Moto wa ujangili wawaka Arusha

*DPP kupitia jalada la kesi aliyobambikiwa mwandishi

*Serikali yaingia kazini

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Baada ya Gazeti hili, JAMHURI, la uchunguzi kuchapisha kuhusu kuibua ujangili unaofanywa na mfanyabiashara mwenye asili ya Kiarabu, Saleh Salim Al Amry na baadaye kulalamika kuwa Mwandishi wake wa Arusha, Hiyasinti Mchau, amebambikiwa kesi ya rushwa, serikali imelivalia njuga, JAMHURI limebaini.

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, baada ya kupewa taarifa za mchezo huu mchafu uliofanywa na Ofisi ya TAKUKURU Arusha kwa kushirikiana na mtuhumiwa wa ujangili, Al Amry, amesema: “Nimeipokea taarifa, nitamwelekeza mwanasheria wa ofisi yangu Arusha alipitie jalada kuona kama lina ushahidi au vinginevyo.” 

JAMHURI linafahamu kuwa baada ya TAKUKURU Arusha kupata taarifa hizo wamesema watatumia kila mbinu kuonyesha kuwa wako sahihi. “Ufahamu hakuna ofisi yoyote inayoweza kukubali kuonekana inafanya kazi kwa kubambikia watu rushwa hata kama watu wake wamefanya kweli.

“Nafahamu wamesema watajenga ushahidi wa kina kuhakikisha Mchau anatiwa hatiani, ila bahati nzuri, ushahidi tayari upo. Kesi iko mahakamani, naomba tusiuzungumzie, wataishia kuumbuka. Songeni mbele JAMHURI mnafanya kazi nzuri sana, mnafanya kazi ya kizalendo. Mahakama itabaini mbivu na mbichi na kila mtu atalipa kutokana na matendo yake. Katika hili, hakuna atakayebaki salama,” amesema ofisa mwandamizi wa serikali.

Baada ya kufunguliwa kesi hii inayotiliwa shaka na kila mtu, JAMHURI liliwasilisha vielelezo vya mauaji ya wanyama majike, ndege, watoto wa Al Amry wakiwa wanachezea silaha za uwindaji kinyume cha sheria na mawasiliano kati ya Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, James Ruge na Gazeti la JAMHURI likimwomba ulinzi siku tatu kabla ya kwenda kumhoji Al Amry anayetuhumiwa kuua wanyama bila hofu wala vibali, lakini badala ya kushirikiana na gazeti kuokoa maliasili za nchi akalitelekeza.

“Naomba mtulie. Serikali iko serious kulinda maliasili za nchi hii. Suala hili sasa liko mikononi mwa mamlaka za uchunguzi. Baada ya kusoma habari yenu sisi tunachunguza mtandao wa ujangili si mtu mmoja. Wenye kufanya mchezo wanafahamu serikali isivyo na mchezo, serikali imeamua kulifanyia kazi kweli kweli. Hatutajali huyo Al Amry anatamba ana uhusiano na nani hapa nchini, tutahakikisha haki inatendeka kwa kila awaye.

“Tayari tunazo taarifa nzuri za awali, ikibainika mtu wenu ameomba rushwa kweli, mtatusamehe, itabidi awajibike kwa matendo yake. Ikibainika amebambikiwa rushwa, mkondo wote uliohusika tutausafisha. Wajulishe tu, kuwa serikali iko kazini saa 24, imelivalia njuga hili na kila mtu ataona matokeo si muda mrefu. Naomba niishie hapo,” amesema mmoja wa maofisa wanaolishughulikia suala hili.

Wiki iliyopita gazeti hili lilichapisha habari inayosomeka hivi:

Katika hali ya kusikitisha, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, James Ruge, ametumia dhamana aliyopewa na taifa kushiriki kukandamiza haki za wanyonge, JAMHURI limebaini.

Tukio hilo limetokea Desemba 26, mwaka jana wakati JAMHURI likifuatilia sakata la ujangili unaodaiwa kufanywa na mfanyabiashara wa uwindaji wa kitalii mwenye asili ya Kiarabu, Saleh Salim Al Amry, mkazi wa Arusha.

