Maulid ni jukwaa la kumtangaza Mtume Muhammad (S.A.W)

Kwa mujibu wa kalenda ya sikukuu za kitaifa nchini Tanzania, juzi siku ya Jumapili tarehe 10, Novemba 2019 ilikuwa siku ya mapumziko kwa mnasaba wa kuadhimisha mazazi ya Kiongozi wa umma wa Waislamu duniani, Mtume Muhammad Bin Abdillahi Bin Abdil-Mutwalib Al-Haashimy Al-Qurayshiy. Siku hii hujulikana kwa jina la ‘Siku ya Maulid’. 

Nchini Tanzania sherehe za Maulid kitaifa ziliandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) chini ya Kiongozi Mkuu wa Waislamu nchini Tanzania, Mufti Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally Mbwana, ambapo mkusanyiko wa Maulid ulifanyika katika viwanja vya Furahisha usiku wa Jumamosi tarehe 9, Novemba 2019  na kufuatiwa na Baraza la Muulid lililofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Mwanza. 

Maulid ni neno lenye asili ya lugha ya Kiarabu likiwa na maana ya mahali pa kuzaliwa; wakati wa kuzaliwa. Kwa muktadha tunaoungazia maana ya pili ndiyo haswa tunayoikusudia; wakati wa kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Allaah amrehemu na ampe amani). 

Kwa pande zetu na kwa mujibu wa matumizi, neno ‘Maulid’ linakusudiwa kumaanisha ‘mkusanyiko wa watu wenye lengo la kuelezea maisha ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kwa lengo la kutekeleza jukumu la kumfuata akiwa ruwaza (kiigizo) njema’ kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Surah ya 33 (Surat Ahzaab) Aya ya 21 kuwa: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.”

Mbali ya kuyaeleza maisha ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), mkusanyiko wa watu kwa jina la ‘Maulid’ hukusanya pia usomaji wa aya za Qur’aan na tafsiri zake, mawaidha na kwaswida. 

Maulid ni tukio mashuhuri duniani linalofanywa katika nchi mbalimbali na kwa karne kadhaa tukio hili limechangia kwa kiasi kikubwa kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na pia kuutangaza Uislamu kiasi cha kufanya shughuli za Maulid ambazo hutoa nafasi ya kumtakia rehema na amani Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kufanywa na baadhi ya Waislamu kila wiki hususan siku ya Alhamisi misikitini na madrasani, kila mwezi kwa ratiba za wafanyaji mbalimbali kwa sehemu kubwa ya miezi 12 ya mwaka na kwa namna ya kipekee katika mwezi wa Rabiiul Awwal (Mfungo Sita).

Kumtakia rehema na amani Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ni kumuomba Mwenyeezi Mungu aendelee kumrehemu na kumpa amani Mtume Muhammad na ni sehemu ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ya kututaka tumuombe yeye aendelee kumpa rehema na amani Mtume wake kama ilivyokuja katika Qur’aan Surah ya 33 (Surat Al-Ahzaab) Aya ya 56 kuwa: “Hakika Mwenyezi Mungu anampa rehema Mtume na Malaika wake (wanamuomba Mwenyezi Mungu afanye hivyo). Enyi mlioamini, ombeni (Mwenyezi Mungu Ampe) rehema na ombeni (Mwenyezi Mungu Ampe) Amani.” 

Tunaona kupitia ayah hii kuwa kumuomba Mwenyezi Mungu Amrehemu (Ampe Rehema) Mtume Muhammad na Ampe Amani, yaani kwa kifupi, kitendo cha kumswalia Mtume Muhammad ni agizo la Mwenyezi Mungu kwa waumini. Agizo hili halikuwekewa mnasaba na wakati maalumu bali umuhimu wa utekelezaji wake unaonekana pale kitendo cha kumswalia Mtume kilipokuwa ni nguzo miongoni kwa nguzo za Swala. Yaani, Swala, kwa mujibu wa madhehebu ya Imam Shaafy, haitimii pale nguzo hii ya kumswalia Mtume itakapoachwa kwa makusudi au kwa kusahau.

Kama haitoshi, Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ametufundisha kuwa kumswalia Mtume kunatakiwa kutangulizwa kwa yule anayetaka kumuomba Mwenyezi Mungu haja zake. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alimsikia mtu aliyekuwa akiomuomba Mwenyezi Mungu pasi na kutanguliza kumtukuza Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume, akamfundisha kwa kumwambia: “Atakapoomba mmoja wenu basi aanze kumtukuza na kumsifu Mola wake Mtukufu, kisha amswalie Mtume, kisha baada ya kufanya hivyo na aombe anachokitaka.”

Mfano mzuri wa kutanguliza kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume Muhammad kabla ya maombi ni Swala ya Jeneza ambayo ni dua ya kumuombea marehemu na katika takbira nne kunapatikana kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu kwa kusoma Surat Al-Faatiha (Sura ya Kwanza katika Qur’aan Tukufu yenye Aya 7), kisha kumswalia Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), kisha kumuombea marehemu na hatimaye kujiombea na kuwaombea wengine.

Kuyasema yote haya ni kuonyesha wajibu wa kumswalia Mtume Muhammad unaotekelezwa wakati wa mikusanyiko inayojulikana kwa jina la Maulid.

