Siku chache baada ya JAMHURI kuripoti tukio la watu wawili kuathiriwa na kinachodhaniwa kemikali mkoani Geita, hali za waathiriwa wa kemikali hizo wameanza kubabuka ngozi.

Wananchi hao wakazi wa kitongoji cha Kiomboi, kijiji cha Iririka kata ya Nyarugusu mkoani Geita, wameliambia gazeti hili matatizo waliyoyapata yanawaathiri kwa kiasi kikubwa kushiriki tendo la ndoa.

Waathiriwa hao – Jackson Msengi na Malemi Kang’ong’o –  wameamua kupaza sauti zao kuililia Serikali, wakiomba kusaidiwa kupata matibabu baada ya hali zao kuendelea kuwa mbaya kila kukicha.

Wakizungumza na JAMHURI, wakati wakielekea kuomba msaada kwa Mkuu wa Wilaya, waathiriwa hao wa kemikali   wamesema licha ya muda mrefu kupita tangu kupata madhara hayo, matibabu kwao yamekuwa kitendawili.

“Kama unavyotuona, hali zetu zinabadilika kila kukicha na  ngozi ya mwili inakuwa nyeupe kama walivyo wenye ulemavu wa ngozi (albino), pia hatuwezi kufanya tendo la ndoa kwani maumivu ni makali sana sehemu za tumbo na kwenye nyonga,” anasema. 

Naye Msengi, amesema: “Sasa kwa vile hatujapata msaada wowote wa kuchukuliwa vinasaba na kujua tatizo ni nini, tumeingiwa na hofu na ndiyo maana tumefika katika ofisi ya mkuu wa wilaya kumweleza na ikibidi aingilie kati ili tusaidiwe, vinginevyo tumeanza kukiona kifo,’’ amesema Kang’ong’o.

Waathirika hao wameiomba Serikali kuwawezesha kuchunguzwa ili kubaini madhara yaliyoko ndani ya ngozi zao ili watibiwe baada ya mmiliki wa ghala walilokuwa wakifanyia kazi, Richard Kasubi, kudai kuwa si waajiriwa.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi, ameahidi kulitolea taarifa tukio hilo huku akiomba apewe muda wa kulifuatilia kwa ukaribu zaidi.

“Ninaomba mnipatie muda ili nifuatilie suala la hawa vijana na nitalitolea ufafanuzi siku si nyingi,’’ amesema Kapufi wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.

Januari 3, mwaka huu, JAMHURI iliandika habari zinazohusiana na tukio hilo, huku lengo likiwa mamlaka husika kuingilia kati kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi hao lakini hadi sasa hakuna msaada wowote.

Hata hivyo, baada ya habari hiyo kutoka gazetini, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samweli Manyele, alimtaka mwandishi wa makala hiyo kuwasiliana na Wakala wa Afya na Usalama kazini (OSHA).

Prof. Manyele ameiambia JAMHURI, OSHA ndiyo wenye jukumu la kuchukua sampuli za waathirika wa kemikali na kuzipelea ofisini kwake kwa ajili kufanyiwa uchunguzi ili kubaini aina ya kemikali iliyotumika.

Akizungumza na JAMHURI, Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Mjawa Mohamed, ameahdi kufuatilia suala hilo huku akikiri ofisi yake kutopata taarifa. Amesema atalifuatilia na kulifanyia kazi haraka.

“Mara nyingi taarifa za matukio kama hayo huwa tunapewa na wamiliki wa sehemu ambazo wahusika walikuwa wanafanyia kazi, lakini kwa vile unasema mmiliki anadai yeye hakuwa amewaajiri…huyo anakimbia bure lakini mwisho wa siku atakayewajibika ni yeye,” amesema Mjawa.

Desemba 8, mwaka jana, watu hao walipewa kazi za kupakua kemikali za kuchenjulia marudio ya dhahabu aina ya lime, mifuko 600 kwa ujira wa Sh. 50,000/-.

Wapagazi hao wamesema walipofika majumbani mwao na kupata maji ya kuoga walianza kuhisi miwasho na maumivu makali sehemu zote ambazo walikuwa wanagusisha mifuko ya kemikali hizo.

“Desemba 10, tulikwenda kwenye zahanati ya Nyarugusu ambako tuliambiwa tutumie kwanza dawa tulizokuwa tumenunua dukani zikiisha ndiyo turudi kwa uchunguzi zaidi, ambapo tulifanya hivyo na kupitia kituo kidogo cha polisi Nyarugusu ambako tulipewa PF3 huku polisi wakishauri twende katika hospitali teule ya mkoa wa Geita kwa uchunguzi zaidi,’’ amesema Msengi.

