MWALIMU NYERERE: MAENDELEO NI KAZI

Hotuba ya Rais wa Chama, Mwalimu Julius K. Nyerere, Kwenye Mkutano
Mkuu wa TANU wa 16.
Waheshimiwa sasa ningependa kuufungua Mkutano wetu rasmi. Nasema katika
ufunguzi huu kazi yangu kwa leo itakuwa, asubuhi hii, ni kuwasilisha kwenu
Taarifa ya mambo yaliyofanyika, katika utekelezaji wa maazimio tuliyoyapitisha
katika mkutano uliopita.
Hiyo ndiyo kazi nitakayoifanya. Kabla ya kuifanya kazi hiyo, ningependa kueleza
kwanza kwamba Mkutano huu tumeufanya kitofuti kidogo na mikutano yetu ya
namna hii. Sasa kama mnavyojua, tunakutana mara moja kila baada ya miaka
miwili tunafanya mkutano wa kazi kama huu.
Lakini vile vile, tunayo mikutano mingine na mwakani kutakuwepo mkutano wa
namna hii ambapo tutashughulika na mambo ya uchunguzi na mengineyo. Sasa
kwa mwaka huu. kwa desturi katika mikutano yetu hii, huwa tunakaribisha vyama
vya ndugu zetu kuja kushiriki nasi katika mkutano huu.
Kwa mfano, katika Mkutano uliopita,tulikuwa na wenzetu kutoka sehemu
mbalimbali pamoja na Zaire, Zambia na sehemu zingine. Mwaka huu tunakusudia
kwamba Mkutano huu uwe ni mkutano wa kazi na kama ni mkutano zaidi wa
kuulizana tumefanya nini katika miaka miwili hii iliyopita. Kwa hiyo, tukadhani si
mkutano unaowahusu sana wenzetu, afadhali kama tuna aibu zetu, tukasemezana
wenyewe hapa hapa bila kuwaingiza sana wenzetu.
Wenzetu, tunawakaribisha mwakani katika kutano utakaofuata ; kwa hiyo ndiyo
maana mnaona wenzetu hawapo. Lakini tunao ndugu zetu, kwanza tunao ndugu
zetu wa Afro- Shiraz, wao wako hapa hapa, kwa hiyo mnawaona hapa. Na pia
tunao ndugu zetu wa Vyama vya Wapigania uhuru, wao wako hapa hapa ; wao sio
kwamba ni wa kukaribisha watoke nje waje wao wako hapahapa.
Kwa hiyo, ndugu zetu hao tunao- kwanza tunao sasa hivi kwenye mkutano na kwa
sababu tunayo shughuli yetu itakayofuata leo mchana ni kupokea salaam za ndugu
zetu hao. Na kwa sasa nadhani ningependa nichukue nafasi hii kuwakaribisha

ndugu zetu kwamba wamejaliwa kuwa nasi katika mkutano huu. Tunawashukuru
sana.
Sasa baada ya hapo waheshimiwa, nasema kazi yangu ni kutoa taarifa
yautekelezaji wa maazimio tuliyoyapitisha katika Mkutano wetu wa 15 mwaka juzi
ambayo sasa hivi tumeyathibitisha kwamba yameandikwa sawa sawa kama
mlivyopewa katika kijikaratasi hiki. Nasema kwamba tumekubaliana kwamba
mkutano huu uwe ni mkutano wa kazi na kazi tutafanya wote si baadhi wafanye
kazi na wengine wasifanye kazi.
Kwa hiyo, nilivyofanya ni kwamba nimetayarisha taarifa, imechapishwa na
mtapewa kila mtu atapewa, ikiwa kuna wajumbe hapa ambao hawajatekeleza
azimio la Kisomo chenye Manufa, ole wao, mimi sikusudii kuwasomea taarifa hii.
Mimi nimefanya kazi yangu, nimetayarisha na Mchapishaji wa Serikali
tumembembeleza ametuchapia na sasa tutawapeni na kazi ya mkutano huu ni
kuona kama kweli tumejitahidi kutekeleza maazimio hayo.
Kwa hiyo nitataka kujua kama akina Rajabu Diwani na wengine waliomo humu
wamefanya jitihada ya kutekeleza maazimio hayo na njia moja ya kuonyesha
kwamba wametekeleza ni kusoma ripoti hii siyo mimi niwasomee.
Wananchi ripoti hii- taarifa hii kama nilivyosema inajaribu kueleza utekelezaji wa
maazimio tuliyoyapitisha. Maazimio hayo mtakumbuka ni mengi,
nitawakumbusheni machache. Moja tulikubaliana kwamba tuanze bila kuchelewa
jitihada ya kusomesha kila mtu Tanzania kusudi ifikapo mwaka 1975/76 iwe
Tanzania hakuna mtu asiyejua kusoma wala kuandika. Hilo ni moja ya maazimio
yetu hayo.
Pili tulisema kwamba tugeuze, tutazame tena upya mpango wetu wa Miaka Mitano
huu tunaouendeleza sasa hivi, tuone kama inafaa tuubadilishe kusema kweli
tulikubaliana tuubadili kusudi tuyatilie mkazo mambo fulani fulani,
tutakayotamka. tukasema tungependa mambo matatu yapewe umuhimu mkubwa
kuliko tulivyokusudia katika wakati wa kutayarisha mpango wa miaka mitano.
Kwamba tutilie mkazo mkubwa sana jitihada za kuwapa wananchi maji, shule na
matibabu. Tulikubaliana hivyo. Na taarifa hii inajaribu kueleza tulivyofanya
katika jitihada ya kutekeleza mambo hayo ya kisomo cha watu wazima kinaitwa