Al Amry anadaiwa kuwaingiza nchini watalii wa uwindaji kutoka Saudi Arabia mwaka 2019, ambao pamoja naye, waliwinda na kuua wanyama na ndege ambao hawamo kwenye orodha ya ‘wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa’ kisheria, huku wakipiga picha zaidi ya 100.

Wakati wa kufuatilia taarifa hizo, JAMHURI lilimtafuta Al Amry kwa njia ya simu kwa wiki kadhaa kupata kauli yake juu ya tuhuma zinazomkabili bila mafanikio, ila kwa alichokijua moyoni mwake akaomba mwandishi wa JAMHURI akutane naye ofisini kwake Arusha, badala ya kutoa majibu kwenye simu.

Ijumaa ya Desemba 24, 2021 Al Amry alipopokea simu kwa mara ya kwanza na kuzungumza na mwandishi wa JAMHURI jijini Arusha, Hyasinti Mchau, aliomba kabla ya kujibu maswali atumiwe picha hizo.

Maswali ya JAMHURI kwa Al Amry yalikuwa kwanza kutaka kufahamu iwapo anazitambua picha tulizonazo. Pili, kama wakati wa uwindaji huo walikuwa na leseni za kuua nyati na simba. Tatu, kufahamu ni mwindaji mahiri yupi (Professional Hunter – PH) aliyekuwa naye wakati wa uwindaji. Swali la mwisho lilikuwa ni ukweli kuhusu kuhojiwa kwake kwa kukutwa na kiwango kikubwa cha madini ya tanzanite na dhahabu.

Dakika chache baadaye Al Amry alitumiwa picha, na Mchau anasema: “Alipopokea picha akanipigia simu akitaka tukutane ofisini kwake Jumapili asubuhi (Desemba 26).”

Baada ya hapo Mchau akapiga simu ofisi za JAMHURI, Dar es Salaam kuomba uchapaji wa habari kuhusu ujangili unaodaiwa kufanywa na Al Amry kusubiri hadi watakapokutana kupata maelezo ya upande wake na kupata majibu kama sehemu ya haki ya asili ya mtu anayetuhumiwa kwa lolote, JAMHURI kitaaluma lilisitisha kwa muda habari hiyo.

Kwa kutambua unyeti wa mkutano kati ya Mchau na Al Amry pamoja na mustakabali wa masuala ya ujangili nchini, JAMHURI likaona ni vema taasisi nyeti za serikali zikashirikishwa. Hii ilikuwa ni baada ya kupata taarifa za ujahili wa Al Amry kuwa anatumia baadhi ya watu ndani ya vyombo vya dola kubambikia wananchi kesi.

JAMHURI liliamua kuwashirikisha TAKUKURU Mkoa wa Arusha inayoongozwa na Kamanda Ruge kwa kuwasiliana naye. Katika kuweka kumbukumbu, JAMHURI liliamua kutumia WhatsApp, Ruge akatumiwa ujumbe unaosomeka hivi:

“Salamu Kamanda. Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… Taarifa;

Kuna Mwarabu anajulikana kwa jina la Saleh Salim Al Amry. Background ya huyu mtu ni mwanajeshi aliyepigana vita ya pili ya Saddam Hussein upande wa United Arab Emirates (UAE) akitokea jeshi la Yemen.

“Huyu mtu amehamia Tanzania na anaishi Arusha. Amekuwa mwiba kwa serikali na nchi, akihujumu uchumi kwa njia ya ujangili akiwa amewaweka viongozi wengi kwenye ‘payroll’ yake.

“Huyu mtu ameua wanyama wengi sana ambao hawaruhusiwi kuwindwa. Tumekuwa tukitoa taarifa zake kwa kuandika, lakini haguswi!

“Tunazo taarifa za ujangili alioufanya za kuua wanyama na ndege aina ya ‘kori bustard’, majike ya swala, simba wadogo, nyati na nyumbu Desemba 2019. Nakutumia picha.

“Gazeti la JAMHURI limemhoji kuhusu hizo picha. Amemwita mwandishi [wetu] ofisini kwake Jumamosi saa tatu asubuhi [baadaye ikasogezwa mbele hadi Jumapili saa tatu asubuhi].

“Angalizo tu, ndiyo maana ninakupa taarifa asije kumfanyia mchezo mchafu, kumbambika rushwa kwa nguvu kwa kupitia TAKUKURU. Tuna taarifa huyu Mwarabu anawatafuta maofisa kutoka ofisini kwako ili mwandishi atakapofika wampachikie kesi kinguvu.

“Nimekupa taarifa tu ‘in advance’ lakini huyu mwandishi ni lazima aende siku hiyo kwa kuwa Jumanne lazima tuiambie serikali mali za nchi zinavyomalizwa.”

Ruge akajibu kwa kifupi: “Nikushukuru sana ndugu yangu kwa taarifa hii.”

Ruge abadilika ghafla

Mkutano kati ya Al Amry na Mchau ulimalizika kwa muda mfupi baada ya maofisa wa TAKUKURU kuingia ofisini kwa Al Amry na kumkamata Mchau kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa (kesi ipo mahakamani).

Baada ya tukio hilo ambalo JAMHURI liliitarajia na siku mbili kabla kumpa taarifa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Ruge, Mchau akapelekwa ofisini na kuhojiwa kwa muda mrefu.

Ruge alipotafutwa na Mhariri wa JAMHURI kuomba aingilie kati suala hilo kwani analifahamu, alijulishwa mapema, mazungumzo yalikuwa hivi:

Ruge: Mimi niko Namanga, nje ya ofisi kikazi. Kwa kawaida sisi tukitoka nje ya ofisi tunakaimisha kila kitu. Kwa hiyo wasiliana na ofisi watakusaidia.

Mhariri: Nimewasiliana nao na wanasema wanasubiri kauli yako tu, wamuachie kwa dhamana hadi kesho.

Ruge: Ni nani anasema hivyo?

Mhariri: Ofisa mmoja anaitwa Rama (aliyeshiriki kumkamata Mchau).

Ruge: Nimekwambia kwa utaratibu wetu (TAKUKURU) nikiwa nje ya ofisi siwezi kutoa maelekezo hayo. Wapo maofisa pale ofisini wanaoweza kukusaidia.

Mhariri: Mimi nadhani hutaki tu kutusaidia. Umeamua kututesa. Lakini tulifahamu tangu awali kwamba mwandishi angeshikishwa rushwa!

Ruge: Kama ulifahamu ni hatua gani ulichukua kuzuia kitendo hicho kisitokee?

Mhariri: Hatua niliyochukua ni kukutaarifu wewe! Sasa ni nani mwenye dhamana ya kuzuia na kupambana na rushwa zaidi yako? Tulikutaarifu lakini sasa umeamua kututesa. Ninaamini kuna sehemu haki haijatendeka. 

Ruge: Hebu tusubiri hadi kesho.

Hata hivyo, wakati Ruge akidai kuwa Namanga, JAMHURI linafahamu kuwa ni yeye ndiye aliyeelekeza kukamatwa kwa Mchau bila kujali ‘tahadhari’ aliyopewa na JAMHURI awali.

JAMHURI linafahamu pia kwamba wakati maofisa wa TAKUKURU waliokuwa na Mchau kwenye gari dogo wakifuatana na Al Amry aliyekuwa na gari namba T 438 DSS aina ya Arphard wakiwasili ofisi za TAKUKURU, Ruge alikuwapo!

“Wakati mahojiano yakiendelea Ruge alikuwapo. Nilimuona,” anasema Mchau.

Akizungumzia kitendo alichokifanya Ruge, mwanasheria mkazi wa Morogoro na wakili wa kujitegemea, Everist Mnyele, anasema:

“Ni kitendo kibaya kabisa kufanywa na ofisa aliyepewa dhamana na mamlaka ya kuzuia rushwa. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka (ofisi). Kwa nini amkamate mtoa taarifa? 

“Makosa ya matumizi mabaya ya madaraka ni mabaya kwa kuwa yanawaumiza wanyonge na ndiyo maana huwa hayamo kwenye msamaha wa Rais. Sasa ninyi waandishi mnapo pa kusemea, mtu wa kawaida atafanya nini kama aliyepaswa kumlinda amemgeuka?”