Maulid ni tukio muhimu na miongoni mwa mambo ya kheri yanayopaswa kufanywa. Na hata madai kuwa mikusanyiko ya Maulid haifai kwa kuwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) hakuifanya yamekosa nguvu ya hoja kwa kuzingatia matukio ya aina mbili:

Wapingao mikusanyiko ya Maulid (kumtangaza Mtume Muhammad, kumswalia na kuelezea maisha yake) kwa madai kuwa mikusanyiko hiyo na kwa mtindo wa Maulid haikufanywa wakati wa Mtume Muhammad, wamekuwa mstari wa mbele kuandaa na kugharamia mikusanyiko ya mashindano ya Qur’aan Tukufu na kutoa zawadi kwa washindi, jambo ambalo pia halikufanywa wakati wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). 

Ni dhahiri kuwa kufanya kwao mashindano ya Qur’aan Tukufu ambayo hayakufanywa wakati wa Mtume Muhammad ni ushahidi tosha wa kukubali kuwa mlango wa kufanya jambo lolote la kheri katika Uislamu upo wazi muda wa kuwa haliendi kinyume na Qur’aan Tukufu na Mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na ndiyo maana leo tunafaidika kutokana na maendeleo ya teknolojia kuisoma Qur’aan Tukufu kupitia simu zetu za viganjani ingawa jambo hilo halikufanywa wakati wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani).

(2) Taasisi kubwa ya Kiislamu nchini Saudi Arabia iitwayo Rabita (Muslim World League) ilifanya utafiti juu ya sababu zilizosababisha baadhi ya watu hasa katika nchi za Ulaya kumdhihaki Mtume Muhammad na kufikia kumchora kikatuni, wakabaini miongoni mwa sababu hizo ni watu kutomjua Mtume Muhammad na maisha yake na matukufu na mambo mazuri yanayomhusu kiasi cha kuvutwa na yale anayopakaziwa na kumchukia pamoja na kuuchukia Uislamu (Islamophibia).

Baada ya kubaini haya taasisi hii inayoongozwa na Mufti wa Saudi Arabia iliamua kuunda Kamisheni Maalumu ya kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na kumtetea kama njia ya kukabiliana na changamoto ya kutojulikana maisha na matukufu yake.

Dhima kuu ya kamisheni hii iitwayo ‘GLOBAL COMMISSION FOR INTRODUCING THE MESSENGER’ ni kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kwa kufanya tafiti, kuandika vitabu kwa lugha mbalimbali kuelezea maisha yake na matukufu yake, kuandaa mikutano, midahalo, makongamano, semina, maonyesho na ziara mbalimbali kwa lengo la kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kwamba yeye Mtume Muhammad ni Mtume wa Rehema (Prophet of Mercy) na kujibu kila aina ya ‘kupakaziwa’ mambo mabaya. 

Kwa kujiridhisha na kujionea wewe mwenyewe, msomaji wa makala hii, harakati za kamisheni hii tafadhali tembelea wavuti zilizoanzishwa na kamisheni hii na kuwekwa katika lugha mbalimbali zikiwemo lugha mashuhuri za kimataifa. Anuani za wavuti hizi ni: (www.mercyprophet.org), (www.mercyprophet.com) na (www.mercyprophet.net). 

Bila shaka utakubaliana nami kuwa mtindo huu wa kuunda kamisheni ya kuandaa mikutano, midahalo, makongamano, semina, maonyesho na ziara mbalimbali kwa lengo la kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) haukupata kufanywa wakati wa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) lakini ni jambo la kheri linalostahiki kuungwa mkono, na kwa hakika halitofautiani sana na ile mikusanyiko – mapokeo yanye jina la ‘Maulid’ ambayo tangia na hapo lengo lake ni kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), kuyaeleza Maisha yake (Siira), kutoa fursa ya kulitekeleza agizo la Mwenyezi Mungu la kuwataka walioamini wamswalie Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani), kupata fursa ya kujuana watu kutoka maeneo mbalimbali, na kuamrishana mema na kukatazana mabaya kupitia mawaidha na nasaha mbalimbali zitolewazo katika mikusanyiko hiyo.

Angalizo pekee ni kuwa mikusanyiko hii ya kheri kwa jina la ‘Maulid’ haina budi kuchunga mipaka iliyowekwa na Uislamu na kuifanya kwa namna inayochunga heshima ya Mtume Muhammad ambaye yanahusishwa mazazi yake. Jambo lolote lisiloendana na hadhi ya mikusanyiko hii kama vile uchezaji wa kaswida unaofanana na ngoma mbaya ya ‘kigodoro’ hayana budi kukemewa kwa nguvu zote na kukomeshwa.

Haya tuungane na tuhamasishane kuhudhuria Maulid kwa lengo la kumtangaza Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kama tunavyoungana na kuhamasishana kuhudhuria mashindano ya Qur’aan Tukufu aliyoteremshiwa, na twende mbele zaidi kwa kuandaa mikutano, midahalo, makongamano, semina, maonyesho, pia utoaji wa huduma za kijamii kama vile huduma za afya na uchangiaji wa damu salama na mambo mengine ya kheri, ikiwemo kuwapa faraja wagonjwa, yatima, walemavu, wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Tumswalie Mtume Muhammad!       

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.