Wakati Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro ikitoa ratiba ya mpangokazi wa Kamati Shirikishi ya Mapendekezo ya Kumaliza Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro, mkakati mpya wa kukwamisha mpango huo umebainika.

Mpango huo, uliotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo Januari 6, mwaka huu, unalenga kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ili kumaliza mgogoro wa Loliondo uliodumu kwa miongo kadhaa.

Kumekuwapo sintofahamu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuonekana kuunda kamati tofauti na maelekezo ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Injinia Ramo Makani.

NGOs ambazo zimetuhumiwa na Waziri Mkuu kwa kuchochea vurugu, hadi akaagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akague matumizi ya mabilioni ya shilingi kutoka kwa wafadhili, viongozi wake kwa sasa ndiyo washauri wakuu wa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa katika mgogoro wa Loliondo.

Wameruhusu NGOs hizo zipite huku na kule vijijini kuwahamasisha wananchi ili wapinge mpango wa Serikali wa kutenga eneo la uhifadhi ili kuilinda Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA). Majina ya NGOs na watu wanaopita vijijini kushawishi wananchi kupinga mpango wa Serikali, tunayahifadhi kwa sasa.

Taarifa hiyo inaonesha kuwa kutoka Mkoa wa Arusha, wajumbe kwenye Kamati iliyosukwa kwa maelekezo ya Gambo ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala Mkoa, Afisa Utalii Mkoa, Mwanasheria, Afisa Ardhi na Afisa Mwandamizi LGA.

Wajumbe kutoka taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni wawakilishi wawili kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, na wawakilishi wawili kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kutoka Wilaya ya Ngorongoro ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Katibu Tawala Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Ngorongoro, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mwenyekiti Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira; Afisa Ardhi na Afisa Utalii Wilaya.

Pia kutakuwamo wajumbe 16 wa jamii, mwakilishi wa dini ya Kiislamu, mwakilishi wa dini ya Kikristo; na kwa upande wa wawekezaji kutakuwa na mwakilishi mmoja mmoja kutoka kampuni za OBC, AndBeyond, Thomson Safaris Ltd na Buffalo Luxury Camp.

Sekretarieti inaundwa na watu watano ambao kati yao, watatu ni wale walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, na kuwamo kwenye taarifa aliyosomewa Waziri Mkuu ikidaiwa kuwa ni ya ‘wananchi.’

Chanzo cha habari kimeiambia JAMHURI kuwa wajumbe wawili wanatoka kundi linaloitwa la jamii ambalo kimsingi ni la wamiliki wa NGOs.

Wakati Gambo akitarajiwa kufika Loliondo Januari 16, kumekuwapo taarifa zisizotiliwa shaka kuwa baadhi ya wamiliki wa NGOs wameshaanza kupita vijijini kuwaandaa wananchi kupinga mpango wowote wa kulitenga eneo la Loliondo.

Baadhi ya wajumbe kwenye kutoka NGOs hizo wanadaiwa kutumia nguvu za fedha kuwaandaa wananchi ili pindi kamati itakapopita katika maeneo yao, waoneshe msimamo wa kutounga mpango huo.

“Wananchi wameandaliwa waseme wanataka WMA (Hifadhi ya Jamii), utakumbuka hata siku ile kijijini Ololosokwan Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha (Maiko Laizer), alieleza msimamo wa kuifanya Loliondo kuwa WMA.

“Mpango wote huu nyuma yake kuna Mkuu wa Mkoa ndiyo maana tunasema ni vigumu sana hili jambo kufanikiwa kwa sababu yeye na wenzake katika wilaya wameshaungana na NGOs,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kinasema msimamo wa Gambo na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume, ni kuhakikisha NGOs zinaendelea kuwapo.

“Huo ndiyo ukweli. NGOs zinafanya kila linalowezekana ili zibaki, maana zinajua kutulia kwa Loliondo ni kupoteza mapato makubwa zinazopata sasa. Kinachotia shaka zaidi ni kuona Gambo na Mfaume ndiyo walioamua kuwa watetezi wa mashirika hayo,” kimesema chanzo chetu.

Wakati hayo yakiendelea, kuna taarifa kuwa CCM Mkoa wa Arusha imekusudia kufanya mikutano mahsusi katika Wilaya ya Ngorongoro, hasa tarafa za Sale na Loliondo yenye sura ya kukiimarisha ikiwa ni pamoja na kuwapokea wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani. Hata hivyo, nyuma ya mpango huo, lengo ni kuendesha propaganda za kukwamisha mpango wa muda mrefu wa Serikali wa kuligawa eneo la Loliondo.

