Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, amesikiliza kilio cha wananchi na kuanzisha mchakato kufuta Tangazo la Serikali Na. 28 la mwaka 2007 lililoweka mpaka mpya kati ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wananchi wakazi wa Wilaya ya Mbarali.

Februari 27, mwaka huu ilikuwa siku ya pekee kwa wakazi wa Wilaya ya Mbarali, RC Makala na viongozi walipohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa katika Kata ya Imalilo-Songwe ukahudhuriwa na mamia ya wakazi wa Mbarali.

Matukio ya wazee na kina mama kububujikwa na machozi, huku wengine wakichangia kwa hisia kali baada ya kupewa fursa ya kueleza kero zao, yalimfanya Makala kusema: “Mimi ni mtu mzima, nimeona kigingi kilipo ni mjini kabisa… Kwa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Mkoa, ambaye ni mimi ndiye aliye karibu zaidi na Rais. Nimesikia, Rais Magufuli ni msikivu, nawaomba mnipe nguvu… Rais Magufuli ndiye mwenye uamuzi na mamlaka ya kulifuta tangazo hilo. Kwa pamoja tuandae ujumbe tutakaomfikishia Mheshimiwa Rais, ambaye nina uhakika atalifuta tangazo hili ambalo ni kero.”

Makala amefika katika Kata ya Imalilo-Songwe akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya na kwenda moja kwa moja lilipo moja ya mawe ya mpaka wa Hifadhi ya Ruaha, ambalo kimsingi lipo katika makazi ya watu. Alipofika kwenye mkutano wa hadhara, amesema: “Tumekuwa na matatizo ya wananchi na Hifadhi ya Ruaha.

“Rais alisema tushughulikie migogoro bila kujali itikadi za vyama vya siasa. Na Rais alisisitiza kuwa uwezo wa kutatua migogoro na kero zinazowakabili wananchi ni moja ya vipimo vya uwezo wa kiuongozi kwa Mkuu wa Mkoa. Sasa ninyi mnataka mimi nitumbuliwe? Nasema mgogoro huu tunaumaliza na Mbarali inaendelea kuwa salama. Kama wapo waliojipanga kwa ajili ya siasa, hapa si mahala pake.”

Alitoa fursa ya wananchi kueleza kero zinazowakabili, na wachangiaji wote 11, wameeleza kero moja tu ya mgogoro wa mpaka kati ya TANAPA, kwa maana ya Hifadhi ya Ruaha na wakazi wa Wilaya ya Mbarali.

Abdulkarim Abbas, ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM (Kata), alikuwa mchangiaji wa kwanza. Amesema wakazi wa Mbarali hawaelewi nia ya Serikali maana tangazo lililotolewa na mipaka ikatanuliwa, vijiji vinne kati ya vitano kwenye kata yake vimeingizwa kwenye hifadhi. 

Abbas amesema tangazo hili la Serikali la mwaka 2008 (uhalisia ni la mwaka 2007), ingawa limebakiza baadhi ya vijiji – limechukua mashamba yanayotumika kuzalisha mpunga na mahindi, hali itakayowaua njaa hata wakibaki.

Bernard Malangi, yeye amesema TANAPA haikushirikisha wananchi katika kuweka mipaka mipya inayoviingiza kwenye hifadhi vijiji vilivyokuwapo Mbarali hata kabla ya uhuru, na akaeleza mshango wake: “Kila mwaka, mipaka ya TANAPA inaongezeka. Kuna nini hapa?”

Diwani (mstaafu), George Chaura, amesema kinachomshangaza ni kwamba Serikali imewekeza Sh milioni 730 katika mradi wa Mwendamtitu, kuwawezesha wananchi kumwagilia mashamba yao baada ya shamba la Mbarali kubinafishwa, hivyo akahoji iweje Serikali imewekeza katika miundombinu ya umwagiliaji, halafu mashamba hayo sasa imeyarudisha kwenye hifadhi zisikostahili kufanyika shughuli za kilimo.

