Mamia ya wananchi wanaoishi jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara (NMGM) unaomilikiwa na African Barrick Gold (ABG), wako katika hatari ya kuugua saratani ya mapafu, damu na kuwa viziwi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, wananchi hao wako katika hatari ya kuathiriwa na saratani ya mapafu (pneumoconiosis) na damu (silicosis) kutokana na magonjwa ya kuharibika njia ya hewa yanayosababishwa na kemikali zilizoko kwenye chembechembe za mchanga.

 

Pia wako katika hatari ya kuharibikiwa ngoma za masikio (ear drums) na hivyo kuwa viziwi kutokana na kelele za milipuko ya baruti mgodini hapo.


“Kemikali za sumu zilizoko kwenye mawe na mchanga kwenye machimbo ya madini, pamoja na dawa za Cyanide na Mercury zinazotumika kusafishia dhahabu ni hatari sana kwa afya za watu wanaoishi jirani na machimbo,” amesema daktari mmoja wa magonjwa ya binadamu. Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa zaidi ya familia 100 zinazokadiriwa kuwa na watu zaidi ya 500 zinaishi jirani na NMGM.


Uongozi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa upande wake unatambua kuwa ni familia 60 pekee zinazoishi jirani na mgodi huo.


Wananchi hao wameendelea kuishi jirani na machimbo hayo kutokana na kampuni ya ABG na Serikali kuchelewesha mpango wa kuwalipa fidia za usumbufu na mali zao.


“Kampuni inaendelea na mchakato wa kufanya tathmini ya mali za wananchi chini ya usimamizi wa Serikali,” kimesema chanzo cha habari na kuongeza:


“Siyo tu kwamba watu wanatakiwa kuhama kutoka jirani na mgodi, bali kampuni inahitaji maeneo ya kuendesha shughuli za uchimbaji madini.”


Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi hao wamekataa kupokea fidia wakidai ni ndogo isiyoendena na thamani ya ardhi na mali zao zikiwamo nyumba na mashamba ya mazao mbalimbali.


“Wengine wameshafungua mashauri katika Mahakama ya Ardhi wakiulalamikia Mgodi wa North Mara kwa kuwapunja malipo ya fidia kinyume cha sheria,” amedokeza mmoja wa wananchi hao, Augustino Sasi.


Mbali ya kuwa katika hatari ya kukumbwa na maradhi tuliyoyataja hapo juu, wananchi wanaoishi jirani na NMGM wanakabiliwa na adha ya vumbi, kelele na nyumba zao kupasuka nyufa kutokana na milipuko mikubwa ya baruti mgodini.


Alipoulizwa na JAMHURI, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Ernest Kabohola, amekiri ofisi yake kupata malalamiko ya watu 60 kuhusu madai ya fidia dhidi ya NMGM.


“Hawa wote wanaishi jirani na mgodi, ni watu ambao wanaweza kuwa affected (kuathirika), wako kwenye maeneo hatarishi,” amesema Kabohola na kuendelea:


“Tumeshamjulisha meneja wa mgodi na tunayashughulikia malalamiko haya kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mara na Mdhamini Mkuu wa Serikali.”


Habari zisizo rasmi zinasema wananchi hao wanadai fidia ya Sh zaidi ya bilioni 20 ndipo waweze kuhama kutoka jirani na mgodi huo.


Ofisa uhusiano wa ABG Tanzania, Foya Nector, alipotakiwa na JAMHURI kutoa ufafanuzi kuhusu wananchi hao alikwepa jukumu hilo.


Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa ABG Tanzania, Deo Mwanyika, hazikuzaa matunda baada ya JAMHURI kumpigia simu mara kadhaa wiki iliyopita, ambapo mara zote ilikuwa ikiita bila kupokewa.


5854 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!