Nakutambua, nitambue

Jina langu ni Nani. Umri wangu ni zaidi ya karne ishirini na moja. Nimeumbwa kwa udongo na maji. Ninaye ndugu yangu, majirani na marafiki. Nimejaaliwa kupata watoto, wajukuu, vitukuu na vilembwe. Niko ulimwenguni.
Nimekula chumvi nyingi na kuona mambo mengi. Hii ni sifa muhimu kwako kutambua. Nimetawaliwa, nimenyanyaswa, nimenyonywa na nimeonewa. Sababu ni unyonge wa vizazi vyangu. Laiti vizazi hivyo visingekuwa na ujinga, ushamba na ulimbukeni, leo ningekuwa tajiri wa matajiri ulimwenguni.
Muumba wangu amenipa mali nyingi na kunibariki tumbo lenye rutuba. Amenizawadia hewa safi na majira ya joto, kipupwe, kiangazi na masika. Lengo la Muumba wangu ni vizazi vyangu visipate shida. Lakini vinapata taabu kutokana na ujinga na ulimbukeni.
Nafahamu una hamu ya kunijua mimi ni nani kimaumbile. Nakuomba usiwe na wasiwasi punde tu utanijua. Nimeshapewa majina mengi na vizazi vya wenzangu wa kutoka Matlai na Machweo ya jua. Wamenikuta Nani nikiwa mwenye afya, uwezo na mali kedekede.
Si mimi tu, ndugu yangu, majirani na marafiki zangu wote tumepachikwa majina na hao watokao ng’ambo ya mto. Binafsi nililia sana na kuwakemea wanangu wanavyoonewa. Nilifurahi wanangu walipozinduka. Kumbe ikawa bure ghali. Naendelea kulia na kusikitika.
Kuzinduka kwao kulihitaji akili na ufahamu wa mambo na mazingira yaliyowazunguuka. Na hayo ndiyo yaliyokuwa matazamio yangu. Hali haikuwa hivyo, wanangu waliingiwa na fahamu za kusigana, kupigana na kusalitiana. Eti! wameona huo ni upeo wa fahamu zao. Naumia wanangu.
Majawabu yakawa heri ya wale waliotoka ng’ambo ya mto kuliko hawa wanangu. Wao ndiyo wakashika mikuki na mishale na kuvaa mataji ya rushwa, ufisadi, usaliti na ukuwadi. Sielewi ni lini nitatokana na majanga ya ujinga, umaskini na maradhi.
Ungependa nikueleze mengi kuhusu maisha yangu lakini muda si rafiki kwangu. Karatasi na wino ni bidhaa adimu na ghali kwangu. Haya ni baadhi ya majanga wanayonifanyia vizazi vyangu. Basi, pokea maelezo hayo machache ni ziada kwako. Kwani hakuna ziada iliyo mbovu. Sasa najieleza.
Kwenye rasi yangu nimepewa vichuguu, milima na majabali yaliyohifadhi sampuli za madini – chuma, shaba, bati na fedha. Dhahabu, almasi, mawe na jasi. Sijasahau chumvi, mafuta na zebaki. Achilia mbali urani (uranium), rubi, gesi asilia. Vilembwe wangu wanajipamba kwa vito vya feruzi, yakuti, lulu na vinginevyo.
Nina sura ya tabasamu yenye kumvutia yeyote kuniangalia. Moyo wa imani na upendo na ulimi wa fasaha. Vicheko ni pumzi yangu na furaha ni huba yangu. Walio ng’ambo ya mto huja kwangu kufuata mazungumo, ushauri, makazi na biashara salama.
Kifua kimejaa mito, maziwa na bahari zenye kulea na kuhifadhi viumbe vingi vya kuvutia. Samaki, viboko, mamba n.k. Wanangu hupata ajira. Wajukuu huvutiwa na mazingira ya maeneo hayo kwenda kuoga na kucheza michezo ya majini na fukweni na kukonga nyoyo zao.
Tumbo lenye rutuba linalotoa watoto wa kike na kiume kuanzia kwa binadamu, mnyama, ndege na mdudu. Watoto wenye akili, watundu na watukutu. Cha ajabu baadhi ya watoto hujisahau kujitambua na kutambua ulimwengu ulivyo. Hiyo ndiyo sababu ya kutengeneza shaka.
Miguuni nimejaa vichaka, misitu, mbuga na mabonde yenye rutuba, mboji na chemchemi. Kilimo cha mazao ya chakula na biashara ni sifa yangu. Misitu na nyasi zinaulizana hali. Wadudu, ndege na wanyama huwavuta wafanyabiashara na watalii kuingiza mapato katika hazina yangu.
Simba, chui, ndovu na twiga. Mamba na mijusi, mbuni na korongo, vipepeo, duduvule, nyenze na senene vyote hivyo ni vivutio na baadhi ni vitoweo kwa vizazi vyangu na vya wenzangu. Utajiri wote huo uliwafanya  wa ng’ambo kupora, kuhadaa na kughilibu.

Tazama ramani utaona nchi nzuri,
Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka,
Nasema kwa kinywa halafu kwa kusitiri,
Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania.

>>ITAENDELEA

931 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons