Meneja wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dk. Milali Machumu, analalamikiwa kwa kuendeleza ubabe kwa wafanyakazi wa chini yake, huku akiendelea kuwahamisha vituo vya kazi kwa madai kwamba wanatumikia adhabu.

Baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo wamelieleza JAMHURI kwamba tangu yalipoibuliwa, na gazeti hili lianze kuandika ‘madudu’ yanayofanywa na kiongozi huyo ikiwamo kushindwa kukusanya mapato kutoka kwa wadau mbalimbali, sasa hasira zimehamia kwa wafanyakazi wote huku akiwatishia kuwafukuza kazi.

‘‘Meneja huyu amekuwa na vitisho vingi kwa wafanyakazi wa chini yake kwamba ni lazima awafukuze kazi mapema hata bila kuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo.

“Mmezungumza na waandishi wa habari na wameandika kuhusu mimi na taasisi hii, sasa hii ni vita mliyoitangaza, niwahakikishie kuwa huu ni wakati wangu wa kushambulia kuliko hata mwanzo,’’ kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Watumishi hao ambao wameomba majina yao yasitajwe gazetini, wanasema Dk. Machumu anawakosesha ari ya kufanya kazi kutokana na vitisho na lugha chafu ambayo amekuwa akiwatolea mara kwa mara, kwani anaweza kuingia kila chumba cha ofisi akiwafokea bila sababu za msingi na kuwaeleza lazima awafukuze kazi.

Wanasema hata mlinzi akichelewa kidogo kufungua geti anafokewa na kutishiwa kutimuliwa kazi na kwamba manyanyaso haya ya wafanyakazi yamechangiwa kwa kiasi kikubwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Wanaeleza kwamba uhamisho ambao unafanyika kwa watumishi kutoka makao makuu ya taasisi hiyo, anauleza kuwa ni adhabu kwa wale ambao wamekuwa wakihoji kuhusu taratibu za utendaji wa kazi ambazo zimekuwa hazifuatwi na meneja huku akituhumiwa kuigeuza taasisi ya Serikali kama kampuni binafsi.

‘‘Hapa tulipo tunaishi kwa hofu sana kama si Watanzania, tumechoka kunyanyaswa na kiongozi huyu ambaye hana utu zaidi ya kuendekeza ubabe usiokuwa na tija kwa taasisi hii kwani hataki hata kushaurika,’’ kinaeleza chanzo chetu.

Wanaohamishwa katika vituo vya taasisi hiyo wanasema ofisi zina mazingira duni kwani vyumba ni vidogo, hakuna umeme wala kompyuta na hivyo kuwaweka katika mazingira magumu katika utekelezaji wa majukumu yao.

‘‘Kama anavyosema, vituo hivi vya kazi ni maeneo ya kutumikia adhabu na kutokana na mazingira yenyewe, tunaamini kuhusu hilo,’’ kinaeleza chanzo chetu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk. Yohana Budeba, alipoulizwa na JAMHURI kuhusu taratibu za kuwahamisha watumishi hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi wakati mwingine. 

Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa MPRU wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo na kumtafuta Mtendaji Mkuu ambaye ana taaluma ya Sayansi ya Bahari atakayechangia sekta ya utalii katika maeneo ya hifadhi za bahari kukua na kuongeza mapato ya Serikali.

Wanasema kama kutakuwa na ugumu kufanyika hilo, taasisi hiyo iwe chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) badala ya kuwaacha wawekezaji kutoka nje ya nchi wakiendesha biashara zao katika fukwe za bahari bila kulipa mapato yoyote.   

Pamoja na sheria ya ulipaji wa tozo ya dola za Marekani 1,500 iliyopitishwa na Serikali mwaka 2009, na kutakiwa kuanza kutumika rasmi Julai mosi mwaka huo kwa wamiliki wa hoteli ambazo ziko katika maeneo ya hifadhi za bahari katika kituo cha Mafia. 

Meneja huyo alitakiwa kufanya vikao na wamiliki wa hoteli hizo lakini hadi leo hii hajatekeleza maagizo hayo na kushindwa kukusanya tozo hizo na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya dola za Marekani 80,000 kwa kituo cha Mafia pekee.

Kutokana na muundo mpya wa utumishi ulioidhinishwa na Msajili wa Hazina mwaka 2006, Bodi ya Wadhamini ya taasisi hiyo iliwapandisha vyeo baadhi ya maofisa wake akiwamo Dk Machumu, lakini amewashusha vyeo na mishahara bila sababu za msingi.

Miongoni mwa madai yaliyotolewa na Dk Machumu ni kuwa watumishi hao walijipandisha vyeo wenyewe, huku akifahamu hakuna mtumishi anayejipandisha cheo mwenyewe. Bodi ya Wadhamini ndiyo iliyohusika katika mchakato huo baada ya kuona utendaji wao hivyo vyeo vyao ni halali.

Kutokana na maboresho ya miundo ya utumishi, Msajili wa Hazina aliidhinisha miundo ya utumishi ya Bodi ya Wadhamini ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kwa barua ya Mei 16, 2006 yenye kumbukumbu namba TYC/T/200/598/02/7 iliyobadili miundo ya utumishi ya taasisi ya mwaka 1999.

Maboresho hayo yalipanua wigo wa mishahara kwa kada zote za taasisi akiwamo Mtendaji Mkuu aliyepanda kutoka PGSS 19 hadi PGSS 21.

Wanasema mfumo huo (scheme of service) hauwezi kuhalalisha vyeo vya baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo akiwamo, na kubatilisha vyeo vya wajumbe wote wa menejimenti kwa madai kwamba walijipandisha vyeo.

Pamoja na kuwahamisha baadhi ya watumishi katika vituo vingine vya kazi, hajawalipa fedha zao za uhamisho hadi sasa na kati ya Sh milioni 10 walizostahili kulipwa wameambulia malipo ya Sh milioni 1 tu.

Wanasema hiyo ni njia ya kuwanyanyasa, kwani huko wanakohamishiwa wamekuwa na maisha magumu mno na wanazungushwa kulipwa fedha zao zinazokuwa zimebaki baada ya kutanguliziwa malipo ya Sh milioni 1 na wale waliolipwa zaidi ni Sh milioni 2.

Kinacholalamikiwa kingine ni kufanya uhamisho bila kuihusisha Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo. Licha ya watumishi watatu waliokuwa wajumbe wa menejimenti kushushwa vyeo na kuhamishwa kutoka makao makuu ya taasisi hiyo kwenda katika vituo vingine vya kazi, mwezi uliopita meneja huyo amefanya tena uhamisho kwa watumishi wengine.

Waliohamishwa ni Haji Mahingika kutoka kituo cha Mafia kwenda Tanga, Anitha Julius kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam na Musa Ali kutoka Mafia kwenda Mtwara.

Dk Machumu alipohojiwa na JAMHURI kuhusu malalamiko ya watumishi wake kutolipwa fedha zao za uhamisho na kuhamishwa bila utaratibu, anasema, “endeleeni kuandika tu.”

By Jamhuri