Misamaha ya kodi ilivyoumiza nchi

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/2016 imefichua jinsi nchi inavyopata hasara kutokana na misamaha ya kodi iliyotolewa na Serikali.
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha matumizi yasiyostahiki ya misamaha ya kodi kwa wanufaika wasiostahili Sh bilioni 3.46.
Katika mapitio ya ripoti za kiuchunguzi wa kodi za tarehe 31 Mei, 2016 yalibaini manunuzi ya magari 238 kutoka nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2012 na 2014 kwa kutumia majina ya walipakodi wawili; ambapo magari 175 yaliingizwa nchini kwa kutumia jina la M/s Lake Trans Ltd na magari mengine 63 yaliyobaki yaliingizwa nchini kwa kutumia jina la mlipakodi M/s State Oil (T) Ltd. Magari yote yalisajiliwa na kumilikiwa na walipakodi wasiostahiki.

Orodha ya magari yaliyonunuliwa kutoka nje ya nchi na kupewa msamaha wa kodi kwa wanufaika wasiostahiki ni kama ifuatavyo:
Kampuni ya A. Gure Transport Ltd, magari 110, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 1,540,563,984.38
Al-Hushoom Investment, magari 58, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 58 957,997,155.02
Lake Trans Ltd, magari 5, kiasi cha kodi inayodaiwa sh 70,496,098.40. E. Awadh & Co. Ltd magari 24, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 363,238,932.25
Kampuni nyingine ni ATN Petroleum Co. Ltd magari 11, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 169,927,729.92. Simera Transport Ltd magari 6, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 71,137,753.92. FAA Truck (T) Ltd, magari 18, kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 192,809,247.31. Bafadhil Transports Ltd, magari 6 kiasi cha kodi inayodaiwa Sh 88,837,365.51.

Jumla ya magari ni 238 na yaliingizwa nchini na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 3,455,008,266.71 kutokana na kutolipiwa kodi stahiki.
Hali kadhalika, ripoti hiyo imebainisha kuwa wanunuzi wa magari hayo walikataa kuwa hawakununua magari hayo.
“Hii inamaanisha kuwa uhalali wa misamaha ya kodi iliyotolewa ilikuwa ni ubadhirifu kwa lengo la kuidanganya Serikali ili kukwepa kulipa mapato ya Serikali bila Serikali kufahamu; hivyo, suala hili linashughulikiwa na polisi kitengo cha uchunguzi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Swali la msingi ni kuwa iliwezekana vipi umiliki wa magari haya uliwezekana kusajiliwa kabla ya kulipa kodi iliyotolewa misamaha ya kiasi cha Sh 3,455,008,267, au ni kwa namna gani magari haya yaliyopewa misamaha ya kodi yalinunuliwa na wanufaika ambao hawakustahili kupewa misamaha ya kodi.
CAG anasema kwamba kwa namna yoyote ile, hii inathibitisha kuwa usimamizi wa mifumo ya utoaji wa misamaha ya kodi bado unahitaji kuboreshwa ili kupunguza matumizi mabaya ya misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara wasiostahiki.

Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha hatua za kuchukua ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali kwa kusema;