Amesema wao wamewapokea wafugaji kutoka Ihefu, walioondolewa mwaka 2012, na sasa Mbarali ina ng’ombe wapatao 50,000 na kwa kufuata maelekezo ya Serikali wametenga maeneo ya wakulima na wafugaji, hivyo akahoji ikiwa vijiji hivyo vitaingizwa kwenye hifadhi chini ya mpaka mpya hao ng’ombe, wafugaji na wananchi watakwenda wapi?

Isaac Alfayo, amemwambia Makala kuwa kila kitu ndani ya Wilaya ya Mbarali kiko chini yake ikiwamo viwanda vya kuzalisha mchele vinavyolipatia Taifa chakula baada ya wakazi wa Mbarali kuwa wamevuna mashambani, hivyo akamtaka atamke palepale kwenye mkutano wa hadhara kuwa amelifuta tangazo hilo na wananchi wako huru kuendelea na shughuli zao.

Makala alimjibu kwa kusema kuwa mwenye mamlaka ya kufuta tangazo hilo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli, ambaye ndiye mmiliki wa ardhi yote nchini. Huku wakionekana kujirudiarudia kwa hoja ile ile ya mpaka wa Hifadhi ya Ruaha, Zaire Mwanda, alishangiliwa kupita kiasi, aliposema: “Mkuu wa Mkoa tunaomba utamke kuwa TANAPA Mbarali basi inaondoshwa.”

Mzee Shaban Olelenganaro, ameteka hadhira na kuwafanya watu kutokwa machozi, pale aliposimulia kwa lafudhi ya Kimaasai kuwa tangu enzi za mkoloni, mpaka umekuwa ng’ambo ya mto Ruaha na katika miaka ya 1950 walikuwa wakiyaona mawe ng’ambo ya Mto Ruaha, sasa anashangaa kwa nini yamevushwa hadi katika vijiji vya Kata ya Imalilo-Songwe.

Amesimulia historia ndefu ya ukaazi wao katika Wilaya ya Mbarali na kusema baadhi ya watu wametolewa katika eneo la Ihefu na kuletwa Mbarali, ila sasa mipaka mipya inawaondoa kuwapeleka kusikojulikana. “Zamani sisi na TANAPA tulikuwa marafiki. TANAPA walituchangia hadi Sh milioni 3 kwa ajili ya shughuli za maendeleo kama madarasa… leo TANAPA anageuka adui? Kwa nini?

“Hivi, haya mashamba mnayotaka kuchukua watu wana mikopo benki. Sekondari watoto wameshindwa ajira pekee ni kilimo hapa Mbarali kwani Serikali haina ajira. Mnataka twende wapi? Leo hata mkitaka twende mashamba ya [Mbarali ya Mbarali Estate Haroon] Mulla Mbunge haitatutosha,” amesema mzee huyo na kisha akapiga magoti huku akitokwa machozi na kusema: “Chonde chonde baba, chonde chonde…” Karibu kila aliyekuwa kwenye mkutano huu alitokwa machozi kwa tukio hili.

Baada ya kuonekana kama hali ya hewa imechafuka, Mbunge wa Mbalali, Mulla, ameomba nafasi kuchangia hoja kama mwakilishi wa wananchi, na akasema: “Kwanza nijiondoe hapa kwenye meza kuu, niende huku kwa wananchi. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, hili tatizo ni kubwa. Tumekwenda kwenye jiwe pale umeona. TANAPA wanasema wanazuia vyanzo vya maji, kuna chanzo gani cha maji [pale]? (wananchi wakashangilia).”

Mbunge Mulla amesema suala la mgogoro wa mipaka mipya lililoanzishwa na Tangazo la Serikali Na 28 amekwishalifikisha ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Maliasili na Utalii, bungeni na ofisi mbalimbali za Serikali kuomba upatikane ufumbuzi kwa kurejesha mpaka katika eneo la awali ambalo ni ukingo wa Mto Ruaha, lakini kumekuwapo ugumu asiofahamu unatokana na nini.

