Mfumo wa kuwapata wabunge EALA haufai

Tumewapata Watanzania kenda ambao kwa miaka mitano ijayo watatuwakilisha kwenye Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Waliochaguliwa ni Fancy Nkuhi (CCM), Happiness Legiko (CCM), Maryamu Ussi Yahya (CCM), Dk. Abdullah Makame (CCM), Dk. Ngwaru Maghembe (CCM), Adam Kimbisa (CCM), Habib Mnyaa (CUF), Josephine Lemoyan (CHADEMA) na Pamela Massay (CHADEMA).
Sina shaka na uwezo wa baadhi ya wabunge wetu hawa kutuwakilisha katika EALA, ingawa hatua hii inatupatia fursa ya kuanza kuhoji staili inayotumiwa kuwapata. Kupatikana kwao kumekuja baada ya kuwapo msuguano mkali ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msuguano wa awali ulihusu kanuni wakati wa upigaji kura. Kama ilivyotarajiwa, CCM na Chadema walioongoza walinyukana walivyo.
Kwa namna mambo yalivyoendeshwa hadi kuwapata wabunge hawa tisa, nashauri huko tuendako yatupasa kuwa na kanuni nzuri zaidi za kuwapata wabunge watakaotuwakilisha EALA. Lakini si huko pekee, bali hata kwenye vyombo vingine vya kimataifa vinavyohitaji uwakilishi wetu kama nchi.
Tumewapata wabunge wa EALA kwa namna iliyotawaliwa zaidi na mihemko, u-vyama na itikadi za wapigakura (wabunge) badala ya kujiegemeza kwenye uzalendo kwa maana ya kuwapata wawakilishi sahihi wenye uwezo wa kujenga na kupangua hoja mbalimbali kwenye Bunge hilo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Ingawa siamini sana, lakini kuna minong’ono kuwa miongoni mwa wabunge wetu waliochaguliwa, wamo ambao kwa kweli wamepata nafasi hiyo kwa sababu tu za ushabiki wa kisiasa badala ya sifa na uwezo wao.
Kama kweli hiyo dosari ipo, ni wajibu wa Watanzania kujipanga vizuri ili kuwapata wawakilishi kwa mtazamo wa ki-nchi zaidi badala ya ushabiki unaotawaliwa na siasa za ndani ya nchi yetu.
Bunge la Afrika Mashariki si chombo cha kupelekwa watu waliotokana na ushindani wa siasa za vyama nchini mwetu. Tuna wajibu wa kuhakikisha tunawapata wabunge imara ambao kwao ‘Tanzania’ ndio kila kitu.
Hatupeleki wabunge EALA kwenda kuwashambulia CCM, Chadema au CUF. Tunapeleka wabunge wa kwenda kuyalinda na kuyasimamia maslahi ya Tanzania yote. Hili si Bunge la watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu tu! Hili ni Bunge linalohitaji Watanzania wenye uwezo wa kusimamia kile watakachotumwa na Watanzania kwenda kukitetea au kukipinga.
Kwa sababu hiyo ni lazima tuwe na wabunge wenye uwezo wa kielimu wa kutosha na weledi wa masuala yanayohusu mtangamano. Hili la kujua kusoma na kuandika ni heri likaishia huku huku kwetu.
Katika nchi wanachama wa EAC, Tanzania ndio kinara wa rasilimali. Hakuna nchi nyingine inayotazamwa kwa jicho la husda zaidi ya Tanzania. Utajiri wa madini upo Tanzania, utajiri wa ardhi upo Tanzania; utajiri wa wanyamapori upo Tanzania, vivutio vya utalii vipo Tanzania, wingi wa watu upo Tanzania, kijiografia Tanzania ndio iko pazuri zaidi; nchi iliyofanikiwa kuupunguza ukabila, udini na ukanda ni Tanzania. Kwa ukubwa Tanzania ndio nchi kubwa zaidi- hata kama Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi zikiwekwa pamoja hazifui dafu kwa Tanzania kwa ukubwa. Nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi ni Tanzania; nchi yenye watu waungwana wenye uwezo wa kuwaambukiza wenzao upendo, umoja, mshikamano na udugu, ni Tanzania.
Nchi yenye sifa zote hizi inapaswa kuwa kinara kwenye Bunge la EALA na EAC kwa jumla. Inapaswa kuwa na wawakilishi makini ambao wakizungumza kwenye vikao, wenzao wa nchi wanachama wawaelewe na waheshimu msimamo wao. Itakuwa aibu kwa Tanzania kuongoza kwa mazuri yote hayo, halafu ikaongoza pia kwa kuwa na wabunge vilaza!
Kwa kuona na kusikia, nchi inayoandamwa zaidi ili iruhusu matumizi ya rasilimali zake kwa manufaa ya EAC ni Tanzania. Mathalani, suala la ardhi ni miongoni mwa mambo makubwa ambayo wanachama wa EAC wangependa kuona Tanzania inalegeza msimamo. Tukiwapata wabunge legelege kuna siku wanaweza kulemewa kwenye vikao na hatimaye kujikuta tukiangukia kwenye kile kilichomo kwenye matamanio ya majirani zetu.