Ninaishauri Serikali;
(a)   Kuendelea kupitia upya motisha za kodi zinazotolewa kwa lengo la kupunguza viwango vya misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia moja (1%) au chini ya zao la ndani (GDP) na kuongeza kiwango cha makusanyo ya mapato.
 (b) Kuendelea kupitia sera za kiuchumi na kodi kwa lengo la kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija. Hili linawezekana kwa kuboresha ukaguzi na udhibiti wa motisha za kodi, kuimarisha usimamizi na uchunguzi dhidi ya matumizi ya motisha za kodi.
(b) Ichunguze na kukusanya kodi iliyotakiwa kulipwa yenye thamani ya Sh 3,455,008,266.71 kutokana na magari yaliyonunuliwa nje ya nchi na kisha kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa wote waliohusika.
(c) Kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi inayotolewa kutokana na ununuzi wa magari kutoka nchi za nje, kwa kuhakikisha kuwa magari hayo hayasajiliwi kwa kutumia majina ya watumiaji wengine zaidi ya watu waliyoyaagiza.
(e) Kuboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa misamaha ya kodi ya magari yanayonunuliwa kutoka nje ya nchi, kwa kuhakikisha kuwa magari hayo hayasajiliwi kwa kutumia majina ya watu tofauti na waliyoyaagiza.
Tathmini ya misamaha ya kodi
Tathmini ya mifumo ya udhibiti wa misamaha ya kodi iliyofanywa, inabainisha pia mifumo ya udhibiti wa misamaha ya kodi za mafuta yaliyonunuliwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya uchimbaji wa madini.
“Ulinganishi wa nyaraka za mafuta yaliyonunuliwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za matumizi ya uchimbaji wa madini zinazohusiana na kampuni za uchimbaji wa madini za Buzwagi, Bulyanhulu na Geita pamoja na mapitio ya mifumo inayotunza taarifa za bidhaa za mafuta kupitia kitengo cha forodha makao makuu, ulibaini jumla ya magari 49 na lita 4,248,802 za mafuta yalinunuliwa kutoka nje ya nchi.”
Hata hivyo, CAG anaeleza kuwa ofisi yake haikuweza kujiridhisha kuwa mafuta hayo yalipokewa na makampuni ya uchimbaji madini kwa sababu hakukuwa na nyaraka zinazothibitisha mapokezi ya mafuta hayo. Magari husika yaliondoka Dar es Salaam katika kipindi cha Oktoba, 2014 na Desemba, 2015.
“Nina shaka kuwa lita 4,248,802 za mafuta yaliyopewa misamaha ya kodi yanaweza kuwa yametumika kwa ajili ya matumizi mengine tofauti na shughuli za uchimbaji wa madini; hivyo, kuisababishia Serikali hasara ya ukosefu wa mapato.”
“Kadhalika, uchambuzi wangu wa nyaraka za matumizi ya mafuta yaliyopewa misamaha ya kodi katika kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Buzwagi uligundua lita 20,791,072 za mafuta katika kipindi cha miezi 18 kuanzia Julai, 2014 na Disemba, 2015 yalikuwa yamesafirishwa kwenda kwa mkandarasi – M/S Aggreko Company Ltd –  ambaye hakustahili kupewa msamaha wa kodi.”
Ripoti hiyo inaeleza kuwa thamani ya mafuta yaliyopewa misamaha ya kodi ilikuwa ni Sh 10,174,647,166. Usafirishaji wa mafuta kwenda kwa makampuni ambayo hayastahiki kunufaika na misamaha ya kodi ni kinyume na matakwa ya Agizo Na. 480 la Serikali lilitolewa tarehe 25 Oktoba, 2002 ambalo linataka kuachwa kutolewa kwa misamaha ya kodi za mafuta kwa makampuni ambayo hayastahiki kunufaika na misamaha hiyo.

