ukweli wao na walidai hawakutendewa haki katika baraza la kata ndipo wakamshitaki na kumfungulia kesi namba 29 ya rufaa na kesi namba 108 ya uvamizi. 

By Jamhuri