Hatima ya Stephen Masele kuendelea au kutoendelea kuwa mbunge katika Bunge la Afrika (PAP) inajulikana wiki hii.

Masele ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekaliwa vibaya kisiasa, na aliyeshika mpini kwenye vita hiyo ni Spika Job Ndugai ambaye naye anatoka katika chama hicho.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 40 kwa sasa ni Makamu wa Rais wa PAP; nafasi ambayo taarifa za ndani zinasema huenda ikafikia ukomo wiki hii endapo Ndugai ataendelea kuwa na msimamo mkali dhidi yake.

Wiki hii wabunge wataamua hatima ya Masele katika PAP baada ya kutakiwa ajieleze mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge; pia katika Kamati ya Wabunge wa CCM.

Mwanasiasa huyo anaitwa wakati ambao yuko kwenye mvutano mkali na Rais wa PAP, Roger Nkodo Dang, ambaye amekumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya madaraka na unyanyasaji wa kingono.

Hata hivyo, Spika Ndugai anasema kuitwa kwa Masele mbele ya kamati hizo hakutokani na mgongano wake na viongozi wenzake ndani ya PAP; badala yake kunatokana na kile alichosema ni uchonganishi wa Masele unaolenga kuvuruga mihimili ya utawala nchini.

JAMHURI limethibitishiwa kuwa miongoni mwa “vitendea kazi” vitakavyotumika kumbana Masele ni ujumbe mfupi wa maandishi (sms) aliokuwa akituma sehemu mbalimbali ukilenga kuleta “mgongano” kwenye mihimili.

Ujumbe huo unadaiwa kupelekwa kwa viongozi wa juu wa nchi ukilenga kulishambulia Bunge la Tanzania.

Mbele ya umma na hasa kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, Masele amejitengenezea taswira ya kusimamia haki dhidi ya Dang, lakini hapa nyumbani, na kwa mujibu wa Spika Ndugai, mbunge huyo amekuwa na mambo ya “hovyo hovyo” yanayochafua taswira ya nchi.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC mwishoni mwa wiki, Spika Ndugai hakutaka kueleza bayana mambo ya “hovyo hovyo” anayomtuhumu Masele, badala yake amewataka Watanzania wawe na subira hadi mahojiano yatakapomalizika.

JAMHURI limeelezwa kuwa kati ya hatua ngumu zinazoweza kufikiwa dhidi ya Naibu Rais huyo wa PAP ni kumfuta kwenye bunge hilo.

“Spika Ndugai amekwisha kueleza kuwa kuna ushahidi wa namna anavyogonganisha mihimili,” ameeleza mmoja wa wabunge wa Bunge la Tanzania na kusisitiza kuwa katika maelezo ya Spika bungeni kuna sentensi zenye kumhukumu Masele ingawa ametakiwa kwenda kuhojiwa kwenye kamati.

Spika Ndugai anasema katika uwakilishi wa PAP kumejitokeza matatizo makubwa hasa upande wa Masele.

“Kuna matatizo makubwa sana ya kinidhamu ambayo nisingependa kuyafafanua leo humu kiasi cha kutosha. Lakini tumelazimika kumtafuta Mheshimiwa Masele kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu (Mei 13, 2019). Badala yake amekuwa akigoma… kuna ‘clip’ zinaonyesha zimerushwa baada ya kumwandikia arudi nyumbani ili aje ahudhurie kikao cha maadili hapa, ameonekana akilihutubia bunge lile akisema japo ameitwa na Spika, Waziri Mkuu amemwambia a ‘disregard’ [apuuze] mwito wa Spika na aendelee na mambo yake kule, kitu ambacho ni uongo na kutudhalilisha kama nchi.