Mzee Sperwa Kashu, yeye amerejea historia ya kabla ya Uhuru na kusema kuwa yeye ameishi Mbarali kabla ya mwaka 1952. Amesema enzi za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Basil Mramba, walisema Ihefu inaharibiwa na mifugo wakahamisha wafugaji na katika kuepusha mgogoro, Serikali ilisema watenge maeneo ya wakulima na wafugaji. “Walisema magari hayana mafuta, tukatoa hela wakaweka mafuta na kuchora ramani,” amesema.

Amesema walipokea wageni waliohamishwa kutoka maeneo mbalimbali, ila akaonya kuwa TANAPA isipoangalia inaweza kujikuta inacheza mchezo wa wakoloni waliokuwa na ramani nyingi. “Michoro ya mkoloni alikuwa na nia ya kutufanya watumwa,” amesema mzee Kashu na kufafanua kuwa mkoloni hakutaka kuona Waafrika wakijitegemea kwa chakula au chochote hivyo kila walipojaribu uzalishaji, alianzisha jambo jipya na kuwafukuza.

Mzee huyu amesema wamepata kwenda na Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete hadi Madibila kuangalia namna ya kutatua mgogoro huu, lakini bado hali imeendelea kutoeleweka. Anasema kuanzia Dodoma Hifadhi ya Ruaha inapoanzia mpaka Mbarali ni mbali kiasi kwamba ukiamua kutembea umbali wa hifadhi hiyo ni lazima viatu viishe na watoto wabebwe na punda. “Hiyo Ruaha bado haitoshi? (akashangiliwa).”

Anasema siku nchi inapata Uhuru, katika Kata ya Rujewa Mbarali wazee walizimia siku bendera ya mkoloni iliposhushwa kupandisha Bendera ya Tanganyika, hivyo akashagaa Uhuru gani ulipatikana ikiwa TANAPA sasa inawaingilia hadi kwenye vijiji vyao vya asili? “Tulitoa ng’ombe sana hapa kwenda Msumbiji katika vita ya ukombozi na vita ya Kagera. Wananchi wamezaliana baada ya Uhuru, leo mnatuondoa twende wapi?”

Habib Seif, amesema hata wananchi waliolipwa fidia ambao vijiji vyao vimeingizwa kwenye Hifadhi ya Ruaha katika Kata ya Msangaji baadhi walikuwa wanaandikiwa fidia ya Sh milioni 5, lakini wanaambulia 50,000: “Uonevu ulikuwa wa hali ya juu. Watu wametapeliwa. Mtu anaandikiwa fidia Sh milioni 5, anawekewa noti za Sh 500 kwenye bahasha na kuambiwa atafungulia nyumbani, akifika nyumbani anakuta ana Sh 50,000, kwa hasira wakazimalizia baa.”

Diwani wa Viti Maalum, Turket Kashu (CCM), amesema mpaka mpya uliotangazwa na TANAPA hauwatendei haki wananchi kwani wakazi wa Imalilo-Songwe wamepokea watu waliohamishwa eneo la Msanga, ambapo watoto wao waliacha shule, leo tena wanataka kuwahamisha wakazi wa Imalilo-Songwe waliokaa hapo kabla ya Uhuru? “Hata kama ni Ilani ya CCM tunaomba ipelekwe bungeni irekebishwe.”

Diwani Chuki Jeremiah (Chadema) amesema kwa hali ilivyo Serikali pekee ndiyo yenye uwezo wa kumaliza mgogoro huo kwa kuondoa vigingi vilivyowekwa kwenye makazi ya watu na kuurejesha mpaka ng’ambo ya Mto Ruaha.

