Transfer ni kubadilisha hati au leseni ya makazi kutoka jina la mmiliki wa awali kwenda kwa mmiliki mpya. Transfer inaweza kufanyika kutokana na mauzo, kupewa zawadi, fidia, n.k.
Kwa hiyo, kuzuia transfer ni kuzuia kubadilishwa kwa hati kutoka mmiliki wa awali kwenda mmiliki mpya. Mara nyingi tumezoea kuzuia transfer kwa kutumia Mahakama (court injunction).
Sasa yatupasa tufahamu kuwa ipo njia nyingine nyepesi ambayo haihusishi Mahakama. Ni njia ya maombi kwa Kamishna wa Ardhi kwa mujibu wa Sura ya 113, Sheria ya Ardhi, namba 4, ya mwaka 1999 vifungu vya 38, 39 na 41.
Kabla ya kuona ufanyeje kutumia njia hii, ni vema tuone mazingira ambayo yakikutokea unaweza kutumia hiyo njia.

1. Haya yakitokea unaweza kupeleka maombi kwa Kamishna;
a) Mume wako au mke wako ameuza kiwanja au nyumba yenu na kuna namna ambavyo mauzo hayo unadhani siyo halali kwa sababu yoyote ile ya kisheria pengine ya kutokushirikishwa, au kushirikishwa lakini baadaye kunyimwa haki yako kwa mujibu wa makubaliano au vinginevyo. Lakini wakati huo unadhani huna la kufanya kwa kuwa mauzo tayari yamefanyika na pengine hata wewe ulishasaini.
b) Una maslahi na haki katika nyumba/kiwanja cha mirathi. Mali hiyo imeuzwa bila wewe kushirikishwa au umeshirikishwa lakini haki zako za msingi hazikuzingatiwa au namna nyingine yoyote ambayo kwayo unahisi mchakato haukwenda sawa. Lakini wakati huo unadhani huna la kufanya kwa kuwa mauzo tayari yamefanyika na pengine hata wewe ulishasaini.
c) Umemuuzia mtu nyumba/kiwanja lakini amekataa kutekeleza baadhi ya makubaliano ya msingi yaliyo katika mkataba wenu wa mauziano na sasa anafanya mchakato wa kubadili hati.
d) Na mazingira mengine yoyote ambayo tayari nyumba/kiwanja kimeuzwa lakini ukaona kuna haja ya kuzuia mchakato wa kubadilishwa jina la mmiliki ili baadhi ya mambo yawekwe sawa kwanza.

2. Maombi kwa Kamishna
a) Utaandaa maombi maalumu kwa njia ya maandishi. Maombi utayaelekeza (address) kwa Kamishna wa Ardhi Tanzania.
b) Kichwa cha maombi kitakuwa ‘kuzuia kubadilishwa kwa umiliki wa nyumba/kiwanja namba.., plot namba…, title namba…’ Utaweka taarifa zote kama zinavyoonekana kwenye hati.
c) Utaeleza jina lako na wewe ni nani mpaka utake kuzuia ubadilishaji wa umiliki.
d) Utaeleza maslahi yako katika nyumba/kiwanja hicho kwa mfano mke halali, mkopeshaji, mrithi halali, mtia saini katika mkataba wa mauziano n.k.
e) Hakikisha unaambatanisha nyaraka zote muhimu kama kopi ya hati kama unayo, cheti cha ndoa, mkataba wa mkopo, mkataba wa mauziano kama unao, hati ya usimamizi wa mirathi n.k.
f) Utaeleza ni kwa vipi utaathirika ikiwa zuio lako halitakubalika na hivyo transfer kuendelea na hatimaye kuhamia jina la mmiliki mpya.
g) Utaandika jina lako na utasaini, kisha utakwenda ofisi za ardhi na kuuliza ofisi ya Kamishna wa Ardhi ilipo na hapo utaacha maombi yako.
h) Pia wakati mwingine kutokana na uharaka wa jambo ni muhimu kuhakikisha unamuona Kamishna wa Ardhi na kumueleza tatizo lako moja kwa moja.

3. Faida za njia hii dhidi ya ile ya Mahakama.
Haina gharama kubwa, ni nyepesi, haichukui muda mrefu, hatua na mchakato wake ni za kueleweka zaidi, kwa ufupi njia hii ni bora zaidi kuliko ile ya Mahakama.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

Dar es Salaam,
Na Bashir Yakub

0784 482959
[email protected]

By Jamhuri