Miaka 92 ya Rais Mugabe na ndoto za kuwa bondia

MugabeRais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amesema kwamba ana nguvu ambazo hata kama akipanda ulingo wa ndondi anaweza kumpiga mpinzani wake.

Rais Mugabe, ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 92, akiwa ni kiongozi pekee barani Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, alikwishatoa tangazo kwamba hana mpango wa kustaafu.

“Nani kasema nimechoka,” anahoji Rais Mugabe akibezwa na wapinzani kwamba hana budi kustaafu sasa na yeye akiwajibu kuwa hana sababu kwani anaweza hata kurusha ngumi.

Rais Mugabe alipoulizwa kuhusu mrithi wake wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 92 tangu azaliwe, alihoji tena: “Mbona mnang’ang’ania kupata mrithi?

“Unataka nikutwange ngumi uanguke chini ndipo uamini kwamba bado nina nguvu?” Alijibu Rais Mugabe alipokuwa akizungumza na mwandishi wa Gazeti la Serikali ya Herald.

Rais Mugabe anasisitiza hatastaafu katikati ya muhula wake wa sasa, ambao ulianza 2013.

“Mbona nilikubali kuendelea kuongoza? Labda ningekuwa na maradhi au ninaugua au siwezi kuongoza, hapo ungezungumzia kuhusu kustaafu kwangu, lakini niko mzima wa kumtwanga mtu ngumi,” anasema Rais Mugabe.

Wakati Rais Mugabe akisema hayo, mmoja wa wabunge kutoka chama cha ZANU-PF, anasema huenda akafikishwa kortini kujibu mashtaka ya kumtukana Grace Mugabe, mke wa rais huyo.

Mbunge huyo, Justice Wadyajena, anadaiwa kutumia ‘lugha ya matusi’ dhidi ya mwanachama mwenzake wa chama tawala cha ZANU-PF aliyekuwa ameweka picha ya Grace kwenye gari lake.

Mkasa huo unafuatiliwa na watu wengi kama sehemu ya mzozo wa ndani ya chama kuhusu mrithi wa Rais Mugabe, ambaye anazidi kung’ang’ania madaraka.

Wadyajena amenukuliwa kwenye nyaraka za mahakama kwamba alimwambia Jimayi Muduvuri: “Wewe ni mjinga sana, sawa na huyu mama yenu.” Atafikishwa kortini Victoria Falls.

Mke wa Rais nchini Zimbabwe huitwa ‘amai’, maana yake mama na wafuasi wa chama cha ZANU-PF. Mbunge huyo amekanusha madai hayo.

Tayari Rais Mugabe ameshtukia mpango wa kutaka kumng’oa madarakani akisema kwamba baadhi ya wapinzani wake ndani ya chama cha ZANU-PF wanafanya mipango hiyo “Lakini hawataweza.”

Rais Mugabe ameahidi kupambana na rushwa ndani ya chama na kukabiliana na maofisa wa chama hicho ambao kazi yao ni kutoa na kupokea rushwa.

Hasira za Rais Mugabe zilionekana wazi kutokana na madai ya njama za kutaka kumwua, yanayodaiwa kuandaliwa na naibu wake, Joyce Mujuru. Hata hivyo, Mujuru alikanusha madai hayo ambayo yamekuwa yakimwandama.

Rais Mugabe alisema kutokuwapo kwa Mujuru kwenye mkutano huo wa chama, kunaonesha kuwa anaogopa na amemshutumu kuwa fisadi anayepanga kumwondoa madarakani kwa kushirikiana na maofisa wengine wa chama.

Mujuru ambaye amekanusha madai hayo, alionekana kuwa katika nafasi nzuri kuongoza chama kutoka kwa Mugabe ambaye walipigania naye uhuru wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa watawala Wazungu.

Chama tawala cha Zimbabwe kinakumbwa na vita ya ndani kwa ndani kuhusiana na nani atarithi nafasi ya Rais Mugabe, ambaye ameongoza tangu uhuru wa taifa hilo.

Hivi karibuni, ofisa mwingine mkuu wa chama tawala, Robert Gumbo, amenukuliwa akizungumza na waandishi wa habari akisema Rais Mugabe amegeuza chama kama mali yake binafsi.

Gumbo alisema lengo kuu la Rais Mugabe lilikuwa kuendeleza uongozi wa chama kwa niaba ya mke wake, Grace.