'Kisomo chenye Manufaa' ya kuwapa wananchi maji, ya kuzidisha elimu, ya shule
na kuwapa wananchi matibabu. Tarifa hii imefanya jitihada kwa kifupi kueleza
tulivyofanya kutekeleza mambo hayo.
Sasa katika taarifa yenyewe ambayo nitajaribu kuieleza kwa kifupi tunasema yako
mambo fulani fulani ya msingi ambayo kama hayakufanyika huwezi kutekeleza
hayo mambo tuliyosema tuyatekeleze. Huwezi kusomesha watu wazima, huwezi
kuzidisha elimu, huwezi kuzidisha maji wala huwezi kuzidisha matibabu. Mambo
yote hayo, nasisitiza katika taarifa yanategemea uchumi wa nchi.
Kwa bahati mbaya Mwenyezi Mungu hakutupa uwezo wa kusema 'maji njoo'
yakaja, hakutupa uwezo wa kutibu kwa miujiza tu au kusomesha watu kwa miujiza
tu, tukasema 'wananchi tangu leo wote muwe mnajua kusoma' basi wote tangu leo
wawe wanajua kusoma.
Kwa bahati mbaya tunapoamua kufanya mambo hayo,lazima tuyatimize kwa
juhudi mara nyingi sana ni juhudi zinazotokana na juhudi zetu za uchumi. Kwa
taarifa jambo la kwanza linalotiliwa mkazo ni umuhimu wa uchumi wetu,
tunasema katika taarifa yapo sasa hivi tukipita pita mahali, wananchi wanasema
wanapata maji ya bure, maji ya bure ni yale ya mvua, ikianza kunyesha unaweza
ukatega mdomo hivi ukanywa lakini maji mengine yote si ya bure yanagharimiwa.
Hakuna elimu ya bure ingawa kwa sasa hivi wanafurahi wananchi huko, wanasema
'tunashukuru' ninapozipata huzikataa pale pale, wenzangu wengi huko hukubali
mkasema kuwa 'ndiyo kweli tunatoa elimu ya bure'. Hatutoi elimu ya bure, wala
hakuna nchi yoyote ina uwezo wa kutoa elimu ya bure, hakuna. Elimu yote
nilazima ingharimiwe, kwa sababu lazima walimu walipwe mishahara yao, lazima
shule zijengwe, lazima vitabu vinunuliwe na chaki zinunuliwe na kalamu
zinunuliwe na wino ununuliwe na mabenchi wanayokalia watoto yanunuliwe na
viti vinunuliwe.
Elimu ya bure maana yake ni nini, hakuna hata kidogo kitu kinaitwa elimu ya bure,
ni njia ya mkato tu ambayo haisemi kweli inasema tu kwamba mzee mwenye
mtoto hatumtozi mfukoni mwake hela, tukamwambie hela hizi ni za elimu ya
watoto wako.

Tumeondoa hii. Tunatozana tu kwa jumla, tunatozana wote kwa jumla na baada ya
hapo tunasema, haya nendeni shule sasa. Watoto wanakwenda shule na nchi nzima
inalipa. Tunachokataa ni mtoto wa Tanzania akose kusoma kwa sababu baba yake
au mama yake hana uwezo wa kumlipia tu, tunasema Tanzania ina uwezo wa
kumlipia japo baba yake hana. Kwa hiyo, tunaondoa jambo hili la kusema kila
mzazi amlipie mtoto wake au mzazi anapompeleka mtoto hospitalini alipe dawa
kutoka mfukoni mwake, tunasema nchi italipa.