Mwindaji Mahiri (PH) anayemfahamu vizuri Al Amry ameliambia JAMHURI kuwa ilikuwa ni hatari sana mwandishi kwenda ofisini kwake.

“Huyu jamaa ni ‘mafia’. Ningefahamu mapema ningemkataza Mchau asiende. Ni hatari sana. Halafu fedha zake huwa kama zina mashetani. Akimpa mtu anakuwa kama zezeta. Anafanya chochote bila hata kutumia busara ya kawaida,” anasema PH huyo ambaye ni mtu wa karibu na Al Amry.

JAMHURI limemtafuta Kamanda wa TAKUKURU, Kamishna Salum Hamduni, likamtumia picha za wanyama na ndege waliouawa na majibu ya Ruge, yeye akasema: “Nipo likizo mtafute Naibu Kamanda.”

Kamishna Hamduni alimtumia Mhariri wa JAMHURI namba ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Neema Mpembe Mwakalyelye, aliyemwachia ofisi. Kamishna Hamduni alimtumia namba ya simu ya Naibu Mkurugenzi Neema, Mhariri wa JAMHURI.

Mhariri wa JAMHURI alipompigia simu Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU Neema, alipokea simu akamsikiliza huku akisikika kujibu watu wengine, baadaye bila hata kulipa uzito suala aliloelezwa akasema: “Hiyo ni jinai, hatuwezi kufuta kesi, acha kesi iendelee na ushahidi utamtoa ikiwa hana hatia.”

Alitoa majibu hayo baada ya awali kumuuliza Mhariri: “Wewe ulikuwapo?” Mhariri alimweleza kuwa mbali na Mchau aliyebambikiwa kesi, alikuwapo mtu wa pili aliyeshuhudia unyama huo. Akasema yeye hawezi kuingilia suala ambalo ni jinai.

Baada ya majibu hayo, Mhariri wa JAMHURI alimwambia Neema: “Naibu Mkurugenzi, kwanza naomba ufahamu kuwa mbali na uandishi mimi ni Mwanasheria. Unafahamu kwa nini sheria iliweka mkondo wa Administrative Law? Hivi kweli mwandishi wetu amebambikiwa kesi, unataka ahangaike mahakamani miaka mitatu hadi mitano, kisha ithibitike kuwa hakuwa na kosa?

“Lakini pia, ndiyo maana ninyi viongozi mpo. Hivi kweli nakueleza kuwa watu wenu Arusha wametenda kinyume cha maadili na sheria za kazi, bila kunisikiliza unanipa majibu mepesi tu, na kutetea watu walioko ofisini wanafanya uhalifu wakati ninyi TAKUKURU mnapaswa kuchunguza kila taarifa mnayopewa kwa mujibu wa sheria?”

Baada ya kumwambia hivyo, sauti yake ikabadilika kidogo akawa mpole, ila akasema: “Basi fuata utaratibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya hao maofisa nasi tutafuatilia kama yatakuwa na mashiko.” Baada ya hapo, Mhariri alikata simu kwa masikitiko juu ya usikivu wa ofisi hii ya umma.

Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinasema, Al Amry yupo anatamba kuwa yeye ameiweka mfukoni serikali na anaweza kuingia ofisi yoyote akafanya lolote bila kuchukuliwa hatua yoyote hapa nchini. Mmoja wa watu waliokuwa wamekaa naye juzi, alisema: “Mimi nakwambia hata huyo Ruge nikitaka kumwondoa hapa Arusha namwondoa. Acha kumwondoa, hata nikitaka kumfunga namfunga, sembuse hawa waandishi wa magazeti. Watapiga kelele sana na hakuna kitakachobadilika zaidi ya wao kuumia,” amekaririwa akisema.

JAMHURI linaendelea kufuatilia katika vyombo vya dola na watendaji wa serikali kushuhudia mwisho wa upatikanaji wa haki Tanzania na ulinzi wa rasilimali za umma iwapo wanalindwa wenye mali au watetezi wa haki.

Pamoja na habari hizi, zinaambatanishwa picha mbalimbali za wanyama na ndege alioua, huku akiwatesa wanaojaribu kuanika habari zake.