*Asema aliwahi kuitosa TLP dakika za mwisho na kuhamia NCCR-Mageuzi

*Mwanzo ilikuwa ahamie Chadema, Mtei akamkatalia akijua…

*Adai ana mipango ya Serikali

* Aamua kurudi CCM kujisalimisha

Upinzani nchini una changamoto ya kupata makada wa kweli, kwani hata wale waasisi wa vyama kadhaa ama wamehamia vyama vingine, au kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mfano halisi ni Leo Lwekamwa, mwasisi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP). Ni Mwenyekiti wa Kwanza wa chama hicho cha upinzani  kilichojizolea umaarufu mkubwa wakati wa Uchaguzi wa Pili wa mfumo wa vyama vingi nchini uliofanyika mwaka 2000. Mwanasiasa huyo, mtaalamu wa magonjwa ya mifugo, alifanya mahojiano na Mwandishi wa gazeti hili, ALFRED LUCAS, Alhamisi iliyopita jijini Dar es Salaam, ambako pamoja na mambo mengine amezungumzia siasa za Mwenyekiti wa sasa wa TLP, Augustine Mrema, na sababu za yeye kurudi CCM. Fuatilia…

Swali: Wewe ni mwasisi wa Chama cha Tanzania Labor (TLP), mlianzishaje chama hicho?

Jibu: TLP ilitokea mapema mwaka 1991 kutokana na mwelekeo wa dunia, ambako mageuzi yalikuwa yameshika kasi Tanzania. Mimi na wenzangu wakati tunaingia kwenye mageuzi tuliwaza sana. Tuliwaza juu ya kumkomboa kiuchumi Mtanzania hasa mfanyakazi kwa sababu Wafanyakazi ndiyo hasa walioikomboa nchi hii kutoka kwenye mikono ya utawala wa wakoloni. Basi sisi tulianzisha chama hicho na sera yetu kuu ilikuwa ni kumkomboa mfanyakazi kiuchumi. Tuliamini kwamba ukimkomboa kiuchumi mfanyakazi, maana yake umekomboa uchumi wa nchi.

Sisi TLP tuliamini kwamba mkulima, mvuvi, mfugaji au mtu wa kuchimba madini wote ni wafanyakazi kwa kuwa wanatoka jasho ili kupata riziki. Hata mfanyakazi wa ofisini anatumia akili ambako anatoka jasho. Kwa jinsi wanavyovuja jasho hatukutaka kuwagawa, bali tuliona wote ni wafanyakazi ambao wanastahili kukombolewa kiuchumi. Ndiyo maana tuliona lazima wawe na chama chao na ndiyo hasa msingi wa kuanzisha TLP.

Swali: Mlikuwa waanzilishi wangapi? Wataje wenzako unaowakumbuka kwa sasa?

Jibu: Tulikuwa wachache kwa sababu mambo haya yanaanza na wachache. Na kwa kuwakumbuka tu ni kwamba tulikuwa na Prosper Rwegoshora, Julius Miselya, Peter Golugwa, Boniface Mgeta. Kwa uchache ni hao.

Swali: Nadhani leo unaweza ukatoa siri kwamba vikao vyenu mlikuwa mnafanyia wapi?

Jibu: Tulikuwa tunakutana ofisini kwangu. Mimi nilikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Dawa za Mifugo kutoka Ujerumani. Kampuni ilikuwa inafahamika kwa jina la Hoechst AG-West German Pharmaceutical Giant. Nilikuwa Meneja Masoko wa kampuni hiyo, hivyo tulikuwa tunakutana ofisini hapo bila wakurugenzi wangu kujua. Mambo yote yalifanyika hapo, mpaka chama kilipopata usajili wa awali au wa muda.

Swali: Kwanini hamkuwa na wale wanamageuzi wengine waliofahamika kwa jina la National Conversion, walioungana na Kamahuru ya Zanzibar?

Jibu: Aaah! kule tuliona hakuna kitu, sisi tulijiona kwamba tumejitosheleza na tunamudu vema na sera yetu ya wafanyakazi kuliko wao. Hivyo, tukawaacha nasi kubaki tukipambana peke yetu mpaka tukapata usajili wa kudumu.

Swali: Inaonekana mlifeli, ilikuwaje mkamchukua Augustine Mrema?

Jibu: Sasa katika hilo hilo la kufeli, actually haikuwa kufeli, ila tulikosa umaarufu na kuwa tulikuwa na wanachama wachache. Hali hii ilisababisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji George Liundi,  kuanza kutunyanyasa. Alikuwa akituandikia barua za vitisho eti hatukuwa na viongozi wa mtaa, madiwani, wabunge mara baada ya uchaguzi wa mwaka 1995. Hivyo akatuona kama kijiwe na akataka kufuta chama.

