Umuhimu Wa Misitu Katika Maeneo ya Vijiji

Tanzania Bara ina vijiji vingi na kwa bahati nzuri vipo vijiji vyenye maeneo mazuri ya misitu ya asili na vingine vinayo, lakini imeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zisizo endelevu.

Kwa jumla rasilimali muhimu vijijini ni ardhi na misitu ya asili, rasilimali ambazo zinatumika sana kwa shughuli za kilimo na ufugaji. Kama nilivotangulia kueleza, ipo mikoa yenye vijiji vilivyo na rasilimali misitu ya kutosha. Kinachotakiwa hapa ni juhudi za kuvisaidia vijiji husika viweze kunufaika na rasilimali walizonazo.

 

Ukiondoa ardhi, misitu ya asili pamoja na ile ya kupandwa ndiyo rasilimali muhimu inayoweza kusaidia vijiji kupunguza umasikini kama si kuutokomeza kabisa. Kusema kweli ardhi na misitu ya asili katika maeneo ya vijiji ndiyo mitaji yao ya kwanza na ikitumika vizuri na kwa njia endelevu vijiji vyetu vitakuwa mfano katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 

Hata hivyo, kitu cha kusikitisha ni kuwa matumizi ya rasilimali ardhi na misitu katika vijiji vingi yamekuwa si endelevu. Kwa miaka 50 ya Uhuru wetu kilimo vijijini hakijawa endelevu kwa msingi kwamba mbinu za wakulima wengi ni kutegemea jembe la mkono hivyo matumizi ya matrekta na majembe ya kukokotwa na wanyama (maksai) pamoja na matumizi ya mbolea na mbegu ni kwa kiwango cha chini mno. Nadiriki kusema kuwa shughuli zetu za ugani katika sekta za kilimo, mifugo na misitu hazijatoa mafanikio tuliyoyatazamia katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Taifa letu.

 

Kutokana na hali hiyo, bado tunashuhudia kilimo cha kuhamahama ambako eneo lenye msitu au uoto wa asili linafyekwa na kuchomwa moto (slash & burn farming system). Mkulima baada ya kufanya hivyo huweza kutumia eneo alilofyeka kwa muda mfupi (sana sana miaka mitatu) na hatimaye kuhamia sehemu nyingine na kufanya kama alivyofanya kwenye sehemu aliyotoka.

 

Hali hiyo imekuwa inajirudia mwaka hadi mwaka kwenye maeneo mengi vijijini yenye misitu au uoto wa asili, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa kwa misitu yenyewe na mazingira kwa jumla. Vilevile, kilimo duni husababisha wakulima kupata mavuno haba na hivyo kuendelea kutegemea rasilimli misitu kuwa katika hali ngumu maana ni mapanga, mashoka na kuichoma moto hasa nyakati za kiangazi.

 

Ardhi inayotumika kwa kilimo kisicho endelevu hupoteza rutuba yake haraka na kumfanya mkulima kuhamahama kila mara na hivyo kusabisha uharibifu mkubwa kwa misitu ya asili na mazingira ikiwamo kuvuruga vyanzo vya maji na ardhioevu.

 

Katika Tanzania Bara jitihada za kushirikisha wananchi katika masuala ya kuhifadhi misitu zilianza miaka ya 1980 na 1990 kupitia uhisani wa Serikali ya Sweden chini ya shirika lake la misaada SIDA.

 

Kupitia programu iliyokuwa ikijulikana: Misitu kwa Jamii (Community Forestry), Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaaa (OW-TAMISEMI) ilitekeleza programu hiyo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Kagera na Singida.

 

Hivyo Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kutambua umuhimu wa kushirikisha vijiji na wadau wengine kwa lengo la kuhusisha jamii katika usimamizi na umilikaji rasilimali misitu. Mkazo katika kutekeleza shughuli za misitu kwa jamii uliwekwa kwenye kuhifadhi misitu ya asili kwa manufaa ya vijiji, lakini pia kuongeza nguvu katika kupanda miti vijijini (Village Afforeststion).

 

Ingawa mafanikio hayajawa ya kuridhisha sana, bado dhamira ya kufanya hivyo ilikuwa nzuri. Bustani nyingi za miti zilianzishwa katika maeneo mbalimbali wilayani, vijijini na katika maeneo ya shule.  Watu walipewa elimu ya kutunza bustani za miti pamoja na kupanda miti katika maeneo yao na shule ziliotesha miche ya kutosha.

 

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Programu ya Misitu Vijijini ilibadilishwa na kuwa ya kushughulikia usimamizi wa ardhi katika ujumla wake (Land Management Programme-LAMP). Kupitia programu ya LAMP, yalifanyika majaribio katika misitu ya Mgori (Singida), Duru-Haitemba (Babati) na SULEDO (Kiteto) ambayo ilimilikiwa na vijiji zaidi ya kimoja.

 

Kutokana na uzoefu uliopatikana, Wizara iliweza kufanya mabadiliko muhimu katika Sera na Sheria ya Misitu kwa kuingiza suala la usimamizi shirikishi wa misitu na hivyo kuwesheza jamii, vijiji na watu binafsi kuwa wadau muhimu katika kutunza misitu ya asili na kupanda miti kwa faida yao na Taifa letu kwa jumla.

 

Kulingana na Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya Misitu ya 2002, jamii nchini Tanzania sasa ina uwezo wa kusimamia, kufanya doria, kutoza faini kwa watumiaji haramu wa rasilimali misitu, na kutoa vibali kwa mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu wanayoimiliki.

 

Vilevile wanayo fursa nzuri na mamlaka ya kutunga Sheria Ndogo Ndogo zisizokinzana na sheria mama ya misitu na kuweka kanuni za usimamizi na matumizi endelevu.

 

Pamoja na hayo, Sheria ya Misitu inatoa vivutio kwa jamii kuhifadhi maeneo ya msitu katika ardhi ya kijiji ambavyo ni pamoja na:-i).  Kusamehewa mrabaha wa serikali kwa mazao ya misitu katika misitu waliyoihifadhi na wanaisimamia na kuitumia kisheria;

ii). Kubakiza asilimia 100 ya maduhuli yatokanayo na mauzo ya mazao ya misitu,

iii). Kutoza ushuru kwa mazao ya misitu usiokuwa chini ya viwango vilivyowekwa na serikali kisheria na kutoza faini kwa waharifu;

iv). Kusamehewa ushuru wa serikali za mitaa;

v).  Kusamehewa miti iliyohifadhiwa (reserves trees) inayopatikana katika eneo la kijiji;

vi). Kutaifisha mazao ya misitu na zana zilizotumika kufanya uhalifu.

 

Kwa misingi hiyo Serikali za vijiji na viongozi wa jamii na kimila wanatakiwa kuwa makini sana katika kuhakikisha kuwa vijiji na jamii wanapata manufaa yanayotokana na kuwapo na rasilimali misitu (hasa ile ya asili) katika maeneo wanayoyasimamia. Hapa suala la Uongozi Bora na imara katika vijiji na vikundi vya kijamii ni muhimu sana.

 

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012. Anapatikana kwa simu na. HYPERLINK “tel:0756%20007%20400”0756 007 400.

By Jamhuri