Mmoja wa wanaokusudiwa kurejea CCM anatajwa kuwa ni Diwani wa Viti Maalumu, Maanda Ngoitiko (Chadema), ambaye ni kiongozi wa Pastoral Women Council (PWC). Kwa sasa hati yake ya kusafiria imezuiwa na mamlaka za nchi.

“Anaamini akirejea CCM anaweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kurejeshewa hati yake ya kusafiria. Yuko radhi arejee ili kutoa picha kuwa si mpinzani, na kwa hiyo iwe rahisi kupewa hati ya kusafiria,” kimesema chanzo chetu.

Maanda, kama alivyo Tina Timan; wanatajwa kuwa na asili ya Kenya wakitajwa kuwa miongoni mwa vinara wa migogoro katika Loliondo.

NGOs zinatajwa kupata nguvu kutoka kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, William Nasha, ambaye kwa miaka yote amekuwa mtumishi katika mashirika hayo.

“Kilichopo hapa ni watumishi wa Serikali walioungana kuipinga Serikali, NGOs zimepata fedha nyingi kutoka…(Shirika moja la Ulaya) kwa ajili ya kusaidia kueneza chuki ili Loliondo isitulie,” kimesema chanzo chetu.

 

Kinachoendelea Loliondo

Baada ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa ‘kuahirisha’ uamuzi wa kutangaza kilomita za mraba 1,500 za Pori Tengefu la Loliondo, kwa upande wa mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) ni ushindi mkubwa.

NGOs na wafuasi wake wamechukulia jambo la kushindwa kutangazwa uamuzi huo kama ushindi dhidi ya Serikali. Baada ya Waziri Mkuu kuhitimisha ziara wilayani Ngorongoro na kuacha maagizo kwa wadau wote kurudi kwenye meza ya mazungumzo kusaka maridhiano, wakazi wa Loliondo walifurahia ushindi kwa mara ya pili. Wanaamini kulisha ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, kulima maeneo ya Karkarmoru na kandokando ya Mto Pololeti, sasa rukrsa!

Jijini Arusha na Loliondo, NGOs zimemwaga mamilioni ya shilingi kutekeleza mikakati ya kupinga kutangazwa Pori Tengefu la Loliondo.

Injinia Makani alifika Loliondo na kuweka utaratibu wa kutekelezwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu, lakini hali ilivyo sasa ni kwamba Mkuu wa Mkoa, Gambo, ana mpango wake mwenyewe. Kigezo anachokitumia ni cha kwamba yeye ndiye mwasisi wa wazo la maridhiano, na Waziri Mkuu alimpa ‘nguvu’ za kusaka suluhu.

Maandalizi ya mpangokazi, uwakilishi wa kamati shirikishi na bajeti vimefanywa jijini Arusha na kamati ndogo ya siri, tofauti na maelekezo ya Makani.

Kamati ndogo ya siri imeundwa na NGOs za PWC, NGONET, PALISEP, PINGOs FORUM, TNRF, TPCF, UCRT, Trias, Ndorobo Safaris, AndBeyond, CORDS na wataalamu washauri chini ya uratibu wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya na mkoa; na viongozi wa Serikali katika ngazi ya Wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha.

Kamati hii inawahusisha Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Gambo, na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ngorongoro, Rashid Mfaume; Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ngorongoro, William Nasha; Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Raphael Siumbu; Mwenyekiti wa Halmashauri, Matthew Siloma; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ibrahimu Sakai; na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer.

Kamati hii ndogo ya siri imetayarisha mpango kazi, bajeti na uwakilishi wa kamati shirikishi itakayoshiriki kutoa mapendekezo ya ‘kumaliza’ mgogoro wa ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo. 

Yamekuwapo maandalizi ya kutengeneza mfumo mpya wa Hifadhi ya Jamii (WMA) au kutenga ukanda wa malisho ya mifugo (reserved grazing land) ndani ya Pori Tengefu Loliondo, tofauti na msimamo wa siku zote wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mashirika yale yale ya PWC, NGONET, PALISEP, PINGOS FORUM, Trias, CORDS, TNRF, UCRT, TPCF, AndBeyond, Ndorobo Safaris na wataalamu washauri chini ya uratibu wa viongozi waliotajwa hapo juu wakiwa jijini Arusha, walifanya jambo jingine kubwa la pili baada ya kupata baraka za wakubwa za kuandaa mfumo mbadala wa WMA au kuanzisha eneo la ukanda wa malisho, wakilenga kufuta Pori Tengefu Loliondo.

Kamati ndogo ya siri iliyokutana ina wajumbe wawakilishi kutoka NGOs za Pastoral Women’s Council (PWC) chini ya uongozi wa Maanda Ngoitiko, ambaye ni Diwani wa Viti Maalum (Chadema), Mtandao wa NGOs Wilaya ya Ngorongoro (NGONET) chini ya uongozi wa Samwel Nang’iria; PALISEP chini ya uongozi wa Robert Kamakia na IRK-RAMAT chini ya uongozi wa Yaniki Idoinyo ambaye ni Diwani wa Ololosokwan (CCM) wakishirikiana na Andbeyond, PINGOs Forum (ya Edward Porokwa); CORDS (Benedikti Nangoro); Ndorobo Safaris (David Peterson); na Tanzania Natural Resource Forum (TNRF) ya Alais-Morindat.

NGOs hizi wakishirikiana na kushauriana na maswaiba wao yaani Nasha, Gambo, Mfaume, Laizer, Sakai, Matthew Timan (mshauri wa NGOs Loliondo) na Tina Timan (mwanaharakati wa PWC), wanafanya mchakato huu wa kutafuta mapendekezo ya kumaliza mgogoro katika Loliondo uwe wa upendeleo, upotoshaji na usiwe shirikishi.

Wanawapendelea baadhi ya wawekezaji wa AndBeyond, Ndorobo Safaris na kutowajali wawekezaji kama Thomson Safaris na OBC. 

Wanapendelea baadhi za koo za Kimaasai za Purko na Loita kwa sababu ya wingi wao, uwezo na elimu yao kuliko koo nyingine za Sale, Kisongo, Batemi, Laitayok na kadhalika. Lolote likisemwa au kuandikwa kuhusu NGOs na koo rafiki za wakubwa linapigiwa kelele kuwa ni upotoshaji.

NGOs zinahamasisha Wamaasai wapeleke ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, zinawashinikiza Wamaasai kuweka makazi holela ya maboma eneo lote la Pori Tengefu ili kuifukuza OBC na kuharibu mazingira.

Baada ya NGOs za PWC, NGONET, PALISEP, PINGOs FORUM na washirika wao kwenda Arusha na kutengeneza mfumo mpya mbadala wa WMA, kwa upande mwingine NGOs za Ujamaa Community Resource Team (UCRT) na Tanzania Pastoralist Community Forum (TPCF) wanaendelea kuhamasisha ‘uasi’ katika vijiji vya kata saba za Ololosokwan, Soit-sambu, Oloipiri, Oloirien, Oloosoito, Arash na Piyaya.

(i) NGOs za TPCF na UCRT zilipita kisirisiri katika vijiji vya kata hizi na kuzungumza na baadhi ya viongozi ili kwa pamoja wawatafute, wawapendekeze ‘watu wao’ ili wawe wajumbe wawakilishi wa makundi yote ya vijana, kinamama, malaigwanani, wenyeviti na madiwani kwenye Kamati Teule ya Makani. Lengo la mpango huu ni kuhakikisha wananchi wanakuwa upande wa NGOs katika kuamua mfumo mpya wa kuwa na WMA badala ya Pori Tengefu.

Juhudi zinafanywa ili endapo maridhiano yatakwama, basi utumike utaratibu wa upigaji kura. Kwa kutumia utaratibu huo, NGOs zinaamini zitashinda kwa sababu tayari itakuwa zimeshafanya kazi ya kuwashawishi kwa hali na mali wajumbe.

NGOs za TPCF na UCRT zinafanya kile kinachotajwa kuwa ni kurejesha umoja wa Wamaasai wakitumia simu ndani ya vijiji vya kata saba na hata kwa Tarafa yote ya Loliondo. Kurudisha umoja wa Wamaasai maana yake ni kurudisha umoja wa koo za Purko, Loita, Laitayok, Sale na Kisongo kwa njia za simu ili kukabiliana na serikali na wawekezaji dhidi ya mpango wa kutenga kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi.

Kwa namna NGOs zilivyojipanga na kwa msaada mkubwa wa RC wa Arusha na DC wa Ngorongoro, hakuna dalili za kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro wa Loliondo.

By Jamhuri