Kwa mara nyingine Bara la Afrika limeondokewa na mwanamapinduzi jasiri, mpiganaji na mtetezi wa haki na mali za Waafrika. Kiongozi shupavu na mkweli, aliyebeba uzalendo na mwenye msimamo katika hoja na maono yake. Ni kiboko cha mabeberu wa nchi za Magharibi na vibaraka.

Nina mkusudia kiongozi msomi, Robert Gabriel Mugabe, aliyezaliwa na kupitia maisha ya raha, tabu na misukosuko mingi ya kisiasa na kiuchumi katika kuweka mifumo bora ya maendeleo ya jamii nchini Zimbabwe. Amefariki dunia akiwa katika matibabu nchini Singapore.

Septemba 6, 2019 ndiyo ulikuwa mwisho wa kuona nuru ya dunia na safari iliyomchukua miaka 95, ambayo ilianzia Februari 21, 1924. Mungu ampokee Robert Mugabe na kumlaza mahali pema peponi. Amin!

Wazalendo wa Afrika na watetezi wa haki duniani tutamkumbuka mwanamapinduzi huyu Kutokana na ujasiri, ukweli na msimamo wake katika uongozi na ukombozi wa nchi yake Zimbabwe.

Afrika inazidi kupoteza viongozi shupavu wasiokubali kupuuzwa na kudhalilishwa kwa kuhongwa visenti, kashata na anasa zinazotengenezwa na mabeberu. Miongoni mwao ni Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria, Kwame Nkrumah wa Ghana, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Gamal Abdul Nasser wa Misri na wengine wengi.

Utawala haramu wa walowezi wa Rhodesia (sasa Zimbabwe) ulioongozwa na Waziri Mkuu, Ian Douglas Smith, kuanzia mwaka 1964 – 1978 dhidi ya wananchi, ulimkera na kumghadhabisha Robert Mugabe hata kuingia msituni kuanzisha jeshi la vita kupambana na walowezi hao.

Kuasisiwa Chama cha ukombozi – ZANU PF kupigania uhuru wa nchi hiyo dhidi ya walowezi kuliongeza hamasa katika harakati za ukombozi kwa Mugabe na wananchi wenzake. Lakini uzalendo wake ulimtia hatiani mbele ya utawala haramu na akaswekwa jela miaka 10 (1964-1974).

Kifungo chake gerezani kilimtia kiburi zaidi kupambana na walowezi hao. Alitumia vema nafasi hiyo kujielimisha mambo ya sheria, usimamizi, sayansi na elimu kwa ujumla na kutwaa shahada zilizomwongezea mbinu na maarifa zaidi ya kupambana na mabeberu. Hakika alikuwa mtu wa bidii na hakupenda kushindwa.

Baada ya miaka 10 gerezani na nchi yake kupata uhuru mwaka 1980, alishika uwaziri mkuu tangu mwaka 1980 – 1987 na kuanzia mwaka 1987 – 2017 alikuwa Rais wa Zimbabwe. Alipiga pigo takatifu la kuwanyang’anya ardhi walowezi na kuwarejeshea wenyewe wananchi, chini ya ilani ‘One Man One Farm.’

Kitendo hicho kiliwakasirisha mno walowezi na Wazungu wenzao mabeberu wa nchi za Magharibi na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Zimbabwe. Hukumu hiyo, vitisho na njama mbalimbali za kuitia umaskini Zimbabwe, havikuweza kuvunja wala kuteteresha msimamo wake Mugabe.

Katika enzi za uhai wake, Rais Mugabe aliweka sera na kutoa elimu bure, na wananchi wengi walikwenda shuleni. Aliweka mfumo wa afya bure na wananchi walipata matibabu. Mugabe alitambua elimu na afya bora ni vichocheo vya uchumi na misingi ya maendeleo ya jamii katika taifa lolote.

Kiongozi huyo hakujitia hofu, hakuyumba au kuwapigia magoti na kuwasujudia mabeberu kwa hatua walizozichukua dhidi yake na wananchi wa Zimbabwe. Alichofanya ni kuwasema, kuwakemea na kuwasimanga jinsi walivyokosa utu na maneno ya shukrani kwa Waafrika kwa kuwapora mali zao.

Viongozi, wananchi wazalendo na vijana wa Afrika hatuna budi wakati huu wa maombolezo kumkumbuka na kumuenzi kwa mema aliyotutendea. Ameacha mifano ya kuiga katika elimu alipotwaa shahada saba, msimamo katika haki, ukombozi na ukweli katika uongozi. Hakika huyu ni ‘Jongwe.’

By Jamhuri