Ni wangapi wamefanyiwa utapeli katika harakati za kununua viwanja au nyumba. Ni wangapi wamepata hasara kubwa kutokana na michezo ya utapeli iliyotamalaki katika ardhi nchini.
Ni kesi ngapi ziko mahakamani zinazohusisha utapeli katika mauzo na manunuzi ya ardhi. Idadi ni kubwa mno na huu ndiyo ukweli.
Siku zote huwa tunasema ni vigumu kujua ukubwa na hatari ya jambo hili mpaka likukute au limkute mtu wako wa karibu. Lakini swali ni ikiwa watu wamekuwa wakijifunza kupitia wenzao ambao wamekutwa na haya. Kama na wewe bado hujajifunza basi ni muhimu sasa kujifunza.

Mtu anauza ardhi moja kwa watu hata zaidi ya wanne tofauti, mtu anauza ardhi asiyokuwa yake huku akijua kabisa sio ya kwake, mtu anaghushi hati au leseni ya makazi kisha anauza kiwanja au nyumba ya mtu, kiongozi wa serikali ya mtaa anashiriki kuuza ardhi ya mtu huku akijua kuwa juzi mtu mwingine alinunua ardhi hiyo hiyo, kwa ufupi hali ni mbaya na ni vema kusema ili watu wachukue tahadhari.
Wizara ya Ardhi imeshasema mara nyingi kuwa moja ya sababu kubwa inayopelekea watu kutapeliwa katika manunuzi ya ardhi ni wanunuzi wenyewe kutozingatia taratibu za kisheria za manunuzi. Migogoro mingi imezalika hapa.
Mara kadhaa tumewahi kueleza kwenye makala mbalimbali namna salama ya kununua ardhi kwa kuepuka utapeli. Zipo makala nyingi ambazo zimeeleza hatua za kufuata ili uwe salama.
Hata hivyo, leo kitaelezwa kitu kingine ambacho hakikuwahi kuelezwa. Ni namna ya kuhakiki hati au leseni ya makazi ili kujua ikiwa ni halisi (original) au feki kabla ya kununua kiwanja au nyumba.

1. Uhakiki uliowahi kushauriwa
Kabla ya kueleza njia nyingine ya uhakiki inayotakiwa kuelezwa leo hebu tujikumbushe njia iliyowahi kuelezwa katika makala zilizopita. Ni uhakiki wa hati kwa njia ya upekuzi rasmi (official search). Tulisema kuwa kupitia njia hii utaandaa maombi kwenda kwa Msajili wa Hati (Registrar of Title) ukitaka kujua ikiwa nyumba/kiwanja unachotaka kununua kama kina mgogoro au ikiwa kuna mtu mwingine mwenye maslahi juu yake.
Mgogoro ni kama kuna zuio la kifamilia (caveat), zuio kutoka mahakamani na mengine yanayofanana na hayo. Na kuwapo mtu mwingine mwenye maslahi ni kama kiwanja au nyumba hiyo kuwa imesimama kama dhamana ya mkopo n.k. Majibu ya vitu vyote hivi utayapata utakapojibiwa maombi yako ya upekuzi rasmi (official search).

2. Uhakiki wa kuijua hati halisi
Hili ndilo linaloshauriwa leo. Ni uhakiki wa kujua ikiwa hati ni halisi au feki. Upekuzi rasmi (official search) ulioelezwa hapo juu kazi yake siyo kuonesha uhalisi au ubatili wa hati bali husaidia katika kujua taarifa/maudhui (contents) za hati. Na hii ni kwa sababu unapopeleka maombi haya hairuhusiwi kuambatanishi hati.
Ni kupitia njia hii ya kuwasilisha hati halisi kwa msajili unapoweza kujua uhalisi au ubatili wa hati. Basi unachotakiwa kufanya ni kuchukua hati ya kiwanja au nyumba unayotaka kununua na kuipeleka kwa msajili wa hati. Kama muuzaji hatokubali kukupa hati ili ukaihakiki basi muombe uongozane naye akiwa ameishika yeye mpaka kwa msajili.

Lakini hautaenda hivyo bali utafanya maombi maalum ambapo siku utakapokuwa unapeleka hiyo hati utakuwa tayari umepeleka maombi kwanza au iwe siku hiyo ndiyo unapeleka maombi pamoja na hati kwa uhakiki. Pia unaweza kuwatumia wanasheria katika hili.
Msajili wa hati anachokifanya ni kuchukua hiyo hati mliyoileta na kuikagua kwa kutumia mfumo (system) ikiwa ni halali na ikiwa kweli ilitolewa na ofisi yake. Ikiwa iko sawa atathibitisha na kubariki muamala wenu na ikiwa si sawa pia atasema. Hakuna namna ambavyo unaweza kupewa hati feki ikiwa ulipitia utaratibu huu. Hata mabenki yanayokopesha kwa kukubali dhamana za hati hujiridhisha kwa njia hii ili kukwepa dhamana feki.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri