MTANZANIA KUTUNUKIWA SHAHADA YA HESHIMA MAREKANI

 

MMOJA wa wataalam na watafiti wa magonjwa ya akili nchini, Profesa Slyvia Kaaya, ni miongoni mwa watu sita watakaotunukiwa shahada za heshima na Chuo Kikuu cha Dartmouth cha Marekani leo.

 

Prof. Kaaya, wa Chuo cha Sayansi ya Afya cha Muhimili (Muhas) ni mmoja wa wataalam 60 wa magonjwa ya akili nchini anayejishughulisha katika kuendeleza taratibu ambazo zitatumika kunufaisha nchi zenye raslimali ndogo.

 

Ripoti ya chuo kikongwe zaidi Marekani, The Dartmouth, ilisema Prof Kaaya aliungana na Dartmouth kupitia ushirikiano wa DarDar ulioanzishwa mwaka 2001 ili kukiunganisha Chuo cha Geisel na Muhimbili ili kutatua masuala ya afya.

 

Chuo cha Dartmouth kinategemewa kutoa shahada sita katika sherehe itakayofanyika leo, Juni 10. Kila mhusika atakatunukiwa shahada ya Doctor of Humane Letters. Utaalam wa watakaotunukiwa unajumuisha tasnia mbalimbali kuanzia huduma za burudani hadi za dawa.

 

Miongoni mwa watakaotunukiwa ni mdhamini wa Dartmouth na mshirika mstaafu wa taasisi ya Goldman Sachs, Peter Fahey; mjumbe wa baraza la Congress wa zamani na mwakilishi katika Umoja wa Mataifa, Frank Guarini; tibabu na mpasuaji William Holmes; mwigizaji, prodyuza na mwandishi Mindy Kaling na mwasisi-mwenza na mwenyekiti-mwenza wa Carlyle Group, David Rubenstein. Kaling pia atatoa hotuba ya ufunguzi katika hafla hiyo.