Mbunge wa Uganda Robert Kyagulanyi Kurejea Uganda Leo

Mbunge wa Kyandodo Mashariki mwa Uganda, Robert Kyagulanyi ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini humo ajulikanaye kama Bobi Wine anatarajia kurudi nchini Uganda leo akitokea nchini Marekani ambapo alienda kupata matibabu baada ya kupigwa na vyombo vya dola.

“Nitarejea nyumbani siku ya jumatatu,licha ya kuwa bado nna hofu lakini Uganda ndio nyumbani ambapo familia yangu na watu wangu wapo.Nina wasiwasi lakini waganda milioni 44 nao wana hofu hivyo lazima nirudi,” Wine alibainisha hayo wakati akihojiwa na gazeti la Mail na Guardian

“Unaweza kukutana na kitu chochote Uganda,na hata ukiangalia historia ya wapiganaji wengi wa ukombozi wamekuwa wakikamatwa wakati wa ujio wao na mimi sina tofauti na wao hivyo nnatarajia chochote kunikuta wakati nitakaporejea”Bobi Wine alisisitiza.

Wine ambaye aliondoka nchini Uganda mwanzoni mwa mwezi septemba kwa ajili ya matibabu ameeleza pia kuwa hali yake kwa sasa inatengemaa .

Bobi Wine alikamatwa tarehe 13 Agosti baada ya mkutano wa kampeni kaskazini magharibi kwenye mji wa Arua ambapo kuna madai kuwa msafara wa rais ulitupiwa mawe.

Mwanamuziki huyo mwenye miaka 36 awali alishtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa makosa ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria, mashtaka ambayo yalifutwa baadaye. Kisha akafunguliwa mashtaka ya uhaini kwenye mahakama ya kiraia.

“Kwa sababu mimi asili yangu ni Uganda na wala sijatokea katika familia ya hali ya juu kifedha na asili yangu ni mtoto wa mtaani .

Hivyo historia yangu ipo wazi ili kila mmoja aione ,ninapoongea wajione wao pia kwamba nnawakilisha sauti zao kupitie kwangu kwa sababu nnajua maumivu wanayopitia”Wine alitoa ujumbe kwa waganda.

Vilevile Wine alieleza kwamba kipindi atakaporudi Uganda hatasababisha vurugu kutoka kwake au wafuasi wake lakini ataendelea kufanya kile ambacho amekuwa akikifanya kwa muda wote kwa kuwapa moyo waganda na kila mmoja kufanya jukumu lake na kila mmoja kusimama kudai haki yake.

Bobi Wine ni nani?

Nyota huyo wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000, hna anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.

Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka jana wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.

Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).

Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.

“Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki…Ninataka siasa zitulete pamoja… jinsi muziki ufanyavyo.”