Sasa leo nitatoa siri. Kumbuka wakati ule tunasajiliwa Agustine Mrema alikuwa CCM ambako alikuwa Naibu Waziri Mkuu na waziri wa wizara mbalimbali. Akiwa huko, akawa na mvuto wa aina yake kwa kuwa alijitengeneza kama mtetezi wa wanyonge na walalahoi. Alionekana wazi kuwa ni mpenzi wa watu kwa kujali shida zao. Sasa mle ndani ya CCM kulikuwa na mnyukano wa ndani kwa ndani kuhusu kambi ya kuwania madaraka. Mrema mwisho wa siku aliona wazi kuwa asingeteuliwa. Akaamua kujitoa huko. Na alipojitoa alifuatwa na vyama vyote vya upinzani kipindi kile. Yeye aliweka masharti ya kupewa uenyekiti wa karibu vyama vyote vya upinzani ili aunganishe nguvu kabla ya uchaguzi wa mwaka 1995.

Ukweli ni kwamba Mrema alipenda zaidi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Sababu kuu ni chama cha kwao. Ndugu mwandishi, kwenye hizi taasisi hata za kisiasa kuna ukabila. Basi tukiwa wote pale, mzee Edwin Mtei wakati ule alikuwa Mwenyekiti wa Chadema alikataa kumwachia kiti Mrema. Ndani ya kikao cha viongozi wa vyama vya upinzani, Mtei alimjibu Mrema akisema, “Wewe Mrema labda tukupeleke ukawe mwenyekiti wa kata au kijiji, lakini si kuwa mwenyekiti wa Chadema. Ukitoka huko, ndiyo uje ngazi moja baada ya nyingine mpaka taifani.”

Kuona hivyo, ni mimi pekee niliyejitolea kujiuzulu nafasi yangu na kumpa Mrema uenyekiti. Mrema akakubali na sisi tukaanza kubadilisha nyaraka za uongozi kwa Msajili Liundi, ambaye, hata hivyo, hakupenda mabadiliko hayo akidai demokrasia imekiukwa. Akataka kufuta chama akisema TLP imejifuta. Kumbe wakati sisi tunafanya hivyo, NCCR-Mageuzi wao wakawa wanamshawishi Mrema chini kwa chini ili ajiunge nao. Mrema akakubali na akataka kutangaza uamuzi huo akiwa nyumbani kwao Moshi. Baada ya kubadili makaratasi yetu pale kwa Msajili, tukafunga safari kumfuata Mrema ambaye wakati huo alikuwa ametangulia Moshi mkoani Kilimanjaro. Lakini tukiwa Moshi tukaona tu pale viwanja vya Sokoni kumepambwa bendera za NCCR-Mageuzi. Tukashangaa.

Sisi hatukuchangamkiwa wala kupokewa. Lakini tukamwona Sultan Sultan. Mara tukaona msururu mkubwa ukitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambako Mrema amekwenda kupokewa. Sijawahi kuona umati wa watu kiasi kile maana wamejaa barabara nzima. Awali, tulipigwa na butwaa baada ya Mrema kutuchezea akili, tukasema wacha tuwasapoti kwa sababu Mrema tayari ameingia upinzani…siyo mbaya. Tutaungana naye huku huku. Basi tukaishia kumsindikiza hadi Kiraracha alikotangaza kuhamia NCCR-Mageuzi na sisi kurudi Dar kubadili tena nyaraka zetu na kuendelea na chama. Mrema alitutosa na kuhamia NCCR-Mageuzi kwa mipango ya Serikali.

NCCR-mageuzi ikawa na nguvu — akina James Mbatia, Anthony Komu, Masumbuko Lamwai, akina Dk. Ringo Tenga, Dk. Sengondo Mvungi — utaona kuwa hata kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 1995  Mrema alitikisa na kura za Dar es Salaam zilifutwa na Benjamin Mkapa kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais. Kura za Dar zilifutwa kwa sababu gani? Sitaki kujibu leo. Kwanini wapinzani hawakulalamika? Tutazungumz siku nyingine. Lakini kwa kuwa Mrema akawa na kazi yake, pale wakaanza kukatika na kwenye mkutano wao mkuu pale Bwawani Hoteli wakatangaza kumtimua kwa kosa la kutowajibika.

Kwa kuwa Liundi alikuwa anaendelea kutusumbua, mwaka 1999 tukampokea Mrema na kumpa uenyekiti maana hata mwanzo tulikubaliana hivyo. Ajabu ni kwamba safari hii Liundi alikubali haraka. Wakati huo Mrema alikuwa ameisha mvuto, lakini tukasema hapana. Hajaisha sana na tunaweza kumtumia kupata madiwani na wabunge ili Msajili Liundi asiendelee kutusumbua. Nikajiuzulu na kumwachia Mrema uenyekiti.

