Mateso ni mwalimu katika maisha

“Bila mateso na kifo maisha ya binadamu hayawezi kukamilika.”-Viktor Frankl
“Tunapewa baadhi ya mateso kwa ajili ya kutuadabisha na kutusahihisha kwa sababu ya
namna yetu mbaya ya kuishi. Mateso mengine tunapewa si kwa ajili ya kutusahihisha makosa
yetu ya zamani lakini ili kuzuia ya kesho. Mateso mengine hayana lengo lingine isipokuwa
kumfanya mtu ampende Mungu zaidi kwa moyo.”
-Tim Keller.
Daima Ijumaa Kuu inaitangulia Jumapili ya Pasaka. Mafanikio ya kiroho, kimwili, kiutawala,
kisiasa ni safari ndefu. Ni safari inayohitaji uvumilivu, safari inayohitaji uaminifu, safari inayohitaji
imani thabiti.
Ni hakika alivyopata kunena Booker T. Washington kwamba; Nimejifunza kuwa mafanikio
hayapimwi sana na nafasi aliyoifikia mtu katika maisha bali vikwazo alivyoweza kushinda
akijaribu kufaulu. Na mwandishi Ray Charles anasema hivi; hakuna jambo ambalo limeandikwa
katika Biblia, iwe Agano la Kale au Agano jipya, linalosema ukiamini hutakuwa na matatizo.
Juhudi zako ndizo zitakazokufikisha pale ulipopakusudia kufika. Katika maisha kuna mambo
mengi, mengine ni magumu, na mengine huumiza sana moyo. Jifunze kuuambia moyo wako
kuwa nijapopita katika kipindi kigumu cha maisha sitayumba, sitarudi nyuma, sitakata tamaa,
wala sitapoteza matumaini yangu; nitasonga mbele kwa jitihada, kwa ujasiri, kwa matumaini,
kwa malengo, na kwa imani.
Pale unaposema hapa nimefika mwisho, Mungu anasema huu ni mwanzo mpya. Usikate tamaa
kwa sababu ya mazingira, watu wabaya au kipato. Amini unaweza na utaweza daima.
Tutakapojifunza tu kuona lisiloonekana, tutajifunza kutenda lisilowezekana. Badili namna yako
ya kuyatafsiri maisha, yape maisha yako ukweli. Usiyadanganye malengo yako.
Yasiyowezekana ni mambo rahisi sana kwa Mungu kuyatatua.
Mshirikishe Mungu katika mipango yako ya maisha, mshirikishe Mungu katika mapito yako ya
maisha. Mwandishi wa Kimarekani, Anthony Tony Robbin, alipata kuandika; Kila tatizo ni
zawadi, bila matatizo tusingekua.
Kumbe matatizo ni fursa! Ili uishi ni lazima uteseke, na ili uteseke ni lazima uwe unaishi.
Tunapoishi mara moja hapa duniani ni lazima tutateseka tu, hilo halikwepeki. Mateso katika
maisha ni kama usingizi, huwezi ukaukwepa usingizi. Ni lazima utalala tu. Iko hivi; kuna mambo
ambayo huwezi ukayafahamu katika hali ya furaha. Unayafahamu wakati wa mateso na
dhoruba.
Nakubaliana pia na John W. Gardner aliyesema, kutokuwapo kwa matatizo kabisa kungekuwa
chanzo cha kutoweka kwa jamii au mtu binafsi, hatukuumbwa kuishi kwenye dunia ya namna
hiyo. Kimaumbile sisi ni watatuzi wa matatizo na watafutaji wa matatizo.
Watu hawampigi teke mbwa aliyekufa bali aliye hai, watu hawautupii mawe mwembe usio na
matunda bali ulio na matunda. Watu wengi wameshindwa kuyafikia mafanikio waliyonuia katika
maisha yao kwa sababu tu wameruhusu maneno ya watu yawakatishe tamaa.
Mateso katika maisha ni mwalimu asiyeonekana lakini bora zaidi kuliko wale wanaoonekana.
Wakati unapokuwa unakabiliwa na mateso usiulize kwa nini mimi badala yake uliza Mungu
unataka nijifunze nini? Mateso katika maisha ni baraka usiyoweza kuipokea ukiwa unacheka.

