Joyce NdalichakoTanzania ni moja ya nchi ambazo asilimia kubwa ya vijana wanaohitamu masomo kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na kati, ni wengi ukilinganisha na nafasi za kupata ajira katika fani walizozisomea.

Na wengi kutunukiwa vyeti vya stashahada na wengine shahada za juu, lakini pamoja na yote hayo mianya ya wao kupata ajira imekuwa ni migumu ikilinganishwa na miaka zaidi ya 10 iliyopita.

Pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wadau wa elimu kwa kushiriana na Serikali pamoja na mashirika binafsi, lakini ndivyo tatizo linavyozidi kuwa kubwa.

Najiuliza maswali mengi yanayoniletea homa ya kichwa kila siku hasa pale ninapofikiria juu ya vijana wenzangu waliohitimu na waliotunukiwa vyeti, stashahada, na wale wa shahada mwaka huu na wengine kunifanya nidondoshe machozi.

Wengi wakiwa wanafurahi kuvaa majoho na kofia siku ya mahafali yao na kusahau kesho yao itakuwaje baada ya kuvua majoho na kuachana na mitihani ya darasani, huku mtaa na msoto wa ajira ukiwaita na kuwangojea kwa hamu kubwa, baada tu ya kuachana na maisha ya vyuoni.

Na pengine huwa natoa machozi kwa kuona tangazo la kazi likihitaji mtu mmoja, lakini maombi zaidi ya 2,000 yakitumwa ili mmoja achaguliwe. Na cha kusikitisha huenda hata hao 2,000 na zaidi asipatikane hata mmoja mwenye sifa. Hapo ndipo ninapokuwa na maswali yafanyayo kichwa changu kiendelee kuniuma.

Sijasahau zile nafasi chache za kazi zilizotangazwa na Idara ya Uhamiaji zilizofanya watu wakafanye mtihani wa kazi Uwanja wa Taifa,Temeke,Dar es Salaam na kuudhihirishia ulimwengu kuwa vijana wengi wa Kitanzania hawana ajira. 

Pia nahisi ni tukio ambalo liliandikwa kwenye vitabu vya kumbukumbu maarufu kama ‘Encyclopedia’ kwani ilikuwa inauma na kusikitisha sana kuona vijana wengi zaidi ya 10,000 wanagombania nafasi zisizozidi 100 za ajira.

Inaniuma sana hasa kwa hawa waliohitimu mwaka huu na wanaokwenda kuongeza idadi tena ya wale waliosota mtaani kwa miaka zaidi ya kumi, huku bahasha za kaki zilizochakaa na CV zao kuchafuka na wengine viatu vikiwa vimewaisha soli kwa sababu tu ya kutafuta kazi katika ofisi mbalimbali za Serikali na zile za binafsi.

Kinachonishangaza pia ni kuona wengine wanapata kazi tena kwenye makampuni makubwa ya kitaifa na kimataifa huku wakiwa bado shule. Hapa napo najiuliza maswali mengine tena mengi tu kuhusu wao, kuwa wanatumia vigezo gani kupata kazi hizo au kwa nini wao wanaosoma wapate kazi mapema huku wengine wakihangaika kutafuta kazi kwa zaidi ya miaka mitano, na wengine kukata tamaa na kuweka vyeti chini na kutafuta njia ya pili yaani ‘Plan B’ au kujiingiza kwenye vitendo viovu na uporaji wa kutumia silaha, na wengine kuamua kujiingiza kwenye

uuzaji wa dawa za kulevya na ujangili wa wanyamapori wetu pasipo hata kujali athari zake.

Nimepata kuwauliza baadhi ya wakurugenzi ambao hutangaza nafasi za kazi na vijana wengi wa Kitanzania kujitokeza na kazi wakakosa kwa kutotimiza vigezo. Huwa wananipa majibu ambayo kwa namna moja ama nyingine nakubaliana nayo lakini mengine inanibidi nikubaliane nao kwa shingo upande.

Mmoja wa waajiri wa kampuni kubwa tu ya hapa nchini aliniambia kuwa maombi mengi ya kazi hutumwa ofisini kwake tena na watu waliopata ufaulu mzuri katika vyuo vya walivyosoma, lakini wanapoajiriwa kiwango cha ufanyaji kazi wao na ufaulu alioupata na kutunukiwa na chuo chake ni vitu viwili tofauti.

Utendaji kazi ni hafifu mno ukilinganisha na kiwango chake cha elimu na ufaulu ambao yeye aliniambia walimu wake ni kama walimzawadia au kuukandilia. 

Aliniambia vijana wengi wa Kitanzania hususani wanaohitimu vyuo vikuu kwa sasa ni aibu hata kusema kazi wazifanyazo ofisini ukilinganisha na kiwango cha elimu na ufaulu wao.

Akanipa mfano kuwa Novemba mwaka huu aliitwa kwenda kusimamia usaili wa kutafuta watu watatu  kutoka Afrika Mashariki ili wakafanye kazi katika Benki ya Dunia.

Lakini pamoja na kupata maombi zaidi ya 700 kutoka Tanzania na yeye mwenyewe kukaa chini na kupitia ombi moja baada ya jingine, lakini cha kusikitisha alikosa kijana wa Kitanzania mwenye vigezo vya kufanya kazi katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Nilijiuliza sana, shida iko wapi? Na kwa nini iwe kwa Watanzania tu? Mbona kwa wenzetu Wakenya, Wanyarwanda, Warundi na Waganda wanafanya kazi tena kubwa tu kwenye mashirika binafsi yanayomilikiwa na Watanzania wenyewe?