Swali: Ilikuwaje mkasigana?

Jibu: Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 tukapata wabunge 16 na madiwani na ninakumbuka tulipata mpaka kuongoza Halmashauri ya Moshi. Sasa baada ya uchaguzi kuisha ndipo hasa tulipoanza kujua sura halisi ya Mrema kwenye ruzuku. Akaona mafanikio yake ni kama mtaji wake pekee na wale wanachama wa NCCR-Mageuzi wakawa ndiyo wajumbe wa Mkutano Mkuu kiasi kwamba sisi wengine waasisi hatukuonekana. Yeye alibeba wale wanachama wa NCCR-Mrema na kuwaacha NCCR-Marando. Msajili hakutoa msaada na hata mahakamani tukashindwa kwa maana Mrema ni mtoto wa ndani wa Serikali.

Swali: Mbona baadaye ukamkimbia kurudi CCM?

Jibu: Kwanza, sasa baada ya kushindwa huko kote, nikajiona siko ndani ya chama cha siasa. Nikasema bora nirudi CCM wanione, kwamba nashinda nao, nakula nao tofauti na hapo unaweza kuangamizwa kwa kuitwa mchochezi. Nipo CCM kulinda usalama wangu na usalama wao, ila mimi ni mpinzani ndani ya CCM na mimi sasa ni Ukawa ndani ya CCM. Pili, niliamini Rais Jakaya Kikwete huenda akaleta mageuzi, nilimpigia kampeni za nguvu kwa kujitolea tu, sikulipwa lakini mwisho wa siku namuona Rais Kikwete kama Mikhail Gorbachev (Rais wa zamani wa Urusi) tu ndani ya CCM. Si mtu ambaye unaweza kumhusisha na uchafu wa aina yoyote ile kama ufisadi unaotendwa na wengine.

Hapendi ufisadi na ndiyo maana aliwaambia watu wajivue magamba. Rais Kikwete ndiye huyo aliyezuia wizi wa nyumba za Serikali na kurudisha kiasi kikubwa cha fedha kutoka nje zikiwamo zile za EPA. Hawezi kufanya miujiza, kwa kuwa amezingirwa na hali nzima inayoonekana. (hakufafanua). Ndiyo maana hawezi kutimiza maisha bora kwa kila Mtanzania.

Swali: Kwa sasa umekuwa kimya muda mrefu, sababu ni nini na je, kwenye siasa hizi utagombea?

Jibu: Nimekaa kimya kuheshimu system (Serikali). Wa kusema ndani ya chama na Serikali wanajulikana. Mimi ni miongoni mwa watu tuliofundishwa maadili enzi za Umoja wa Vijana wa TANU yaani TANU Youth League. Kwa upande wangu sitegemei kugombea mwakani kwa sababu ya rushwa kwenye chaguzi zetu. CCM wameikubali rushwa kwani ni vigumu kuongoza bila kutoa fedha. Rushwa imekuwa kama dini au utamaduni kwenye chaguzi zetu hizi. Huna hela, huna uongozi na kwangu hilo naliona ni dhambi, kwa hiyo siwezi kufanya wala kushiriki dhambi.

Swali: CCM kuna minyukano hasa kwa wanaosaka kuongoza dola, nini mtazamo wako?

Jibu: Hao si viongozi. Mie naona wanatafuta ajira tu.

Swali: Toa maoni yako kuhusu Uchaguzi Mkuu mwakani?

Jibu: Mtu anayefaa kuongoza Tanzania ni yule ambaye hawezi kuwaonea haya wazembe. Vijana wengi Tanzania hawafanyi kazi. Mtu anayefaa kuongoza nchi lazima asimamie sheria.

Swali: Nini maoni yako kwa siasa za Tanzania?

Jibu: Siasa za Tanzania zimeirudisha nyuma nchi kwa miaka 50, katika maeneo ya kiuchumi.

Swali: Nini maoni yako kwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum?

Jibu: Katiba ina lugha za ulaghai, imekataa kuelekeza nani afanywe nini kama atavunja sheria za nchi na haitamki wazi uelekeo wa uchumi wetu. Katiba ya mwaka 1977 aliketi Sheikh Thabit Kombo na Katibu Mkuu wa TANU, Pius Msekwa. Hii ya sasa imetokana na wananchi, hivyo Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi chini ya mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, ndiyo iliyopaswa kujadiliwa na si kuondoa maoni ya wananchi.

By Jamhuri