Mapya yamfika Muhongo

Mambo hubadilika ghafla. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anatarajiwa kuhojiwa na vyombo vya usalama leo kutokana na sakata la mchanga wenye madini.

Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI zimethibitisha kuwa Prof. Muhongo atahojiwa kuhusiana na ripoti ya uchunguzi  wa mchanga wa madini, ambao umekuwa ukisafirishwa nje ya nchi kwa makontena tangu mwaka 1998.

Muhongo anahojiwa kutokana kushindwa kusimamia Sera ya Madini inayoelekeza kuwa Serikali itawekeza katika kiwanda cha kuchenjua mchanga kutenganisha madini ya dhahabu, copper (shaba), chuma na mengine ndani ya makenikia (mchanga) yanayobebwa kwenye makontena.
Pia upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali katika ukokotoaji wa mrabaha.

Kamati ya Uchunguzi imeitaka Serikali iwachukulie hatua watendaji wa TMAA na wa wizara inayohusika ikiwa ni pamoja na wizara kushindwa kuisimamia TMAA, kujenga ‘smelter’ na kueshindwa kuweka utaratibu wa kufuatilia makinikia.

Vyombo vya ulinzi vimetakiwa kuwachunguza watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wanaoshughulikia madini, jambo ambalo limemweka matatani Prof. Muhungo na watendaji wake. JAMHURI limemtafuta Prof. Muhongo kupata kauli yake bila mafanikio.

Chanzo cha habari kimeeleza kuwa wiki hii vyombo vya dola vinatarajia kuhoji vigogo waliokuwa Wizara ya Nishati na Madini ambapo wataanza na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Paul Masanja.

“Unajua, tangu litoke agizo la Rais kazi ni kubwa. Tunafanya kazi kwa mapana mno. Wiki iliyopita tulianza kufanya mahojiano na baadhi ya wafanyakazi wa TMAA ambao bado tunaendelea nao. Lakini wiki ijayo (hii) tunaanza na aliyekuwa bosi wao hapo awali, Paul Masanja, atafuatia Prof. Muhongo, pia tutaendelea na wengine. Nakwambia hii kitu si ndogo kama unavyodhani,” amesema mtoa taarifa.

Amesema pamoja na kufanya mahojiano na vigogo hao, Meneja Uzalishaji na Usafirishaji wa TMAA, Injinia Jumanne Mohamed, aliyekuwa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam tayari amefika Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano.

“Huyu injinia hakuwepo hapa, lakini amekuja na anatakiwa kutueleza mambo mengi, maana huu uzalishaji na usafirishaji ni kitengo chake kinachohusika hivyo tutataka kujua wamekuwa wakitumia taratibu gani na mengine mengi,” amesema.

Pia amesema afisa mwingine wa TMAA ni Injinia Gilay Shamika, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uthamini wa Madini na Huduma za Maabara kwani kitengo chake kinahusika na upimaji wa madini.

Bunge laandaa tamko

JAMHURI limepata taarifa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipo katika mchakato wa kuandaa azimio la kuunga mkono hatua ya Rais John Magufuli kudhibiti madini ya nchi hii.

Vyanzo vya habari kutoka Ofisi ya Bunge vimeeleza kwamba Bunge linatarajia kutoa azimio la kumuunga mkono Rais Magufuli wakati wa kusomwa na kujadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Pamoja na azimio hilo, Bunge linajiandaa kujadili ripoti ya Kamati ya Kuchunguza Mchanga wa Madini iliyokabidhiwa kwa Rais wiki iliyopita.

“Bunge limejipanga kujadili ripoti hii ambayo imeibua mambo ya kuiumiza nchi, hivyo tunasubiri wakati wa kusomwa kwa hotuba ya bajeti ya wizara husika ili tuweze kufanya maazimio kwa ajili ya nchi yetu,” amesema mtoa taarifa.

Akizungumza na JAMHURI Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema Bunge ni mali ya Watanzania na wabunge wapo kuwakilisha wapiga kura wao ambao ni raia wa nchi, hivyo haliwezi kunyamaza kimya.

“Usiwe na haraka, vuta subira mpaka wakati wa kuwasilishwa na kujadili hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini ndiyo tutakuwa na jambo. Hili suala haliwezi kupita hivi hivi, na jambo jema limekuja wakati vikao vya Bunge vikiendelea,” amesema Ndugai.

Profesa Ntalikwa

JAMHURI limezungumza na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, kufahamu amepokeaje uamuzi wa Rais Dk. Magufuli kumuachisha kazi kwa sababu ya kudai mchanga haukuwa na dhahabu nyingi.