Ukweli wa maisha ni kwamba binadamu hapendi kuteseka. Lakini mateso ni bahati
inayojitokeza kwanza katika sura ya balaa.
Kwa hakika mateso katika maisha ni changamoto. Tena ni changamoto inayoyumbisha akili,
roho na upendo. Wakati wa mateso tunabaki na labda nyingi. Tunabaki na hoja nyingi akilini.
Tunajiuliza, kwa nini mimi? Nimemkosea nini Mungu?
Kuna haja gani ya kuishi kwa kumtumainia Mungu? Fahamu jambo hili; katika maisha unahitaji
watu watakaokuzomea ili umkimbilie Mungu. Unahitaji watu watakaojaribu kukutakia hofu ili uwe
na ujasiri, unahitaji watu watakaosema hapana ili ujifunze mbinu mpya ya mafanikio. Unahitaji
watu watakaokukatisha tamaa ili uweke matumaini yako kwa Mungu. Unahitaji watu
watakaokufanya upoteze kazi yako ili uanzishe biashara yako. Hayo yanaitwa mapito ya
kueleka njia ya mafanikio.
Padre Dkt. Faustine Kamugisha anasema; “Tukubali tunapoteseka hatuwezi kufahamu na
kung’amua barabara mipango ya Mungu juu yetu. Kibinadamu wakati wa mateso ni wakati wa
ukiwa, sononeko, huzuni, giza, lawama, lakini wakati wa mateso kwa binadamu ndiyo wakati wa
kujiandaa kupokea yale aliyoyatumainia na kuomba kwa muda mrefu. Tusinung’unike wakati wa
mateso, tusiogope. Tusonge mbele, wakati wa mateso tunaalikwa kuzungumza na Mungu kuwa
naye karibu. Kumuuliza kulikoni baba?
Mara nyingi watu wanaoishi maisha ya uadilifu wanateseka sana na kusakamwa na jamii ya
watu. Hii ni ishara njema kwao hata kama wanateseka na kusakamwa na jamii ya watu. Mateso
siyo mwisho wa safari yako ya kiroho, kiuchumi na kisiasa. Wakati wa mateso tusiwe kama
kuku.
Kwenye kura ya maoni kuhusu ama sherehe za Krismasi zifanyike au zisifanyike kuku
wanaweza kupiga kura ya zisifanyike. Tusipige kura ya kuyatakaa mateso katika maisha yetu.
Mungu anatumia mateso kutufundisha masomo muhimu.
Mahatma Gandhi anatufundisha kwamba nidhamu inafunzwa katika shule ya mateso. Katika
hali ambayo inathibitisha kwamba mateso ni mtaji katika maisha. Jawaharlal Nehru ameandika
kwamba mtu asiye na furaha ni yule ambaye hajawahi kupata taabu, taabu kubwa sana katika
maisha ni kutokuwa na taabu kamwe. Mateso huwafanya watu wamkumbuke Mungu. Maisha ni
shule ambamo kila majonzi, kila maumivu, kila jambo la kuvunja moyo huleta fundisho kubwa.
Mungu anatupenda zaidi ya sisi tunavyompenda. Ukiwa kwenye majaribu mazito yaambie
majaribu yako kwamba Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda, ukiwa kwenye furaha
iambie furaha yako kuwa Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda.
Ukiwa mgonjwa uambie ugonjwa wako kuwa Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda,
ukiwa maskini uambie umaskini wako Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda, ukiwa mzee
uambie uzee wako Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda.
Ukiwa kijana uambie ujana wako Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda, ukiwa na maadui
zako waambie Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda. Ukiwa na marafiki zako waambie
Mungu ananipenda zaidi ya ninavyompenda. Ukiwa maarufu uambie umaarufu wako Mungu
ananipenda zaidi ya ninavyompenda. Sambaza ukuu wa Mungu kwa kutamka maneno hayo.
Wahenga wetu walitufundisha ya kuwa mvumilivu hula mbivu. Ukitaka kuchuma ua la waridi
sharti uwe tayari kuchomwa na miiba yake. Uzuri na utukufu wa Mungu, furaha ya kumwona
Mungu inapatkana katika mazingira magumu na ya kuumiza sana. Mateso huyapa maisha
ladha, mateso huyapa maisha utamu, mateso hupamba Maisha, maisha hayana maana bila
mateso, bila msalaba.
Katika kitabu cha kumbukumbu cha Mt Perpetua, imeelezwa kuwa siku tatu kabla ya siku
iliyopangwa ya mauaji yake Felicitas alijifungua mtoto. Aliteseka sana. Maaskari waliokuwa

wakimlinda waliona namna anavyoteseka, bado zile damu za uzazi zilikuwa zikimtoka.
Mtoto mchanga alikuwa akimlilia, alikuwa hana mtu wa kumsaidia wala wa kumfulia madaso ya
mtoto, askari mmoja miongoni mwa wale waliokuwa wakimlinda alimuuliza; kama unaomboleza
na kulia hivi itakuwaje tutakapokutupia wanyama wa mwitu? Askari huyu alijibiwa; Nateseka
peke yangu ninavyoteseka sasa baadaye mwingine (Yesu) atakuwa pamoja nami, ambaye
atateseka kwa ajili yangu, kwa sababu nitateseka kwa ajili yake.
Kuvumilia ni kupata. Katika raha vumilia, katika shida vumilia, katika majaribu vumilia, katika
magonjwa vumilia na katika ujane vumilia. Mungu anapomruhusu mtu ateseke, anampatia
upendeleo mkubwa kuliko angempa uwezo wa kufufua wafu.