Kata zinazoathiriwa na mabadiliko hayo ya mpaka ni Luhanga, Mapogoro, Imalilo-Songwe, Rujewa, Igava, Miyombweni, Madibira, Itamboleo, Kongolo-Mswiswi, Utengule-Usangu na Mwatenga. Hifadhi ya Ruaha ikiwa tangazo hili halitarekebishwa itamega wastani wa hekta 10,000 sawa na ekari 25,000 kutoka katika Wilaya ya Mbarali na kuwa sehemu ya Hifadhi hiyo.

Katika majumuisho, RC Makala amesema: “Wote mmeongea kwa hisia kali si za kishabiki, bali kutoka moyoni. Mimi ni mtu mzima, nimeelewa.” 

RC amewataka wananchi kutokuwa na ugomvi na TANAPA kwani kuna watu wanaweza kudhani ni taasisi ya watu binafsi kama NGO, lakini ukweli TANAPA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na ni idara inayoliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni hivyo wananchi hawana sababu ya kugombana nayo.

Makala amesema wapo wanasiasa waliokuza mgogoro huu kwa kuwaambia wananchi kuwa tatizo limekwisha wakati bado lipo bila kufuata taratibu sahihi za kulimaliza. Amesema ndani ya miezi minane amepata Sh milioni 362 na kuwalipa fidia wakazi wa Msagali waliokuwa wamepunjwa, hivyo akawahakikishia wakazi wa Imalilo-Songwe kuwa tatizo lao litaisha.

Amesema tangazo la Serikali Na 28 ndilo lililoleta mtafaruku. “Leo nimekwenda kuangalia lilipowekwa jiwe. Wanyama wanaingia mpaka pale?” amehoji Makala na kushangiliwa, huku wananchi wakiitikia, “Hapanaaaaa”.

“Hayo mawe yaliyowekwa yasiwasumbue. Tangazo la Serikali linafutwa na tangazo jingine la Serikali. Na hilo halitafika bungeni,” amesisitiza. Amewaambia kuwa Machi 29, atapokea taarifa ya Kamati ya Wataalamu na baada ya hapo: “Mtoe ushirikiano wa kutoa maoni. Nimewaomba na niwatoe hofu, endeleeni kuishi. Nimeunda kikosikazi kitapita kuchukua maoni. Nataka na mimi mnikumbuke kuwa kulikuwa na mgogoro na Makala aliumaliza… Hapa Kazi Tu (akashangiliwa).”

Amesema watu wanahamasishwa kufanya kazi, hivyo lazima wapatiwe ardhi walime na huu si wakati wa kuwanyang’anya ardhi wananchi. Amemtaka Mzee Kashu kusaidia kuzuia wimbi la mifugo kutoka kwa wafugaji wa maeneo mbalimbali nchini ambao kwa sasa wengi wanafurika kuelekea Mbarali.

“Nitashiriki kijiji kwa kijiji. Nimetatua migogoro mingi. Mimi mgogoro huu na mimi nataka niwe sehemu ya kuumaliza,” amesema Makala.

Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, akiwa wilayani Mbarali, aliyekuwa mgombea wa CCM na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, aliahidi kumaliza mgogoro huo na kuwahakikishia wananchi kuwa kwa kila hali angeshinda watabaki katika maeneo yao. Rais Magufuli alishinda na sasa ndiye Rais wa Tanzania.

Mgogoro huu uliodumu tangu mwaka 2007 mwishoni, umedumaza shughuli za maendeleo na wananchi hawana uhakika kama wataendelea kuwapo au wataondolewa kwani mawe ya mpaka yamekwama katikati ya makazi yao. Mbunge Mulla anasema suluhisho pekee la kurejesha amani kwa Wanambarali ni kuondoa mawe hayo na mpaka kurejea kwenye kingo za Mto Ruaha kama ilivyokuwa zamani kabla ya tangazo Na 28 la Serikali.

By Jamhuri