Hapo ndipo nikapata jibu kubwa kuwa kuna shida kwenye mifumo yetu ya elimu. Mfumo hauwaandai vijana wa Kitanzania kuingia sokoni mara tu wanapohitimu masomo yao hasa ya juu.

Ukilinganisha na miaka ya 1990 kurudi nyuma, mfumo wa elimu ulikuwa mzuri na masomo yalilenga kumuandaa kijana wa Kitanzania kuajirika na kujiajiri mwenyewe na si kutegemea ajira ya serikali au kutoka kwenye sekta binafsi.

Nilipata kumhoji baba yangu kuwa kwa nini kipindi chao walikuwa hawasoti mtaani kama sasa, alinambia kipindi chao walikuwa na mfumo uliokuwa unawafanya wao wajiajiri na si kutegemea ajira, na ndiyo maana walijituma na wengi wao kugombaniwa wakiwa bado masomoni, tofauti na leo wasomi wanavyogombania kazi.

Hapo ndipo nilipokumbuka ile falsafa ya elimu ya kujitegemea iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, baada ya Azimio la Arusha ambako elimu hii ilimjenga Mtanzania aliyekuwa anasoma kwa kipindi hicho, aweze kuwa wa uwanja mkubwa wa kujiajiri na siyo kuajiriwa – hapo ndipo masomo kama ya kilimo, ufugaji, muziki, sanaa na mengine mengi ya ufundi kama stadi za kazi yalipoanzishwa ili tu kumjenga mtoto wa Kitanzania aweze kijiajiri na si kutegemea ajira.

Lakini pia nikakumbuka lile Azimio la Musoma la mwaka 1974, ambalo nalo lililenga kumjenga mtoto wa Kitanzania kuweza kusoma elimu ya msingi ambayo ingemwezesha ajue kusoma, kuandika na kuhesabu. 

Hapo ndipo Serikali ilipoamua kuajiri walimu wengi ambao walijulikana kama walimu wa UPE ili tu waweze kufundisha vijana wa Kitanzania waondokane na maadui ambao Mwalimu aliwataja kuwa ni ujinga, maradhi na umaskini.

Cha kushangaza mpaka sasa maadui hawa hawajaisha kwani pamoja na Watanzania wengi kwa sasa kujidai kuwa sisi si wajinga, lakini bado hatujaweza kutengeneza kitu ambacho tunaweza kujivunia tuendapo popote pale ulimwenguni. 

Hebu jiulize wembe tunaletewa na Wachina, sabuni, chumvi, viberiti na vinginevyo vingi tunaletewa na Wakenya; nguo tunaagiza nje sasa werevu wetu huko wapi? Au tunajivunia nini, tanzanite, dhahabu au almasi ambazo kila mwaka Afrika Kusini na Kenya wanapewa tuzo na zawadi kubwa na mataifa makubwa duniani kwa uuzaji wa maduni hayo nje? 

Dunia yote inatambua kuwa tanzanite inapatikana Tanzania tu. Tusiongelee hayo kwa leo lakini tuangalie sera yetu ya elimu iko wapi? Nawaulizeni nyie wakubwa mlioko huko juu ambao wengi wenu mnatutia aibu kama nchi, mnashindwa kuelewa hata historia ya nchi yetu, na kusema vitu ambavyo ni aibu tupu kwa nchi yetu. Na ndiyo maana hata sishangai kumwona anayejiita msomi wa chuo kikuu ukimuuliza kirefu cha TANU ni nini anajibu madudu ambayo hata hayapo. Tatizo ni mfumo wetu wa elimu na si vinginevyo. Inamjenga kijana wa Kitanzania kutegemea kazi za ofisini. 

Pia kutokana na utandawazi pasipo hata kujiuliza mara mbili juu ya utoaji wa elimu ya juu na ya kati kwa kuruhusu umilikaji wa vyuo vingi ambavyo kiukweli vingi vikiwa havina hata sifa ya kutoa hata elimu ya sekondari na kuongeza aibu kwa Taifa, kwa kuwa na wasomi wengi wasioweza hata kutengeneza kiberiti au kalamu.

Huku wakitangaza matangazo yanayovutia wateja wao na kuhakikishiwa ajira za uhakika mara tu wamalizapo elimu katika vyuo hivyo, na wanafunzi pasipo hata kutazama na kufikri kwa kina tangazo hilo lililojaa ushawishi mkubwa na wao kujirundika na kulipa ada kubwa, na mwisho wa siku kumaliza na kazi kukosa na kuongeza idadi ya wale tegemezi wa ajira.

Nimalize kwa kuwaomba wadau wa elimu, walimu, wizara ya elimu na wakufunzi wa elimu kutengeneza falsafa na ‘motto’ wa elimu ya Kitanzania ili tuendapo popote pale nasi tuseme falsafa ya elimu ya Mtanzania ni hii, na si kubaki kujing’atang’ata pale wageni watuulizapo sera na falsafa ya elimu ya Tanzania ni ipi tupate cha kujibu pasipo hata kufikiri sana.

Kwa leo naweka kalamu yangu chini kuashiria nimemaliza na kuwaachia wahusika mtafakari ili elimu itakayotolewa iweze kumfanya kijana wa Kitanzania kuajirika popote pale kama walivyo wenzetu Wakenya, Warundi, Wanyarwanda na mataifa mengine ya Kiafrika na duniani kwa ujumla.

 

Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea fani ya Mawasiliano kwa Umma katika Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0763 580901, 0716 216249 au baruapepe: [email protected]

By Jamhuri