“Maamuzi yamekwisha kufanyika, Rais ana mamlaka ya kuchukua uamuzi wowote juu ya wateule wake na hakuna sababu za kuhoji. Naomba suala hili tuliache kwani sina cha kuzungumza juu ya hili,” amesema Prof. Ntalikwa.

Amesema haoni kama kuna sababu za kuendelea kuhoji juu ya hatua aliyoichukua Rais dhidi yake na wala si busara kuzungumzia tofauti ya ripoti ya TMAA dhidi ya Kamati ya Uchunguzi.

Akikabidhiwa Ripoti ya Kamati ya Uchunguzi wa Mchanga wa Madini Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema, “Wapo watu katika Wizara ya Nishati na Madini wanajiita maprofesa kumbe ni madokta.” Kutokana na kauli hiyo JAMHURI lilimuuliza Prof. Ntalikwa juu ya usomi wake.

“Mimi nimepewa uprofesa mwaka 2011 na nilipewa na Chuo Kikuu cha Dodoma. Baada ya kuchapisha tafiti zangu kwenye international journals ambazo ni pamoja na Ethiopian Chemical Society, Journal of Polima Science, na kadhalika. Siwezi kukumbuka yote hapa kwa sasa labda mpaka nikipitia mafaili yangu,” amesema Prof. Ntalikwa.

Amesema kuwa hadhi ya uprofesa ameipata kupitia utaalamu juu ya uchakataji madini – ‘Mineral Processing Engineering’.

Wataalamu wanena

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha  Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, amesema kitendo kilichofanywa na Rais Magufuli ni kitendo cha kijasiri kinachohitaji kupongezwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yake, lakini bado kuna maswali ya kujiuliza.

“Ni lazima kama Taifa tujiulize tumefikaje hapa tulipo. Je, tumefika kwa kujitakia au tumelazimishwa kufika? Na kama tumelazimishwa ni kwa faida ya nani? Hayo ni maswali magumu tunayopaswa kujiuliza kama Taifa,” amesema  Ngowi.

Amesema malalamiko ya Watanzania juu ya rasilimali hasa madini hayajaanza leo wala jana, bali yamekuwapo kwa miaka mingi iliyopita, lakini hakuna aliyethubutu kuhoji juu ya uhalali wa mchanga kutoka katika migodi kusafirishwa nje ya nchi.

“Mara nyingi wanaharakati, wanasheria wamehoji uhalali wa mikataba ya madini na rasilimali nyingine kuwa ya siri, lakini viongozi wameshindwa kutoa majibu ya kuridhisha na kuacha maswali yaliyokosa majibu hadi leo,” amesema Ngowi.

Amesema madudu yanayoonekana kipindi hiki ni matokeo ya ukosefu wa uzalendo wa viongozi waliokabidhiwa madaraka ya kuliongoza Taifa kuanzia miaka ya 1995 wakati wa Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa.

Amesema Tanzania isipokuwa makini katika kila hatua inayochukua kuanzia sasa, kuna hatari ya kujikuta ikishitakiwa katika mahakama za kimataifa na kulipa fedha nyingi kwa kuvunja mikataba iliyoridhia kwa kusaini.

“Ni lazima wataalamu wetu wawe makini sana katika kila hatua wanayochukua dhidi ya wawekezaji hasa katika sekta ya madini, vinginevyo tunaweza kujikuta tunashitakiwa na kushindwa kesi mwisho wa siku tukalazimika kulipa mabilioni ya fedha,” amesema Prof. Ngowi.

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini nchini, Dk. Peter Kafumu, amesema suala hili limefika katika hali ambayo ni muhimu vyombo husika vikaachwa vifanye kazi yake kuliko kuingiliwa na mamlaka nyingine.

“Suala hili tayari lipo ngazi ya juu sana. Nisingependa kutoa maoni zaidi ikaonekana napingana na mamlaka husika. Ninachowaomba Watanzania ni umakini na utulivu wakati huu vyombo vya ulinzi na usalama vinapofanya kazi waliyokabidhiwa,” amesema Kafumu.

Kamati ilipofuatilia utendaji wa TMAA, ilibaini kuwa imekuwa haifungi utepe wa kudhibiti makontena, jambo ambalo linatoa fursa ya watu kuchezea viwango.

Uwezo mdogo wa mashine za ukaguzi (scanner) inayoangalia yaliyomo kwenye makinikia ndani ya kontena, nalo limebainika kuwa tatizo.

“Mfano tulijaribu kuficha vipande vya chuma, scanner haikuona. Hivyo mtu akiamua kuficha vitu kwenye makinikia haviwezi kubainika,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kamati imependekeza kusitishwa kwa usafirishaji wa mchanga mpaka mrabaha stahiki utakapolipwa serikalini kwa kuzingatia thamani halisi ya makinikia.

Ripoti kamili soma ukurasa wa 3.

2156 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons