Tangu mwaka 1974 wakati Filbert Bayi alipoweka rekodi mpya ya mita 1,500 duniani, Tanzania haijapata mafanikio mengine makubwa kiasi hicho katika riadha na hata michezo mingineyo.

Bayi ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), aliweka rekodi hiyo na kuwa bingwa mpya wa mbio hizo kwa miaka mitano, hadi nafasi hiyo ilipochukuliwa na mwanariadha Mwingereza Sebastian Coe mwaka 1979.

Ilipofika mwaka 1978, mwanariadha mwingine mahiri wakati huo, Gidamis Shahanga, alinyakua medali ya fedha katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika mjini Montreal, Canada, kabla ya Suleiman Nyambui naye kushinda medali katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi, mwaka 1980.

Mbali na rekodi hizo za kujivunia, Tanzania pia haijawahi kufuzu kwa mara nyingine tena kwenda kucheza Fainali za Soka za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) tangu mwaka 1980 ilipofanya hivyo kwa kuifunga Zambia.

Ilifuzu kwa bao lililowekwa wavuni na aliyekuwa mshambuliaji mahiri wa kushoto wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Peter Tino, katika mechi ya mwisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Independence mjini Lusaka, tena mbele ya maelfu ya mashabiki wa nchi hiyo wakiongozwa na aliyekuwa Rais wao wakati huo, Dk. Kenneth Kaunda, mwaka 1979.

Ilikuwa ni timu iliyokuwa chini ya unahodha wa Rais wa sasa wa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga, ambaye wakati huo alikuwa beki mahiri nambari mbili na nne.

Pamoja na kuondolewa mapema katika mzunguko wa kwanza wa fainali hizo zilizofanyika nchini Nigeria, lakini ilikuwa fahari kubwa kwa mashabiki wa soka nchini kuona kwamba tunaweza kwa vile ndiyo michuano mikubwa zaidi ya kandanda barani Afrika.

Wakati leo Jumanne Januari Mosi tumeingia katika Mwaka Mpya wa 2013, mashabiki wa michezo yote nchini wanajiuliza kama Tanzania itaendelea kuwa ngazi ya ushindi kwa mataifa mengine katika viwanja vya kandanda, netiboli, masumbwi, mpira wa wavu, gofu, tenisi, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, riadha na kadhalika.

Wanajiuliza kama Tanzania itaendelea kuwa wasindikizaji wa wengine katika michezo hiyo na hata mingineyo, hali iliyowachosha hasa ikizingatiwa kuwa, kwa mfano fainali za AFCON 2013 zinazoanza katika miji tofauti nchini Afrika Kusini Januari 19, mwaka huu, zinashirikisha hadi nchi ndogo kabisa ya Cape Verde.

Wanajiuliza inakuwaje nchi yenye wastani wa wakazi takribani milioni moja tu imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kiasi hicho kisoka, lakini Tanzania yenye zaidi ya wakazi milioni 40 imeshindwa kufuzu kwa miaka 32 hadi sasa.

Kwa mfano, mashabiki wa soka nchini bado wanajiuliza kwa nini Tanzania Bara ilishindwa kupata hata ushindi wa pili katika Michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika Desemba 8, mwaka jana, mjini Kampala, Uganda, kwa timu ya taifa mwenyeji (Uganda Cranes) kutetea ubingwa wake baada ya kuifunga Kenya (Harambee Stars) kwa mabao 2-1 siku ya fainali.

Tanzania Bara au Kilimanjaro Stars pia ilishindwa kupata hata nafasi ya tatu baada ya kufungwa kwa penalti 6-5 na ndugu zao wa Zanzibar Heroes katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na wa nne, siku ileile.

Ingawa wanariadha wa Kitanzania wamekuwa wakishiriki mashindano mbalimbali duniani kuanzia katika bara hili la Afrika yenyewe, Mashariki ya Mbali, Ulaya na sehemu nyingine, ushiriki wao bado umekuwa wa kusindikiza kwani hakuna anayeshinda wala kutunukiwa medali iwe ya dhahabu, fedha au ya shaba na hata zawadi ya fedha taslimu wakiwa washindi ama kwa kushika nafasi ya pili, ya tatu ama ya nne.

Wanaishia kushika hadi nafasi za 20, 30 na hata nyuma zaidi yake, jambo ambalo kwa miaka mingi iliyopita hadi sasa, limeendelea kutawala hasa tokea kizazi cha wanariadha kama Kanali Juma Ikangaa kilipong’atuka rasmi viwanjani katika miaka ya 1990.

Ndivyo pia hali ilivyo katika michezo mingine ikiwamo mikubwa ya masumbwi, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, netiboli, soka ya wanawake, kadhalika.

Pamoja na kikosi cha Taifa Queens kunyakua ubingwa wa mabara kwa mchezo wa netiboli katika mashindano yaliyofanyika hivi karibuni nchini Singapore, lakini inaaminika kwamba timu zote zilizoshiriki michuano hiyo ya kila mwaka hazikuwa lolote wala chochote.

Ndiyo maana Taifa Queens ambayo hata maandalizi yake ilipoweka kambi mjini Morogoro yalikuwa ya zimamoto zaidi imekuwa bingwa. Ilitelekezwa na Serikali na kukiacha Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kikiombaomba kila mahali bila mafanikio.

 

Inawezekana timu hiyo ilipokwenda Singapore na kurejea na kombe ilishinda kutokana na wachezaji wenyewe kutaka kuionesha serikali kwamba wanaweza, na kwamba hawawezi kulinganishwa na kaka zao wa Taifa Stars, dada zao wa timu ya taifa ya kandanda (Twiga Stars) wala wachezaji wa timu ya taifa ya ngumi au nyingine yoyote.

Katika hali hiyo na hata vinginevyo, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikiongozwa na Waziri wake, Dk. Fenela Mukangara, akisaidiwa na Naibu wake, Amos Gabriel Makalla, inapaswa kuweka mikakati au mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba yanafanyika mageuzi makubwa kwa michezo yote mwaka 2013.

Inabidi ivitumie vyama, mashirikisho na mabaraza ya michezo yote nchini kuhakikisha kila moja katika eneo lake la utawala linaweka mipango endelevu, lengo likiwa kuirejesha tena Tanzania katika heshima yake ya zamani kama ya mwaka 1974, 1978 na 1980.

Kila chama au shirikisho kuanzia Baraza la Michezo (BMT), TOC, Shirikisho la Kandanda (TFF), Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (TBF), Chama cha Riadha (RT), Chaneta na kadhalika, linapaswa kufanya tathmini ya kutosha ili kujua ni kitu gani kinachosababisha mchezo wake usipate mafanikio kimataifa.

RT, kwa mfano, inapaswa ihangaike kujua ni kwa nini hakuna mwanariadha mwingine tena aliyefanya kama Bayi tangu mwaka 1974, Shahanga mwaka 1978, Nyambui mwaka 1980 ama Juma Ikangaa aliyeshinda na kuzawadiwa gari aina ya Benz katika mbio za Marathon zilizofanyika mjini Tokyo, Japan, mwaka 1987.

Ndivyo pia nayo TFF inabidi ihakikishe kwamba timu yetu ya taifa ya kandanda inakwenda kwa mara nyingine tena katika fainali zijazo za AFCON 2015. Inatakiwa iweke mikakati madhubuti baada ya kushindwa kwenda Afrika Kusini baadaye mwezi huu na kuendeleza hadithi ileile iliyoanza tangu mwaka 1982.

Ndivyo pia TBF inavyopaswa kujiuliza inakuwaje siku zote timu yake ya taifa ya ngumi za ridhaa imekuwa ya kupandia ngazi kwa wapinzani wake. Inabidi ijiulize kwa nini mabondia wake wote wamekuwa jalala la ushindi wanaposhiriki michuano yote ya kimataifa kama vile ubingwa wa dunia, Olimpiki, ubingwa wa Afrika na hata michezo ya Afrika Mashariki na Kati tu.

Bila kushikamana pamoja, kujitathmini kikamilifu na hatimaye kuweka mikakati endelevu kwa michezo yote nchini, Watanzania wataendelea pia kwa mwaka huu wote, kushuhudia wachezaji ama timu zao za taifa zikiendelea kuwa jamvi la kupatia ushindi kwa wapinzani wao siku zote.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

By Jamhuri