Mkutano wa Mkulo na METL
Juni 8, 2010 zikiwa ni siku chache kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa na kuingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu, Mkulo alianzisha mchakato wa kumuuzia kiwanja hicho METL kwa kuitisha mkutano kati yake, watendaji wa CHC wakiongozwa na Metusela Mbajo na Ridhiwani Masudi aliyemwakiliza Msajili wa Hazina.

Katika mkutano huo walirejea historia ya mgogoro wa kiwanja, na ndani ya siku tatu, METL waliandika baraua  kwa Msajili wa Hazina yenye Kumb. Na. METL/PLOT/2010/10-06 ya Juni 20, 2010 ikimweleza kuwa Waziri wa Fedha Mkulo alikuwa amekabidhi suala la kiwanja kwake (Msajili wa Hazina), na mambo makuu ya msingi yalikuwa mawili.

Kwamba walijadili suala la mgogoro wa kiwanja Na 192 kutokuwa na njia uliodumu kwa muda mrefu na kuwakosesha uwezekano wa kupata Hati ya Kiwanja (kwa mujibu wa sheria kiwanja kisicho na njia hakipatiwi hati). Suala la pili katika barua hiyo iliyosainiwa na G. Dewji, wakasema sasa wapo tayari kukinunua kiwanja hicho kwa bei iliyopendekezwa na PSRC mwaka 1999 ya dola 500,000.

Katika mkutano na Mkulo METL waliihakikishia Serikali kuwa pamoja na nia yao ya kununua kiwanja Na 10, METL ilikuwa tayari kulipa gharama yoyote, iwe ya kesi au itakayotokana na uamuzi huo wa kuuziwa kiwanja hicho.

By Jamhuri