Ushauri uliotolewa na CAG kwa Serikali:
(a) Kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na mafuta ambayo hayakupokewa na makampuni ya uchimbaji wa madini na kukusanya ushuru wa forodha wenye jumla ya kiasi cha Sh 1,599,031,214.
(b) Kufanya uhakiki na ufuatiliaji wa kila mara wa walipakodi wanaostahiki kupewa misamaha ya kodi ili kuhakikisha kuwa makampuni stahiki yanafuata  taratibu na matakwa ya sheria na kanuni, ili kuepuka hasara inayoweza kupatikana kutokana na utoaji wa misamaha ya kodi kwa wanufaika wasiostahili. Kuhakikisha makusanyo ya kodi ya mafuta ya Sh 10,174,647,166 yaliyosafirishwa kwenda kwa mkandarasi asiyestahiki inakusanywa.
(c) Kufanya ukaguzi na uchunguzi wa kila mara wa wanufaika wanaopewa misamaha ya kodi ili kuhakikisha kuwa makampuni yanatii sheria na kanuni; hivyo, kuepuka hasara inayoweza kutokea kutokana na matumizi tofauti ya misamaha.
Pia ripoti hiyo inaelezea kutokuwa na usimamizi unaoridhisha wa bidhaa zilizokaa katika maghala ya kulipiwa ushuru wa forodha na bidhaa zilizoruhusiwa kuingia ndani ya nchi kwa muda maalum.
Ukaguzi na uhakiki uliofanyika katika ofisi za Ushuru wa Forodha za mikoa na mipakani ulibaini kuwa bidhaa 704 zilikuwa hazijalipiwa kodi kwa zaidi ya miaka kumi (10) zikisubiri taratibu na hatua za utoaji mizigo inayotakiwa kulipiwa ushuru wa forodha na hazikuwa katika hali nzuri.
“Kipindi hiki ni zaidi ya kipindi kilichowekwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 42(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004, ambacho kinahitaji bidhaa zote ambazo zimekaa katika maghala yaliyo chini ya uangalizi wa Idara ya Forodha (Customs Warehouses and Customs Bonded Warehouses) kwa zaidi ya siku 60 ziuzwe kwa njia ya mnada wa wazi au kwa njia yoyote ambayo Kamishna ataona inafaa.”
Amesema kuwa kuchelewa kunadi bidhaa hizo kunaweza kusababisha hasara ya kukosa mapato ya Serikali kutokana na uchakavu wa bidhaa wakati wa mauzo.

Orodha ya bidhaa zilizokaa muda mrefu katika maghala ya kulipiwa ushuru wa forodha
Bagamoyo, Misugusugu idadi 62, Morogoro Morogoro idadi 12, Isaka idadi 10, Kigoma idadi 30. Rukwa 58, Kagera (Bukoba, Mtukula, Kabanga, Rusumo and Kyaka) idadi 90, Mwanza idadi 12, Sirari idadi 198, Mbeya, Tunduma 73. Kasumulu 10, Tanga, Horohoro, Pangani 70. Iringa, Makambako 62, Dodoma 9, Malindi 18. Jumla ya bidhaa zilizokaa muda mrefu bila kulipiwa ushuru ni 704.
Mapitio ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabau za Serikali katika rejesta zinazohifadhi taarifa za bidhaa zilizonunuliwa kutoka nje ya nchi na kuruhusiwa kuingia ndani ya nchi kwa muda maalumu katika mipaka ya Mtukula na Namanga, ulibaini bidhaa zenye thamani ya Sh 42,892,721,756 ambazo zilitakiwa kulipiwa ushuru wa forodha wenye thamani ya Sh 2,461,287,015 hazikuweza kusafirishwa nje ya nchi kwa kipindi cha zaidi ya miezi 12 na hakukuwa na vibali vilivyotolewa kisheria kuruhusu kuongezwa kwa muda wa bidhaa hizo kuendelea kukaa nchini.
Pia, hii ilibainika pia kwa magari 952 ambayo yaliruhusiwa kuingia nchini na kupewa kibali cha kukaa kwa muda maalumu kati ya mwaka 2015 hadi Juni, 2016. Hata hivyo hakukuwa na ushahidi unaothibitisha kuwa magari haya yaliondoka nje ya nchi baada ya kwisha kwa kipindi yaliyoruhusiwa kukaa nchini kinyume na Kifungu cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Forodha Na. 117(3) ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.
“Kwa mtazamo wangu, kuwepo kwa bidhaa zilizokaa zaidi katika maghala ya kuhifadhia bidhaa zikisubiri kulipiwa ushuru wa forodha na magari yaliyokaa zaidi ya muda ulioruhusiwa, kunaonesha usimamizi usioridhisha wa bidhaa zilizokaa katika maghala ya kulipiwa ushuru wa forodha na bidhaa zilizoruhusiwa kuingia ndani ya nchi kwa muda maalumu kinyume na Kifungu Na. 117(3) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.”  
Ripoti hiyo imeeleza kuwa upungufu huu unatoa mianya kwa wafanyabiashara wasio waaminifu, hivyo, Serikali kushindwa kukusanya kodi stahiki.

1438 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons