Wazaramo ni miongoni mwa makabila zaidi ya 125 yanayofahamika na kuunda taifa la Watanzania. Ni wakazi wenyeji wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Kiasili wana utamaduni wao na lugha mama mwanana – Kizaramo.

Kihistoria na kijiografia wana ndugu zao kiasili ambao ni Wakwere, Wadoe, Wamashomvi, Waluguru na Wakutu. Lakini kwa mbali wanao Wazigua na Wabondei. Wazaramo wanao watani wao ambao ni Wanyamwezi, Wasukuma, Wadigo, Wamakonde na wengine wengi.

Wazaramo katika mazungumzo yao wanatumia nahau na methali katika lugha yao kama yalivyo makabila mengine hapa nchini.  Wazaramo wana methali nyingi, ikiwamo hii:  “Mwana msekwa ndo mwana.” Methali hii inatoa mafunzo yenye onyo na hadhari.

Methali hii ina chanzo chake kinachotokana na hadithi ya mtoto wa dondola na mtoto wa nyuki katika kutengeneza asali. Leo sitazungumzia hadithi hiyo. Kusudio ni kuelezea maana na funzo tunalopata katika methali hii.

Leo, mtoto anayeonekana hana mvuto, hana uwezo wa kufanya jambo, ni kama dhaifu, anapuuzwa na kuchekwa. Lakini baadaye huonekana ni mtoto mzuri, bora na mchapakazi. Ni mtoto mwema, mkakamavu, mpenda haki na mtetezi wa wanyonge. Naamini tabia hii iko katika jamii ya watu mbalimbali.

Mwonekano wa mtu usitolewe hukumu bila kwanza kupewa nafasi ya uchunguzi na uthibitisho wa mwonekano wake kwako. Ni mzuri au mbaya. Una faida au hasara. Ni salama au hatari na kadhalika, ndipo utoe hukumu. Muungwana hutembea na tabia njema. Habebi tabia ya kebehi na puuza.

Methali hii ina mawanda mapana katika mustakabali wa mifumo ya maendeleo ya watu. Iwe katika uongozi, utumishi au utawala. Iwe katika mambo ya ulinzi, usalama, masomo, michezo au sanaa. Inawezekana methali kama hii inapatikana katika kabila lako. Je, unaitazama vipi?

Tumepata kusikia, kuona au kutenda mambo yanayobeba maneno ‘Mwana msekwa’ na baadaye kubaini si hivyo. Ni kinyume chake.

Tukaanza kubeba maneno, ‘ndo mwana.’ Matokeo ni kuona aibu, kufedheheka na kupatwa na butaa. Lakini kwa ‘mshenzi’ ni sawa kama uji na mgonjwa.

Angalia kwenye masuala ya kazi, masomo, siasa, michezo, maigizo, ngoma na sanaa mbalimbali washiriki wanavyokuwa awali na baadaye. Hata kwenye uongozi wa siasa, utumishi wa umma na katika shughuli mbalimbali, methali hii inavyorandaranda na kuwaumbua watazamaji katika maeneo haya.

Mathalani, Rais Dk. John Pombe Magufuli kabla ya kuwa rais, alipokwenda mikoani kupata wadhamini katika nafasi aliyoikusudia, na wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais, baadhi ya viongozi na wanachama wa chama chake na wananchi walimpuuza na kumkimbia. Walitumia sehemu ya methali, ‘mwana msekwa.’

Alipounasa urais na kutoa msimamo, maono na dira ya maendeleo ya nchi, baadhi ya viongozi na wanachama wenzake pamoja na wananchi fulani, walimdharau na kumpuuza. Na wengine kudiriki kutamka kwamba hawezi kutimiza asemayo. Maneno na vitendo vyake ni nguvu ya soda.

Ndani ya miaka minne tu, kauli anazozitema na kuzisimamia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, bila hofu, bali kwa uwezo na ujasiri, ameushangaza ulimwengu. Waliokuwa marais wa nchi yetu na marais wa Afrika wanampa kongole na heko kemkemu. Hao wananchi ndiyo usipime.

Wazungu wa Canada, Marekani na Ulaya pamoja na Waasia wa India, China na Japan wanakiri Rais  Dk. John Pombe Magufuli si mwana msekwa kama watu wanavyoamini. Yeye ‘ndo mwana.’ hasa wa Afrika. Na wengine kutamka, Magufuli ni mtoto wa mhunzi (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere).

Ukweli usio na punje ya shaka, Rais Magufuli ndo mwana wa Afrika, pale viongozi wa  SADC walipobwaga mioyo yao baada ya kuona shahiri ujenzi wa miundombinu mikubwa ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Nani kama Magufuli? Hapa Kazi Tu, ndani ya mwana msekwa ndo mwana.

153 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!