Wadau mbalimbali wameituhumu mitandao inayojishughulisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia, kwa kile kinachodaiwa kuwa imekuwa ikitumika kisiasa ikiwa ni pamoja na kuitumia mitandao kama sehemu ya vitegauchumi vyao.

Vyanzo vya habari vimeidokeza JAMHURI kwamba asilimia kubwa ya mitandao hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa maneno pasipo vitendo, na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofanyiwa ukatili kila mwaka.

“Kuongezeka kwa ukatili si picha nzuri kwa mamlaka husika, hivyo wanapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa uzalendo ili kuleta matokeo chanya kwa Taifa,” anasema mtoa taarifa.

Anasema kwamba mitandao hiyo imekuwa kama kitegauchumi kwa baadhi ya watu kutokana na kuitumia kujipatia fedha kutoka ndani na nje ya nchi, kwa kisingizio cha kusaidia jamii kuondokana na matatizo yanayotokana na ukatili nchini.

Anabainisha kuwa taasisi hizo hazisaidii kuondokana na ukatili nchini kama zinavyojitanabaisha, bali baadhi zimekuwa zikitumika kisiasa na kiuchumi.

Akizungumzia madai hayo, Afisa, Kitengo cha Jinsia, wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Godfrida Jola, amesema kuwa ukatili unaongezeka lakini kwao ni matokeo mazuri kutokana na elimu inayoendelea kutolewa.

Jola anasema kuwa licha ya ukatili kuongezeka, lakini kuna baadhi ya ukatili unapungua, huku baadhi ya mikoa ukiendelea kuongezeka kutokana sababu mbalimbali. 

Anasema kuwa maeneo ambayo ukatili unaongezeka ni mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora, Songea pamoja na Iringa kutokana na TAMWA kuwa na changamoto ya kukosa fedha za kutoa elimu kwa jamii kwa wakati.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Jeshi la Polisi watoto 2,571 kila mwaka wanafanyiwa ukatili wa kubakwa, jambo ambalo ni hatari kwa kizazi kijacho na nchi kwa ujumla.

Anabainisha kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa Kipolisi wa Kinondoni, zipo kesi 187 zinazohusu matukio ya ubakaji, jambo ambalo si rafiki kwa umma.

“Kuongezeka kwa idadi ya watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia inatokana na mitandao kufanya kazi ipasavyo ya kutoa elimu kwa umma,”anasema Jola.

TAMWA ina umri wa miaka 29 ikiwa inafanya kazi ya kupinga ukatili ya kijinsia kwa wanawake kwa kushirikana na  wahisani mbalimbali kutoka nje nchi ikiwamo Shirika la Misaada la Sweden.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF), Anna Meela, anasema kuwa tatizo lililokuwapo ni mtazamo potofu wa baadhi ya watu.

Anasema kwa upande wao wanaendelea kutekeleza majukumu katika kuhakikisha kila mtu anakuwa na uelewa mpana kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na kutoa ushauri wa kisheria. 

Meela anasema kuwa jambo la muhimu ni kuwapo ushirikiano wa karibu wa Watanzania wote katika kuelimisha jamiii na si kutegemea vyombo vya dola pekee na taasisi nyingine.

“Kuongezeka kwa ukatili kwetu ni sahihi kwani katika mipango yetu hapa awali twakimu zilikuwa ndogo, hivyo ukatili hauwezi kupungua kabla ya kuongezeka, sasa watu wameanza kuelewa wakifanyiwa jambo la ukatili wa kijinsia wanatoa taarifa,” anasema Meela. 

Shirika la WILDAF lina miaka 19 hapa nchini likiendelea kufanya kazi zake mbalimbali ikiwamo kupinga ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na msaada kutoka taasisi mbalimbali nje ya nchi. 

Afisa Programu za harakati, ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai, anasema kuwa kwao ni changamoto, lakini tatizo lililopo ni ufuatiliaji wa kesi kwani zimekuwa zikichukua muda mrefu kutolewa majibu.

“Ili kupunguza ukatili hapa nchini, kesi za aina hiyo zinatakiwa kupatiwa majibu mapema ili kuwe na fundisho kwa watu wanaokuwa na tabia ambazo si rafiki kwa jamii,” anasema Sangai.

Anasema kuwa tayari wameanza kuwajengea uwezo askari waliopo katika dawati la jinsia pamoja na makundi mbalimbali ili waweze kusaidiana kuondokana na ukatili wa kijinsia nchini.

Sangai amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwa na utamaduni wa kutembelea vijiji ambavyo hakuna vituo vya polisi kwa kuweka kambi angalau mara moja kwa mwezi ili kutoa fursa kwa wananchi kuripoti matukio ya ukatili wanayokumbana nayo.

TGNP wana umri wa zaidi ya miaka 20 katika kufanya kazi za harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi pamoja na masuala mbalimbali.

Akizungumza na JAMHURI, Msemaji wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto, Erasto Chingoro, anasema kuwa mashirika ya yasiyo kiserikali yana mchango mkubwa kwa Serikali katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.

Anasema ni kweli ukatili unaongezeka lakini haina maana mashirika hayo hayafanyi kazi, kwa sababu yamekuwa yakifanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu aina za matukio ya ukatili wa kinjisia na kuwashauri.

Anasema kuwa afisa wa Ustawi wa Jamii ngazi ya Kata pamoja na Halmshauri, wamekuwa wakifanya kazi na mashirika hayo kwa lengo la kuwajengea Watanzania uelewa mpana kwa jamii.

“Kiukweli, jamii imeanza kuhamasika na kuibua maovu yanayofanyika katika jamii kwa kutoa taarifa ya kufichua matukio ya ukatili na kuwa tofauti na kipindi cha nyuma,” anasema Chingoro.

Anasema kuwa jamii imekuwa ikitoa taarifa katika mamlaka zote zinazohusika ikiwamo madawati ya jinsia, ustawi wa jamii pamoja na vyombo wa habari ambavyo vimekuwa vikiripoti taarifa za matukio hayo.

Chingoro anasema kuwa majukumu ya mashirika hayo ni pamoja na kutoa elimu, ushauri kwa wale ambao wamekuwa na makovu ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia ili waendelee kujiamini pasipo kukata tamaa katika jamii.

By Jamhuri