“Anapeleka kwenye mihimili ya Serikali, juu kabisa, maneno mengi ya uongo na ushahidi upo. Ni kiongozi ambaye amejisahau, hajui hata anatafuta kitu gani, ukiacha hizo vurugu ambazo hivi sasa zinaendelea kwenye Bunge ambalo analiongoza, ni kubwa. Hizo hazituhusu. Sasa kwa kuwa tumekuwa tukimwita tangu Jumatatu hataki kurudi, kwa niaba yenu [wabunge] na kwa mamlaka niliyonayo basi, nimemwandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi tuliompatia Masele katika Bunge la PAP hadi hapo Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kukamilisha taarifa yake,” Spika Ndugai alisema bungeni wiki iliyopita.

Awali, kumekuwapo taarifa kuwa Rais wa PAP, Dang, amekwisha kuchunguzwa na kubainika kukutwa na makosa ya unyanyasaji wa kingono kwa baadhi ya watumishi wa PAP.

Akizungumza na JAMHURI kuhusu tuhuma za Masele, Spika Ndugai amesema: “Yaani yeye atakapokuja Dodoma mambo yake yote atayakuta pale. Sasa kama hujafika unapoitwa kweli, kwa hiyo mambo yake yote atayakuta Dodoma yako vizuri yanamsubiria.

“Lakini ukweli ni kwamba alipelekekewa wito mara tatu. Alipelekewa yeye straight [moja kwa moja] kwake, including kwa kupewa notification ya whatsapp, [pili] kupitia ofisi yake, yaani kupitia ofisi ya PAP, kwa President [Rais], yaani akikabidhiwa kutoka kwenye ofisi ya PAP.

“Na President wa PAP akipewa nakala, na Katibu wa Bunge wa PAP akipewa nakala, lakini pia tulipeleka katika ubalozi wetu South Africa, kutusaidia kusema anaitwa nyumbani. Kwa hiyo hawezi kusema kwamba hakupata wito… hilo linaondoka, angle inayobakia sasa ni hiyo, kwamba kaambiwa na Waziri Mkuu ‘disregard’ [apuuze].

“Sasa unaposema maneno ya namna hiyo kwenye Bunge la Afrika, wapo watu wa nchi mbalimbali, kwamba nchini kwako Spika wako amekuita urudi, kwamba kuna mambo ambayo, maanake kwenye ule wito, sisi hatukuandika undani, tumeandika tu ni wito wa kurudi nyumbani haraka kushughulikia mambo muhimu, tukimlinda, ili watu wengine wajue anaitwa.

“Sasa yeye anasimama anasema nimeambiwa na Waziri Mkuu disregard, kwenye jumuiya kama ile unaonyesha nchini kwako kuna viongozi ambao hawaheshimiani, hawaelewani, na hata kwenye mahojiano yake mengine anasema government [serikali] ndiyo ina power… yaani kwa kweli hajitambui kidogo kijana wetu huyu.

“Kwa hiyo ndiyo maana tumefika mahala tukasema kwa kuwa anagoma [kurudi] tusitishe kwa muda huu ushiriki wake huko ili arudi, ambao na wenyewe ali-disregard pia,” alipoulizwa sasa Masele anaishi kwa gharama za nani nchini Afrika Kusini, Spika akasema:

“Ameisharudi, ameisharudi Tanzania. Ameisharudi, sasa sema kwa sababu ya hii weekend, matarajio yetu Jumatatu, maana nimesikia anasema anaumwa, anatakiwa afike. Tatizo lake ni tabia zisizokuwa za kiuongozi kwa kweli.

“Siyo kwamba tumekurupuka, tumeenda naye muda mrefu, mimi mwenyewe nikimwita, nikimkanya, nikimwelekeza, uongozi  hauendi hivi, usipende kuwa mchonganishi, mwongo mwongo. Sasa kama hili la Waziri Mkuu, amemwekea maneno mdomoni… sasa ina heshima gani hiyo kwa kiongozi unayejiita wewe kiongozi?”
Spika Ndugai alisema jana Masele alipaswa kuingia kwenye kamati aelezwe makosa yake, lakini akaonya iwapo angekataa kufika kwenye kamati hiyo: “Nimekwambia huyu mtu ni mtu wa kutelezateleza, kwa hiyo, let’s assume kwamba atafika. Sasa asipofika ndiyo tutakaa kikao kuamuru sasa kama aletwe chini ya ulinzi wa polisi, kitu ambacho kitamvunjia heshima zaidi.”