Akizungumza na JAMHURI, Malimi Kang’ong’o amesema awali mmiliki wa ghala hilo alikuwa na majibu yasiyoridhisha na alifikia hatua ya kuwakashifu walipomueleza matatizo yaliyotokana na kazi ya kubeba kemikali.

“Siku alipopigiwa simu na uongozi wa kitongoji na kijiji alikuwa na majibu yasiyoridhisha kwani alituambia kwamba mtu akikupa jembe ukalime ukijikata ni nani alaumiwe? Lakini baada ya waandishi kumtafuta ametutumia Sh 200,000/- kwa ajili ya matibabu,’’ amesema Kang’ong’o

Kwa sasa watu hao wanatumia dawa walizopewa katika hospitali teule ya mkoa wa Geita, huku wakiendelea kuomba msaada ili kwenda kwenye hospitali kubwa kuchunguza kiwango cha madhara ya kemikali hizo katika miili yao.

Wakati wananchi hao wakidai hivyo, mmiliki wa kemikali hizo Richard Kasubi, ameendelea na msimamo wake kuwa, yeye hakuwa amewaajiri.

 

Afya na Usalama Mahali pa Kazi

Wakati Kasubi akidai si mwajiri wa watu hao huku akikiri mifuko waliyokuwa wakibeba ni mali yake, wajibu wa mwajiri kwa mjibu wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi, 2003 inamtaka mwajiri kutoa mazingira yenye afya, usalama na ustawi kwa wafanyakazi wake wote na kuhakikisha kurudi kwa maisha ya kawaida kwa wafanyakazi walioathiriwa.

Sheria hiyo inasema ni lazima mmiliki kutoa na kuendeleza kifaa na mifumo na utaratibu wa kazi ambao ni salama na bila hatari kwa afya ya wafanyakazi. Mwajiri lazima ahakikishe usalama na kutokuwapo na hatari ya kiafya katika utumizi, shughuli, uwekaji na usafirishaji wa kikorokoro na mali.

Lazima vifaa vya usalama kutolewa na kudumishwa katika kila eneo la kazi. Kamwe wafanyakazi wasihatarishwe kwa mnururisho; vitu vinavyowasha; mashine na vifaa hatari; au wanyama na wadudu na hatari; au ajenti zinazoambukiza au mizio; au kemikali hatari; au mazingira hatari wakati wa kufanya kazi kama mafanyakazi wa kilimo.

Mahali pa kazi na mazingira ya kazi ambayo ni salama, bila hatari ya afya na vifaa vinayotosha na mipango ya ustawi wa wafanyakazi kazini unafaa kudumishwa. Wafanyakazi wanafaa kujulishwa vyema kuhusu hatari yoyote ambayo inaweza kutokea na wanastahili kushiriki katika utendaji na ukaguzi wa hatua za usalama na afya.

Sheria hiyo inasema, lazima wafanyakazi watumie vifaa vya usalama kwa uangalifu na kufuata maagizo yaliyoamuriwa ili kudumisha afya yake na kumlinda dhidi ya kuumia. Kamwe mfanyakazi asihusike katika kitendo chochote ambacho kinazuia utekelezaji wa maagizo au matumizi mabaya au kusababisha uharibu au kupotea kwa njia zilizotolewa za ulindaji, usalama na afya ya wafanyakazi wengine. Lazima aripoti kwa mwajiri au msimamizi wa afya na usalama ikiwa hali dhaifu au isiyo salama itatokea.

Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi 2003 inahitaji waajiri kutoa kifaa cha kulinda (PPE) kwa wafanyakazi wanaohusika katika kazi hatari.

Ni lazima mwajiri atoe kifaa cha kinachofaa cha kulinda ikiwa wafanyakazi wanaachwa wazi kwa mazingira ya kuumiza au kifaa cha kudhuru. Aina ya PPE inayohitajika inatofautiana kulingana na kazi inayotekelezwa.

Sehemu ambayo vitu vyenye sumu vinazalishwa, kutunzwa au kuhifadhiwa, Mkaguzi Mkuu anaweza kumtaka mwajiri kutoa huduma za ziada kama mahali ya kuogea, kuandaa uchunguzi wa mara kwa mara wa afya toka kwa taasisi inayokubalika ikiwa ni pamoja na kutoa mavazi ya kujikinga.

865 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!