Mgogoro wa ardhi mkoani Mtwara umechukua sura mpya baada ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Albert Mbila, kujitoa lawamani kwa kusema suala hilo halikuwa na mkono wake.
 Mbila anatajwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufuatiliaji wa Mgogoro wa Ardhi katika Kijiji cha Sinde, Mtwara Vijijini, Marijani Dadi, kwa kushiriki kuchakachua na kuchukua sehemu ya Sh 378,834,735/- zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya malipo ya fidia ya wananchi wa Kata ya Msanga Mkuu, kikiwamo Kitongoji cha Ng’wale, Kijiji cha Sinde.
 Dadi anamshutumu Mbila kwa kuingilia mchakato wa utwaaji wa eneo la kitongoji hicho kinachohitajika kwa matumizi ya upanuzi wa Bandari ya Mtwara.
 “Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alhaj Mbila, alishiriki katika kushinikiza Bandari ipewe hati haraka haraka ya umiliki wa eneo baada ya kuona wananchi wanahoji kuhusu mustakabali wao wa kupewa eneo mbadala kwa shughuli za kilimo na uvuvi.
 “Katika fedha hiyo iliyotolewa na Bandari, Mbila na maofisa Ardhi waliichakachua na kulazimisha iaminike kuwa wananchi wote waliridhia maeneo yao kuchukuliwa jambo ambalo si kweli,” amesema Dadi.
Mgogoro wa ardhi ya Ng’wale na Bandari umedumu kwa miaka 17 sasa kutokana na wakazi wa kitongoji hicho kusema kuwa walifanyiwa mpango wa kudhulumiwa maeneo yao ya asili bila kushirikishwa, kupewa maeneo mbadala wala kulipwa fidia stahiki.
 JAMHURI limefanikiwa kuona hati ambayo Mamlaka ya Bandari Mtwara ilipewa kwa umiliki wa eneo la Msanga Mkuu na Ng’wale lenye ukubwa wa ekari 2,623.57.
Alhaj Mbila anayeishi Kingugi, Dar es Salaam ameshtushwa na taarifa hizo kama ifuatavyo:-
JAMHURI: Unatajwa na mwakilishi wa wanakitongoji cha Ng’wale kuwa ulihusika kushinikiza Bandari kupewa hati ya umiliki kwa maslahi yako binafsi. Je, taarifa hizi zina ukweli wowote?
Mbila: Hapana, kwanza mimi nimekwishastaafu miaka zaidi ya 10 iliyopita. Kwani mtu akistaafu anaondoka na nyaraka za ofisi? Nenda Ofisi ya Katibu Tawala Mtwara utazipata habari zote unazotaka.
 Mimi sikushinikiza chochote na ufahamu kuwa nilikuwa nikiwakilisha Serikali na Bandari ambayo inalihitaji eneo hilo ni sehemu ya Serikali.
 JAMHURI: Suala la wananchi wa Ng’wale dhidi ya Bandari ulilisimamiaje?
Mbila: Nataka nikusaidie ili ufanye kazi yako vizuri. Nimekwambia nenda ofisi ya RAS Mtwara utapata kila kitu. Ninachofahamu ni kwamba taratibu zote zilifuatwa. Mimi kwa sasa ni mstaafu sipo serikalini siwezi kuzungumzia maamuzi niliyoyafanya nikiwa serikalini. Marais wengi wamepita wanapokezana ofisi hata mimi nilikabidhi ofisi, kapate taarifa Mtwara.
JAMHURI: Je, ulichukua kiasi gani cha fedha kwenye pesa ya fidia iliyotolewa na bandari kwenda kwa wananchi?
 Mbila: Sikuchukua pesa yoyote. Huyo aliyekupa taarifa kuwa nilichukua pesa na kushinikiza ndiye akwambie kiasi nilichochukua. Mwezi mmoja na nusu umepita tangu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipoahidi kuwa suala hilo ataliundia timu ya kulifuatilia.
 Aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-TAMISEMI na baadaye akawa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alijitosa kuutatua mgogoro huo, lakini jitihada zake ziligonga mwamba.
 Katika barua ya Novemba 15, 2002 kwenda kwa Katibu Kamati ya Maendeleo Ng’wale yenye Kumb. Na. HA.78/234/01 yenye kichwa cha habari; “Yah: Kuhamishwa katika kijiji chenu cha asili kwa mizengwe ya upanuzi wa Bandari Mtwara” barua hiyo inasema:
 “Tafadhali rejeeni barua zenu Kumb. Na. KMT/MUN/2002/013 ya tarehe 29/07/2002 na Kumb. Na. KMT/MUN/2002/023 ya tarehe 11/11/2002 kuhusu somo tajwa hapo juu, nakiri kuzipokea.
 “Rejea mazungumzo yaliyofanyika tarehe 2/8/2002 kati yangu na Katibu, Ndugu Abdrahaman Mwalim na Mjumbe Ndugu Marijani Dadi, pia mazungumzo ya tarehe 14/11/2002 kati yangu na Mjumbe ndugu Marijani Dadi. Suala lenu linashughulikiwa punde mwafaka utakapopatikana mtajulishwa kwa sasa vuteni subira”.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sinde, Ahmadi Ching’ang’a, anasema mgogoro huo umechangia kutopigwa hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kitongojini hapo.
“Ng’wale imesimama kimaendeleo kwa kipindi chote cha miaka 17 ya mgogoro. Tuliomba kujengewa shule na wilaya, jibu likatoka kuwa hatuwezi kujengewa shule kwa sababu eneo lina mgogoro. Watoto wetu wanatembea mwendo mrefu wa kwenda Shule ya Msingi Mkubiru. Hata hii shule imekwepeshwa kwenye ramani ambayo inahitaji kitongoji hiki wakisema wanaheshimu mali ya Serikali,” anasema Ching’ang’a.
“Tuliomba pia kuletewa umeme wa REA na Kituo cha Afya, jibu likawa hilohilo kwamba eneo lina mgogoro. Huwezi kuamini kuwa Kata ya Msanga Mkuu ina Kituo cha Afya kimoja tu ambacho kipo Namela licha ya kuwa na wakazi takribani 10,000. Kiufupi hakuna mradi wowote wa maendeleo ulioelekezwa Ng’wale kutokana na mgogoro huu,” anasema Ching’ang’a.
 Amesema Ng’wale imeshafikia hatua ya kuwa Kijiji ila kutokana na mgogoro huu jambo hilo halijafanyika.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ng’wale, Ahmadi Ahmadi (49), anasema kuwa kitongoji hicho kabla ya mwaka 2010 kilikuwa katika Kata ya Ziwani. Anasema Kata ya Ziwani ilijumuisha vitongoji vya Msangamkuu, Namela, Sinde, Ng’wale, Nete, Nalingu, Nnazi, Ziwani, Moma, Mkubiru, Mlamba na Minyembe.
Ahmadi amesema mwaka 2010 kata hiyo iligawanyishwa katika kata mbili ambazo ni Kata ya Ziwani na Kata ya Msanga Mkuu. Kata mpya ya Msanga Mkuu ilijumuisha vijiji vya Msanga Mkuu yenyewe, Sinde, Nalingu, Mkubiru na Namela ambapo vijiji vilivyobaki vilikuwa ni vya Kata ya Ziwani hadi leo.
Amesema kwa mujibu wa taarifa alizopewa alipoingia madarakani mwaka 2009 Kitongoji cha Ng’wale tangu Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 hadi miaka ya 1970 kilikuwa na wakazi wasiozidi 120.
 Hadi kufikia mwaka 2000 idadi ya watu wa Ng’wale ilikuwa ni 774. Anasema kwa sasa Ng’wale ina wakazi wasiopungua 1,600. Shughuli kuu za wakazi wa Ng’wale ni kilimo, uvuvi na ufugaji.

1534 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!