Mwenyekiti UVCCM adai Chadema itaambulia majimbo mawili 2020

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James ametamba kwamba chama chake kitashinda katika uchaguzi mdogo wa Agosti 12, mwaka huu katika kata zote na ubunge wa jimbo la Buyungu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni katika Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha, James alisema CCM imejiandaa kupima ‘mitambo’ yake katika uchaguzi huo ili kuhakikisha inakifuta Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Nataka kuwaambia kwa namna mitambo yetu ilivyofungwa hakuna mgombea wa upinzani ambaye atashinda, na mwaka 2020 Chadema watabaki labda ya majimbo mawili tu kusini moja na kaskazini moja,” alisema.
Alisema katika kuhakikisha kazi zinafanyika vizuri, wabunge wa upinzani wataporomoka wote mwaka 2020 na CCM itakaa yenyewe ili kupitisha mambo ya maendeleo kwa Watanzania.

“Bora tukae wenyewe kura ziwe za ndio, wanatuharibia sakafu za bungeni , wenzao wamekaa, wao kila mara wanatoka na kupinga mambo,” alitamba

Akizungumzia jimbo la Arusha, James alieleza kusikitisha na kuongozwa na watu wasio na uwezo na kudai kuwa sasa ni lazima Chadema wote wasafishwe.

Kwa upande wake mgombea wa udiwani wa chama hicho Prosper Msofe ambaye aliwahi kuwa Naibu Meya jiji la Arusha kupitia Chadema na baadaye kujiunga na CCM, aliwaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua tena kwani amejipanga kuwasaidia wananchi kwa ushirikiano na Serikali chama chake.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole amewataka wakazi wa Kata ya Makanya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kumchagua mgombea udiwani wa CCM, Amiri Mbwambo ili awe kiunganishi kati yao na Serikali.

Polepole alitoa kauli hiyo juzi katika Kata ya Makanya wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika kata hiyo ambayo mgombea wake kupitia CCM alijiuzulu kutoka Chadema.

Alisema maendeleo yanayoonekana katika Wilaya ya Same yanatokana na sera nzuri za Serikali ya CCM ambayo ndio imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Awali mbunge wa Same Magharibi Dk David Mathayo aliwataka wananchi wa Makanya kumchagua Mbwambo ili aweze kushirikiana naye kuharakisha maendeleo katika kata hiyo.

Source: #Mwananchi