Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ametajwa kuwa kiongozi aliyependa kutumia vyombo vya habari kuhamasisha ukombozi wa nchi za barani Afrika kutoka katika utawala wa kimabavu wa Wakoloni.

Dokezo hilo limetolewa na mwandishi wa habari mkongwe hapa nchini, Wilifred Miigo, katika mahojiano maalum na JAMHURI Dar es Slaam, hivi karibuni.

“Mwalimu alilipatia msukumo na kipaumbele suala la ukombozi wa nchi za Afrika, alitaka zote ziwe huru, na alitumia sana ‘media’ kuhamasisha suala hilo, ingawa alikuwa mkali kwa mwandishi aliyekosea habari,” amesema Miigo ambaye kwa sasa ni Ofisa Uhusiano Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania.

Hata hivyo, Miigo amesema kwa sasa uhuru wa vyombo vya habari umeongezeka ikilinganishwa na enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere.

Amesema Mwalimu Nyerere pia alikuwa na utaratibu wa kuelimisha watu kwanza kuhusu masuala anayotaka kuzungumzia ili kuhakikisha hotuba zake zinaeleweka vizuri kwa watu wote.

“Mwalimu pia alikuwa na upeo mkubwa katika masuala ya uchumi, siasa na utamaduni wa nchi mbalimbali, lakini pia aliamini alichokuwa anakizungumzia,” ameongeza. Miigo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa waandishi wa habari kujenga tabia ya kutumia mitandao mbalimbali kupata habari.

“Tofauti na zamani, siku hizi kuna vyanzo vingi vya habari, kuna mitandao mingi inayostahili kutumiwa na waandishi wa habari kupata habari,” amesema.

825 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!