Wazalishaji wakubwa wa mifuko mbadala mkoani Kilimanjaro wameingiwa hofu ya kushindwa kufanya biashara yenye ushindani kutokana na wimbi kubwa la shehena ya mifuko hiyo isiyokuwa na ubora kuingizwa nchini kwa kasi kupitia njia za magendo na kuingizwa sokoni bila kulipiwa ushuru.

Mifuko hiyo inaingizwa nchini kila uchao na wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na biashara za magendo mipakani huku wilaya za Siha, Rombo, Mwanga na Same zinazopakana na Kenya zikiwa ndizo njia kubwa za kupitisha mifuko hiyo.

Meneja Mkuu wa kampuni tanzu za Harsho Group, ambao ni wazalishaji wakubwa wa  mifuko mbadala, Joseph Njeru, ameliambia JAMHURI  kuwa mifuko mingi inayoingizwa sokoni kutoka nchi jirani haikidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango nchini (TBS).

Amesema viwango vinavyokubaliwa na TBS na ambavyo kampuni hiyo inatengeneza ni uzito wa gramu 70, lakini mifuko mingi inayoingizwa hapa nchini kutoka nchi jirani ina uzito wa kati ya gramu 50 na 35.

“Unapozalishaji mifuko yenye uzito wa juu na gharama zake zinakuwa juu, hivyo hivyo unapozalishaji mifuko yenye uzito wa chini gharama zake lazima ziwe chini. Sasa sisi tunazalisha kwa gharama kubwa lakini mifuko inayoingizwa nchini uzito wake upo chini,” amesema.

Amesema kutokana na ushindani katika soko, TBS wanapaswa kuhakikisha kuwa wazalishaji na waagizaji wa bidhaa zote wanazingatia viwango vilivyowekwa ili kutowaumiza wale wanaotimiza masharti.

“Tatizo si kuingizwa kwa mifuko kutoka nje ya nchi, tatizo ni kuingizwa kwa mifuko ambayo haikidhi viwango vilivyowekwa. Kama wote tutazalisha mifuko ya gramu 70 tunaweza kabisa kukabiliana na soko vizuri na tuna uhakika mifuko yetu tunayozalisha hapa nchini itauzwa kwa bei ndogo ikilinganishwa na ile inayoingizwa kutoka nje,” amesema.

Mkurugenzi wa Harsho Group, Harold Shoo, amesema pamoja na kuwasilisha kilio chao kwa mamlaka husika juu ya uingizwaji wa mifuko hiyo iliyo chini ya viwango, bado hakuna lililofanyika kuidhibiti.

Amesema wamefanya vikao vyingi na mamlaka za udhibiti wa ubora pamoja na viongozi wa Wizara ya Viwanda kuhusu kilio chao bila kupatikana ufumbuzi wowote.

Awali TBS iliruhusu kampuni hiyo kutengeneza mifuko mbadala yenye uzito wa gramu 50 lakini baadaye ikazuia uzalishaji huo na kusisitiza kiwango kinachotakiwa ni uzito wa gramu 70 lakini pamoja na kusisitiza ujazo huo TBS imeshindwa kuwalinda wazalishaji wa ndani katika kukabiliana na uingizwaji holela wa mifuko hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, amesema uingizwaji wa mifuko mbadala isiyokuwa na ubora unaotakiwa kutoka nje ya nchi ni changamoto kubwa kwa wazalishaji wa ndani.

“Pale TRA tuna chumba kikubwa sana tumejaza hiyo mifuko ambayo haina ubora baada ya kuikamata ikiingizwa nchini kinyemela. Lakini wengi wa wanaoingiza mifuko hiyo ni kina mama, sasa hapa lazima tuangalie namna ya kuwasaidia, maana wapo waliokopa mikopo kutoka kwenye Vicoba, Saccos na kwenye mabenki,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, amezunngumza na JAMHURI na kuweka wazi kuwa shirika lake liliweka vigezo vinne kwa wazalishaji na waagizaji wa mifuko hiyo na ambavyo sharti vifuatwe kwa kila mzalishaji.

Ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na uzito usiopungua gramu 70, mifuko hiyo iwe yenye uwezo wa kurejelezwa, mzalishaji sharti aweke anwani kwenye mifuko anayozalisha au nembo ya biashara na sharti la nne, ubora wa mifuko hiyo uwe umethibitishwa na TBS.

Pamoja na waagizaji, TBS pia imekiri kuwapo kwa baadhi ya wazalishaji wa ndani wanaozalisha mifuko chini ya viwango vilivyowekwa.

“Shirika kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kama vile Baraza la Udhibiti wa Mazingira (NEMC), TRA na Jeshi la Polisi tunafanya ukaguzi sokoni na mipakani kukamata mifuko isiyokidhi viwango vyetu,” amesema.

By Jamhuri