Mkenya ‘kihiyo’ aongoza shule ya kimataifa Dar

Raia wa Kenya asiyekuwa na sifa za ualimu ameajiriwa kuwa Mkuu wa Shule za Kimataifa za St. Columba’s jijini Dar es Salaam; JAMHURI limebaini.

Shule hizo zinazomilikiwa na Kanisa la Presbyterian Church of East Africa, lenye Makao Makuu nchini Kenya, ziko Upanga na Makongo jijini humo.

Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na mambo mengine, imevalia njuga uboreshaji elimu, ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki wa walimu, jambo ambalo, ama halijatekelezwa, au linafunikwa katika shule za St. Columba’s.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini Mkuu wa shule hizo zinazotoa elimu ya msingi kwa lugha ya Kiingereza, David Wathiga, hana elimu wala sifa za kushika wadhifa huo.

Ni kwa sababu hiyo, imebainika kuwa alishawahidi kufukuzwa asifanye kazi hiyo, lakini akarudi kinyemela kwa msaada wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji na wenzao wa Idara ya Kazi wanaohusika na ajira nchini.

“Huyu alikuwa mwalimu wa kawaida katika Kampasi ya Makongo mwaka 2011, kabla ya kufukuzwa kutokana na uwezo mdogo wa kufundisha masomo ya sayansi na hisabati. Kila mmoja anashangaa ni vigezo gani vilitumika kumrudisha na kumpa wadhifa wa juu kabisa,” kimesema chanzo chetu cha habari.

Wakati anatimuliwa, Meneja wa Shule katika Kampasi ya Makongo alikokuwa akifundisha alikuwa Steven Kabumba, na Katibu wa Bodi ya Shule akiwa ni Vida Mwasalla. 

Kabla ya kuachishwa, uongozi wa shule ulimtaarifu kwa maandishi kuwa usigeweza kumtafutia kibali kingine cha kuendelea kufanya kazi nchini baada ya kubaini hana uwezo wa kufundisha.

Mbali na kuwa na kiwango cha chini katika utendaji, imebainika kuwa Wathiga alisoma katika Chuo Cha City & Guilds nchini Kenya ambacho mitihani yake haitambuliwi na Baraza la Mitihani nchini humo (KNEC). Chuo hicho kimekuwa hakitambuliwi kitaaluma mahala popote.

Kwa mujibu wa vyeti ambavyo navyo vinavyodaiwa kuwa ni vya kughushi, Wathiga ana Diploma ya Elimu ya Kiroho (Theological Education by Extension).

Taarifa zaidi zinaonesha Wathiga aliajiriwa shuleni hapo mwaka 2014 baada ya kukingiwa kifua na bodi ya shule hiyo ambayo inadaiwa kuwa ndio ‘inambeba’ kutokana na kuongozwa na Wakenya wenzake.

“Katibu na Mwenyekiti Bodi ya Shule ni raia wa Kenya, na hao ndio wanaomkingia kifua. Bodi hiyo hiyo ndio ilitoa amri ya kurejea kwake ikataka afanyiwe usaili ambao hata hivyo haukufata taratibu,” kimesema chanzo chetu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Veronica Msinjili, ameulizwa na JAMHURI juu ya kurejeshwa kinyemela kwa Wathiga, naye amesema kwa ufupi, “Mimi hiyo sijui”. 

Awali, JAMHURI liliwasiliana na Wathiga, simu yake iliita bila kupokewa. Lakini taarifa zilizopo ni kwamba mkuu huyo amekwenda nchini Kenya.

Msaidizi wake ambaye pia ni msimamizi wa shule hiyo kwa upande wa Makongo, Pauline Mang’ere, alipopigiwa simu aliahidi kuwa angetoa namba mbadala ya Wathiga. Alipotafutwa mara ya pili akaghairi kutoa namba hiyo.

“Aliyekupa namba yangu si akupe ya David? Mimi kwanza sikuelewi na ulimwengu wa sasa umebadilika, kama unamhitaji nenda Upanga utamkuta. Yeye ndiye Mkuu wa Shule, na siyo mimi,” amesema Pauline.

Imebainika kuwa mbali na Wathiga, kuna watumishi wengine katika shule hiyo wasiokuwa na taaluma ya ualimu, lakini wamekuwa wakifundisha.

“Kuna walimu wengine hapa wanafundisha bila kuwa na taaluma ya ualimu, na vipindi vyao mara nyingi wanafunzi hawafanyi vizuri,” kimesema chanzo chetu.

Uongozi wa juu wa shule hiyo umeshikwa na raia wa Kenya, hali inayolalamikiwa na baadhi ya watumishi Watanzania ambao wanadai kuwa na sifa hata kuwazidi wageni hao.

1548 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons