Katikati ya mivutano ya kibiashara kati ya China na Marekani, mgahawa wenye mtandao mkubwa nchini Marekani umeanza kujipenyeza China kibiashara.

Hali hiyo inajitokeza katika wakati ambao hivi karibuni Marekani na China zimeonyesha kutunishiana misulu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutishia kuweka tozo ya takriban dola za Marekani bilioni 300 kwa bidhaa za China ambazo awali hazikuwa zimetupiwa jicho kali la kimapato.

Inaelezwa kuwa Marekani imekuwa katika jitihada za kuuzubaisha uchumi wa China kwa kadiri inavyowezekana, kwa mbinu mbalimbali, na mwezi uliopita nchi hiyo iliweka rekodi ya kiwango cha chini ya wastani wa ukuaji wake wa uchumi kwa maana ya asilimia 6.2, rekodi ya kipekee katika kipindi cha miaka 27.

Mtandao wa migahawa ya uuzaji chakula imekuwa na mwenendo wa kufaidika na hali ya kuporomoka kwa uchumi kwa sababu wateja wake wamekuwa wakitafuta unafuu zaidi, kwa mujibu wa Aaron Allen, mmiliki wa taasisi ya kimataifa katika masuala ya ushauri wa migahawa inayoitwa Aaron Allen & Associates.

Hata kama kuna hali ya kuporomoka, ukuaji wa uchumi wa China bado uko juu dhidi ya ule wa Marekani na kwa idadi ya watu bilioni 1.4, China ni soko linalovutia zaidi wawekezaji wa mitandao ya migahawa ya kimataifa.

“Unapotazama fursa zilizopo, ni dhahiri taasisi za kibiashara za Marekani zinaweza kujipenyeza China,” anasema Allen. Hata hivyo, migahawa inaweza kuhisi nguvu hiyo ya misukosuko kati ya mataifa hayo.

Mgahawa wa McDonald

Mtandao wa kimataifa wa migahawa ya McDonald unatajwa kuwa na mipango ya kufungua migahawa yake zaidi ya 400 China hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, 2019, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa miaka mitano wa kuongeza vituo vyake vya biashara (migahawa) kufikia 4,500 mwaka 2022.

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa McDonald, Steve Easterbrook, anasema kampuni yake imekuwa na imani kubwa kwamba uwekezaji wake nchini China utadumu katika mustakabali mwema.

 “Kuna hali ya ushindani wa kibiashara, ushindani mkubwa tu.  Tumeshuhudia hatua kubwa inayofanywa na watu katika kutanua biashara zao, jambo la kuvutia ni kwamba soko ni kubwa bado,” amesema CEO na kuongeza: “Kuna kundi la watu wa uchumi wa kati, hili ni muhimu kibiashara.”

Hivi karibuni mtandao mwingine wa kimataifa wa migahawa duniani maarufu kwa jina la Popeyes Louisiana Kitchen, umetangaza kufungua migahawa 1,500 China katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Popeyes tayari wana vituo zaidi ya 6,000 China kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.

Migahawa mingine kama Burger King unatajwa kuwa na vituo zaidi ya 1,000 vya biashara China. Mgahawa wa Canada, kupitia mtandao wake wa Tim Hortons mwaka jana ulitia saini kufungua vituo 1,500 vya biashara nchini China katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Mtandao mwingine wa migahawa kimataifa wa Starbucks unatajwa kulenga kutanua zaidi shughuli zake China kama ilivyo ndani ya Marekani.

Mtandao huo wa migahawa maarufu kwa uuzaji wa kahawa, mwaka huu umeadhimisha miaka 20 ya uwepo wake kibiashara nchini China, na una vituo zaidi ya 3,900 vya biashara China kwa takwimu za hadi mwishoni mwa Juni, mwaka huu. Malengo yake ni kufikisha vituo 6,000 vya biashara China hadi kufikia mwaka wa fedha 2022.

By Jamhuri