Mnyukano wa Spika, CAG wapamba moto

Mvutano kati ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, umepamba moto.

Kauli iliyotolewa wiki iliyopita na bingwa huyo wa masuala ya ukaguzi wakati akiwasilisha muhtasari wa ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2017/2018, imemwibua tena Spika Job Ndugai.

Akionekana kukasirika, Spika Ndugai amesema endapo Profesa Assad anaendelea kurudia rudia kauli ya ‘udhaifu’, ataitwa tena bungeni. “Tutakuita, na safari hii itakuwa mbaya zaidi,” amesema.

Amesema maneno ya kuudhi yanayotamkwa na CAG yanamgusa hadi Rais wa nchi, kwa kuwa kikatiba yeye ni sehemu ya Bunge.

“Ziko njia za kumaliza mambo kama haya. Mojawapo aende kwa Mheshimiwa Rais, ajieleze ‘Mheshimiwa Rais, nimepima nikaona nimekosea hapa na pale’…Rais ni sehemu yetu sisi. Rais ni sehemu ya Bunge. Hatupitishi sheria mpaka aweke mkono [sahihi] ndiyo iwe sheria, vinginevyo haiwezekani. Bajeti hii tutajadili, tutaweka vifungu wee hata tufanyeje bila kibali cha rais haiwezi kuwa bajeti…Kwa hiyo matusi yale anayoyatoa kwa kweli kwa kujua au kutokujua kwa kusema neno ‘Parliament of Tanzania’, maana yake rais yuko mle, spika yuko mle, baraza la mawaziri liko mle…sijui profesa [Assad] anajua haya au anajua kujumlisha na kutoa tu! Kwamba maneno haya anatukana kila mtu, sijui kama anajua haya maneno…na jamaa ni shujaa kwa kweli. Ana uthubutu, lakini ni uthubutu wa mbwa kumng’ata yule anayemlisha.

“Sina chuki binafsi na Profesa Assad, ni rafiki yangu, ndugu yangu, Mtanzania mwenzangu, jamaa yangu – wala Bunge la Tanzania halina ugomvi na mtu. Ugomvi wetu ni huo tu kwamba anatumia lugha ambazo ni za udhalilishaji,” amesema Spika Ndugai.

Kuhusu neno ‘dhaifu, amesema: “Neno hili ni la dharau na kejeli, hata katika maisha ya kawaida, wewe unamwita mtu jina fulani, anakuambia tafadhali jina hili silipendi…wewe unang’ang’ania unasema utaendelea kuniita…ni ustaarabu duniani? Tena unaahidi utaendelea kulitumia.

“Bungeni kamati zetu zilitoa kamusi zote hadi za Kenya, akaambiwa toa kamusi yako ya kihasibu wala hakuwa nayo. Neno lile [dhaifu] halina heshima kwa chombo cha mhimili kama Bunge la Tanzania. Hatusitahili neno hilo. Sisi tunafanya kazi nyingi zaidi kuliko item moja anayoifanyia kazi yeye CAG.

“Ni neno ambalo hatulipendi. Ningependa kutumia forum [jukwaa] hii kumwambia kuwa hatulipendi. Mtu mstaarabu utaacha. Unalipenda sana si ujiite wewe? Kama unalipenda sana jibatize useme kuanzia leo naitwa ‘dhaifu’. Na kuonyesha kwamba hatupendi jambo hilo, tumechukua hatua hata kwa wenzetu [wabunge]. Tumechukua hatua kali sana kwa Mheshimiwa Halima Mdee, ninyi wote ni mashahidi. Tumechukua hatua kali sana kwa Mheshimiwa Lema (Godbless). …kwa hiyo kurudia na kuahidi kuwa utarudia, tutakuita tena. Nadhani itakuwa mbaya zaidi.”

Spika Ndugai amegusia ‘kiburi’ cha Profesa Assad akisema inawezekana kikawa kinatokana na kiwango chake cha elimu.

Amesema mataifa ya Ulaya, hasa nchi za Nordic, ni nadra kumsikia mtu akijinasibu kwa usomi wake.