Hayo matamanio si mengine, bali kuifanya ardhi ya Tanzania na rasilimali zake nyingine kuwa ‘mali ya wote’ katika EAC! Hili sharti twende nalo kwa uangalifu, na kwa kweli hatuna budi kusimamia kile kilichoamiwa na Rais Benjamin Mkapa, na Jakaya Kikwete. Ardhi ya Tanzania ni mali ya Watanzania, basi.
Kumekuwapo njama nyingine za kibiashara. Tanzania tumekuwa tukiumizwa, ama hadharani, au chini chini katika masuala mengi ya kibiashara. Kwa miaka kadhaa Wakenya wanataka lango la mpaka wa Bologonja lifunguliwe.
Bidhaa zitokazo Tanzania zinapata vikwazo vingi kuingizwa na kuuzwa katika soko la Kenya. Wakenya wanajua Tanzania ya sasa haihitaji bidhaa kutoka kwao. Wiki kadhaa zilizopita nilizuru Tarime. Nilifurahi mno kuyaona maduka ya Tanzania yakiwa na bidhaa za Tanzania, tofauti kabisa na miaka iliyopita ambako ukiwa Tarime au Mara, ungedhani uko Kenya! Wivu umewajaa majirani hawa, hawapendi bidhaa zetu ziingizwe nchini mwao. Wameshaanza na la gesi. Miaka kadhaa iliyopita walimzuia Mtanzania, Dk. Gideon Mazara kuingiza maziwa Kenya kutoka kiwanda chake kilichopo Musoma.  Hili ni eneo ambalo wabunge wetu kwenye EALA lazima wasimame kidete kuhakikisha linaondolewa.
Ili kuwa na uwakilishi mzuri na wenye tija katika EALA, tunapaswa kuketi na kuona namna nzuri ya kuwapata wawakilishi walio makini kabisa.
Endapo tutaendelea na utaratibu wa sasa wa kuwapata wabunge kwa misingi ya itikadi za vyama vya siasa au chuki, kuna wakati tutawapata wawakilishi wa ajabu sana.
Ikiwezekana tuwe na vigezo na sifa za aina ya watu tunaotaka watuwakilishe. Kwa mfano, tunaweza kuainisha sifa hizo kuwa ni sheria, ujuzi katika uchumi na biashara, masuala ya ushirikiano wa kimataifa na kadhalika.
Baada ya kuweka vigezo, turuhusu wanaombaji wajitokeze nchini kote, kisha wafanyiwe ‘vetting’ na jopo la wataalamu lililoundwa kisheria kwa kazi hiyo. Tupate majina ambayo yatafikishwa bungeni kupigiwa kura bila kujiegemeza kwenye u-vyama. Wabunge wawe na kazi moja ya kuchagua wabunge wa EALA kwa kigezo cha kupata uwakilishi wa nchi, na si kwa mihemko ya kiitikadi. Sheria na kanuni zilizotungwa kuwapata wabunge hawa, zimetungwa na wanadamu, kwa maana hiyo zinaweza kubadilishwa ili kukidhi matakwa ya wananchi na nchi.
Huu utaratibu tunaoendelea nao sasa ni hatari. Hauna manufaa. Tunaweza kuwaacha watu makini wenye uwezo wa kujenga hoja, tukajikuta tukipeleka wachekeshaji EALA. Nasisitiza kuwa hili ni suala la nchi. Halina tofauti na vita. Inapotokea tukahitaji askari wa kwenda kupigana, kinachoangaliwa ni uzalendo wa askari na uwezo wake. Hatuangalii kitu kingine zaidi ya hicho. Hatuangalii ana rangi gani, anatoka mkoa gani, ni wa kabila gani au mwenye mwelekeo fulani kiitikadi. Anapokwenda vitani anakwenda kulitetea taifa, haendi kutetea kabila, dini, rangi, kanda wala itikadi yake.
Kwenye uwakilishi wa nchi katika vyombo mbalimbali vya kimataifa, siasa za ndani sharti zizikwe. Uwakilishi wa nchi tukabiliane nao kama nchi moja ya watu wamoja.
Hili la kuwapata wabunge EALA liende sambamba na mambo mengine yote yanayostahili kutuunganisha. Kwa mfano, sikuona sababu siku ile pale msibani katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, kuwa na watu waliovalia sare za vyama vya siasa! Msiba kama ule haupaswi kuwa na sare wala bendera za vyama. Ulipaswa kupambwa kwa rangi za Taifa letu. Tunapopuuza au kuyaachia mambo kama haya kuanza kutamalaki katika jamii yetu, matokeo yake tunapofuka na kufikia hata kuwachagua wawakilishi wa nchi yetu kwa misingi ya vyama. Hili si jambo zuri.
Sina mamlaka katika hili la wabunge wetu kwenye EALA, lakini kila nikipitia orodha yao, naona kabisa wengine waliomo ni waburudishaji tu ambao kama wabunge wetu wangeweka mbele maslahi mapana ya nchi yetu, wasingewapitisha. Tukivuna aibu, haitakuwa aibu ya CCM, ya Chadema, wala ya CUF. Itakuwa aibu ya Tanzania. Mambo ya nchi tuyape sura ya nchi badala ya u-vyama.