DODOMA
Editha Majura
Rais Dkt. John Magufuli ameagiza wanaoishi maeneo ambayo hayajapimwa, washirikiane chini
ya uongozi wa mitaa yao kupanga, kutafuta kampuni za kuwapimia makazi hayo ili kila mmoja
apewe hati ya kumiliki ardhi yake.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Dkt.
Magufuli ameridhia hatua hiyo ambayo imefikiwa baada ya kubaini uwepo wa watu wengi mijini,
ambao wanahitaji kupata hati hizo lakini wanakosa kutokana na kujenga maeneo yasiyopimwa.
Waziri Lukuvi amesema hayo kupitia kituo kimoja cha luninga, wakati akizungumzia
yaliyobainishwa na mpango wake wa kuzungumza na wananchi ana kwa ana, ili kusikiliza na
kupatia ufumbuzi malalamiko yanayohusu migogoro ya ardhi.
Amesema imethibitika kuwa zaidi ya asilimia 65 ya migogoro ya ardhi nchini imesababishwa na
baadhi ya watumishi wa umma, katika sekta ya ardhi kukosa uadilifu.
Waziri Lukuvi amesema kwa upande wa mijini, pamoja na kuwapo tatizo la kiwanja kimoja
kumilikishwa kwa zaidi ya mtu mmoja (double allocation), wananchi hawana hati za kumiliki
makazi yao kwani wamejenga holela, bila kuzingatia taratibu za mipango miji.
Hata kiini cha kuwapo ujenzi holela kimetajwa na waziri huyo kwamba ni kutokana na manispaa
na halmashauri kuwa na kasi ndogo ya kupima ardhi na kuimilikisha kwa wananchi.
Endapo fursa inayotokana na ridhaa ya Rais Magufuli ikitumiwa vizuri, imeelezwa na Lukuvi
kuwa inaweza kuwa suluhisho la changamoto hiyo.
“Mheshimiwa Rais (Dkt. Magufuli) amekubali kuanzia mwaka huu wananchi wanaoishi maeneo
yasiyopimwa, kwa ushirikiano wao ndani ya mitaa yao watafute kampuni, wapange maeneo yao
ili wamilikishwe na kupewa hati ambazo zitawasaidie kuimarisha uchumi wao,” amesema Waziri
Lukuvi.
Pia, amewataka viongozi wenzake katika sekta ya ardhi, kuhudumia wananchi kwa kuzingatia
sheria na wasisababishe mateso kwa sababu wameteseka kwa miaka mingi, sasa imetosha.
“Wito wangu kwa viongozi wenzangu, kweli tumeanza kubadilika lakini tubadilike zaidi, wala
tusiamue masuala ya ardhi kwa utashi na kwa matakwa yetu binafsi; watendaji wa Serikali
nawaonya tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia sheria,” amesema Waziri Lukuvi.
Sambamba na hayo, amesema mifumo ya utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya ardhi kwenye
ngazi za vijiji, kata na hata mabaraza ya ardhi ya wilaya yamebainika kuwa na upungufu.
Ili kuondoa upungufu huo, amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
imeandaa marekebisho ya sera ili iwe yenye mfumo mmoja, utakaowezesha kuondoa upungufu
uliobainika.
“Kuna baadhi ya kata mtu akipeleka malalamiko kwenye mabaraza ya ardhi wajumbe
wanamwangalia usoni mpaka miguuni, wakiona umevaa kandambili wanajua ‘huyu hana hela
ya kutupatia’, kinachofuata hapo ni kilio tu,” amesema waziri.
Akizingumzia kuhusu aliyoyabaini mkoani Kagera, katika wilaya za Karagwe na Kyerwa, Waziri

Lukuvi amesema kutotekelezwa kwa mpango wa kutenga ardhi kwa ajili ya wafugaji na
wakulima, kunachangia migogoro katika maeneo hayo.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni matumizi mabaya ya ardhi, ikiwamo watendaji wasio
waadilifu kuruhusu wageni kumiliki au kutumia ardhi kinyume cha taratibu na sheria za nchi.

By Jamhuri