Kuhusu kashfa dhidi ya Dang, Masele alieleza kufurahishwa kwake na kazi ya uchunguzi iliyofanywa na kamati maalumu ya PAP.

Amesema ana wajibu wa kuhakikisha haki za wafanyakazi, hasa wanawake zinalindwa, ikiwa ni pamoja na kutonyanyaswa kingono.

“Utafiti umeonyesha rais ana kesi ya kujibu, tumekabidhi (kashfa dhidi yake) Umoja wa Afrika (AU) kwa uchunguzi wa kina. Ni utafiti wenye ushahidi, naye amekiri kwamba amefanya. Ameomba msamaha, lakini haitoshi, hatua zichukuliwe kukomesha tabia hii,” amesema Masele.

Mbunge mwingine wa PAP kutoka Tanzania, David Silinde, anamtetea Masele akisema yuko upande wake katika sakata hilo la kumchunguza Rais wa PAP.

“Mimi nitasimama na Masele na hili nitakuwa nalieleza, kwa sababu hakuna utovu wowote alioufanya na kama amefanya kwa nini asishughulikiwe na kamati za PAP hadi aitwe nyumbani (bungeni Tanzania)?” amekaririwa Silinde akihoji.

Dang ni mwanasiasa kutoka Cameroon. Alishinda urais wa PAP Mei 25, 2015 kwa kupata kura 85 akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Bethel Nnaemeka Amadi.

Dang ni msomi wa masuala ya diplomasia na amewahi kushika nafasi anayoishika sasa Masele akiwakilisha ukanda wa Afrika ya Kati.

Kuhusu kashfa ya Rais wa Bunge la Afrika Dang, wakati Masele akisema ametiwa hatiani, Spika Ndugai amesema Spika huyo ameondolewa tuhuma zote zilizokuwa zikimkabili na hiyo moja ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mwanamke mmoja, inaendelea na uchunguzi hadi Oktoba, mwaka huu itakapofanyiwa uamuzi. “Mhe. Dang mpaka leo tunavyozungumza ndiye Spika wa Bunge la Afrika,” amesisitiza.

Spika Ndugai ameongeza kuwa Masele amethibitisha kwa kila hali maneno mazito aliyoyatoa Askofu Dk. Frederick Shoo katika mazishi ya Dk. Reginald Mengi huko Moshi akisema vijana wanaliangusha taifa, hali iliyomfanya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kukiri udhaifu wa taifa kutowaandaa vijana kuwa viongozi.

Kwa upande wake, Katibu wa Wabunge wa CCM, Rashida Shangazi, ameliambia JAMHURI kuwa CCM hawajakabidhiwa rasmi mashtaka dhidi ya Masele, hivyo wanasubiri akirejea nchini wakitakiwa kumhoji, basi watafuata taratibu na miongozo inayohusiana na utendaji au nidhamu ya wabunge wanaotokana na CCM.

Bunge la Umoja wa Afrika ni mkutano wa wawakilishi wa nchi wanachama wa umoja huo. Ni Bunge lenye wabunge 265 wasiopigiwa kura na raia wa nchi wanachama, bali hutokana na wabunge wa nchi wanachama.

Kwa sasa kazi ya bunge hilo ni kutoa ushauri tu likiwa halina mamlaka ya kutunga sheria. Makao makuu yake yapo mjini Midrand, Afrika Kusini.

Mkutano wa kwanza wa PAP ulifanyika Machi, 2004 chini ya Mwenyekiti wake, Gertrude Mongella wa Tanzania.

Kwa kawaida, Rais wa PAP huwa na makamu wanne kutoka kanda nne za Afrika, Masele akiwa mmoja wao.

Masele hakupatikana kuzungumzia hatua yake ya kusalimu amri kuja kuhojiwa. Taarifa zilizopatikana wakati tukienda mitambo zilisema mbunge huyo ameshawasili nchini, lakini amekuwa hatumii simu zake zilizozoeleka.

2598 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!