“Nordic, mtu akiwa profesa wewe ukamwita profesa fulani, anasema hapana. Hawapendi. Utamwita profesa kama kuna sababu ya kumwita, kwa mfano anataka kutoa mada fulani unawaeleza wale wanaotaka kusikiliza kwamba huyu anayetaka kuongea ni mtu mwenye wasifu fulani. Wale hawatembei na CV [wasifu] zao wamebandika usoni…kila saa profesa, profesa. John ni John, Juma ni Juma.”

Amesema rafiki yake raia wa Sweden amepata kumweleza kuwa tatizo la Waafrika wasomi ni kupenda kuwadharau wasiokuwa na elimu kama zao.

“Ananiambia ‘shida yenu ninyi mtu akishasoma anaona wengine wote mbuzi tu. Anaona kama akili zenu mbovu, hamtoshi’. Waandishi badala ya kuweka vizuri hili jambo tunamkuza, tunamfanya mungu-mtu. Katiba ipi iliyomruhusu mtu adharau wenzake? Lazima tukemee mambo haya. Tuwarudishe wasomi wetu mahali wanastahili kuwa, waone na wenzao nao ni binadamu wanapofanya uamuzi wa mambo fulani wana sababu zao za msingi. Wamefikiri, na hawa ni wawakilishi wa wananchi. Wabunge hawa wamechaguliwa na wananchi. Wameona hawa ni wawakilishi wetu, sasa wewe uwaone dhaifu, uwaone wajinga ndio hao.

“Narudia kumwambia rafiki yangu Mussa Assad hili jambo aliache, taarifa [ya ukaguzi] tutafanyia kazi kama ilivyo ada na Watanzania watapata mrejesho  kwa kila jambo ambalo limetajwa mle ndani. Sisi hatuwatuhumu watu haraka haraka au ovyo ovyo, hapana. Ametuletea queries, tutazifanyia kazi, lakini msisitizo wetu ni mmoja kwamba kwa kuwa Bunge lilishatoa uamuzi kwamba halifanyi kazi na mtu anaitwa Assad kwa sababu amelidhalilisha Bunge, uamuzi huo ni halali na hauingiliwi na mtu yeyote.

“Ni uamuzi wa Bunge kama ulivyo uamuzi mwingine wa Bunge, tena ni azimio la Bunge. Katika nchi za wenzetu kote ikifika mahali Bunge limeonyesha kutokuwa na imani nawe, unajiuzulu. Lakini si kazi yangu wala wajibu wangu. Anampa Mheshimiwa Rais wakati mgumu kweli. Sisi tumeshaamua hatufanyi kazi na mtu anaitwa Mussa Assad, sisi tutaendelea kufanya kazi na ofisi ya wananchi, ofisi ya ukaguzi ya taifa. Ofisi hiyo ina maofisa wengi, wengi wa kutosha kama lilivyo Bunge kwamba nikifa leo Ndugai Bunge la Tanzania limekufa? Akifa leo Mussa Assad ofisi ile ya ukaguzi ya taifa imekufa? Hapana. Sisi ni binadamu tunapita na hizi ni taasisi. Kwa hiyo Bunge halifanyi kazi na Mussa Assad – huo ni uamuzi seriously wala siyo utani hata kidogo.

“Tukikubali sisi Bunge la Tanzania kuwa ni mpira wa kuchezewa chezewa – kupigwa kona kule na kule tutakuwa tumewaangusha Watanzania kwa kiwango kikubwa sana. Kupitia kwenu napenda kuwataarifu Watanzania kuwa Bunge ni imara, tunaendelea kuchapa kazi.”

Akiwa nchini Marekani, CAG Assad alihojiwa na mtangazaji na kusema baadhi ya taarifa za ukaguzi ambazo hazifanyiwi kazi ni matokeo ya udhaifu wa Bunge.

Neno ‘dhaifu’ lilimuudhi Spika na akaamuru CAG ahojiwe katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Hata alipoitwa kwenye kamati hiyo, Profesa Assad hakufuta matumizi ya neno ‘dhaifu’ kwa kigezo kuwa neno hilo ni la kawaida katika lugha ya ukaguzi.

Kamati ya Bunge iliwasilisha taarifa yake bungeni na kukatolewa azimio la kutofanya kazi na ‘mtu’ Profesa Assad.