Tutofautishe timu ya majadiliano na Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni.
Kawaida timu ya majadiliano haiundwi na wakurugenzi wa kampuni, bali wakurugenzi wa kampuni ndio huwa wanateua watu wa kuunda timu ya majadiliano na hao walioteuliwa huripoti matokeo ya majadiliano kwa Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya utekelezaji.
Bodi ya Wakurugenzi husubiri taarifa ya timu ya wataalam kwa ajili ya utekelezaji. Bodi ya Wakurugenzi ndiyo injini ya kampuni na kazi yake ni kutekeleza kile ambacho iliagiza.
Inaweza kutokea katika timu ya majadiliano akaingia mkurugenzi mmoja au wawili, lakini si kwa namba kubwa. Timu ya majadiliano huwa ni timu inayoundwa na wataalam wenye ujuzi na eneo linalotakiwa kujadiliwa ambao wakati mwingine huajiriwa tu kwa ajili ya kazi hiyo, na wakati mwingine huwa si wafanyakazi wa kampuni husika.

Kuna orodha ndefu ya majina inazunguka kwenye mitandao ya kijamii. Orodha hiyo imesheheni watu wenye ma-vyeo na majina makubwa ya Wakurugenzi wa Barrick huku maelezo yakiisherehesha kwa furaha orodha hiyo kuwa hiyo ndio timu ya majadiliano ya Barrick.
Pia wiki iliyopita orodha hiyo hiyo ilifanywa habari kuu katika ukurasa wa mbele kabisa wa gazeti moja binafsi la Kiingereza hapa nchini kwa maelezo hayo hayo kuwa hiyo ndiyo timu ya majadiliano ya Acacia.
Hawa walikwenda mbali hata kuweka picha ya kila mkurugenzi na kusisitiza kuwa bodi hiyo imesheheni wazungu pekee, isipokuwa Mwafrika mmoja tu.
Kwa namna orodha hii inavyoripotiwa kwa mbwembwe, haraka utagundua jambo moja. Utagundua kuwa lengo lake si kutoa taarifa, bali lengo kuu ni kuwatia Watanzania hofu, woga, unyonge, kuwakatisha tama na kuwajengea taswira ya kushindwa hata kabla majadiliano yenyewe hayajaanza.

Na ni walewale waliosema tutashindwa kesi wakati hatujafungua kesi yoyote. Ni walewale waliosema tutalipishwa mabilioni ilhali mhusika akijitokeza na kuomba radhi. Ni walewale waliosema Acacia hajatenda kosa lolote kabla ya mhusika kuja na kukiri makosa. Ni walewale waliojivika usemaji na uwakili wa Acacia hata kabla ya kupewa kazi hiyo na mhusika. Yaani ni walewale na ni walewale.
Jamani, hadi sasa orodha hii si ya kweli. Ukweli ni kuwa hadi sasa Barrick hawajatoa taarifa na orodha rasmi ya timu yao ya majadiliano. Ni walewale tu wame-google wakabeba orodha nzima ya Bodi ya Wakurugenzi wa Barrick kama inavyoonekana kwenye tovuti wakaiita timu ya majadiliano. Tunajua kabisa dua zao zote orodha hii iwe ya kweli, iunde timu ya majadiliano na ikiwezekana kama Barrick wanaweza kupata hata mtaalam kutoka mwezini au sayari nyingine yoyote au hata malaika, basi naye awepo ili kuihakikishia Acacia ushindi. Hii ndio dua yao. Hii ndio dua ya baadhi ya Watanzania wenzetu!

Lakini jambo hili haliondoki hivi hivi, bali limetufunza. Limetuonyesha ni kiasi gani ukoloni ungali unatafuna akili za baadhi ya Watanzania. Baadhi ya Watanzania bado wanaogopa wazungu. Baadhi ya Watanzania bado wanaamini wao ni daraja la pili. Baadhi ya Watanzania bado wanaamini Mwafrika hawezi kumshinda mzungu hata kama ana haki. Baadhi ya Watanzania bado wanaabudu rangi.
Tunao watu ambao kila hatua tunayopiga lazima watafute namna ya kuidhoofisha. Lazima watafute namna ya kuonyesha upande tulio na udhaifu huku wakiacha kuonyesha upande tulio na uthabiti. Yaani hao hata siku tukilipwa hela watasema mmepewa hela ya bandia!
Kuna haja gani ya kusema timu ya Barrick itaiangusha timu yetu na hali hamjajua timu yetu itakuwa na nani nani? Labda tutakodi wale wote waliowahi kuwa wanasheria wakuu wa Marekani! Maana hao ndio mnaowaogopa.
Ndugu zangu, wako watu ambao ukijitokeza ukasema mimi ni mganga naweza kufanya kila kitu kiharibike, watakulipa hela yoyote ufanye hivyo. Yaani wanahakikisha kila hatua tunayopiga inajengewa fitna yake. Ni ukweli kabisa kuwa bora mchawi kuliko mfitini.
Wako watu ukiwahakikishia kuwa kupitia sakata hili unao uwezo wa kuligeuza taifa hili kama Zimbabwe, basi watakulipa kila kitu na wakiishiwa wako tayari wakupe hata wake zao.

Wako watu kwa ndimi zao na matendo yao unaweza kufikiri si raia wa nchi hii. Unaweza kufikiri hawaishi hapa, hawana shangazi hapa, hawana mjomba hapa, hawana kaka na hawana dada hapa. Sitaki kuzungumzia watoto na wake labda wamejiandaa Tanzania ikiwa kama Zimbabwe watakimbia nao.
Haitoshi hata kidogo kuwaita watu hawa wakosa uzalendo. Kutumia maneno Kukosa Uzalendo kuwaelezea watu hawa ni kuwapendelea kabisa. Ni kuwapa sifa njema wasiyostahili. Hawa wamekuwa maadaui wa Tanzania. Yafaa tuwaite maadui wa Tanzania. Ni maadui wa Watanzania wanyonge na maskini.

Hata hivyo kila historia ya ukombozi wa kisiasa au kiuchumi imeshuhudia watu wa aina hii. Hii ni kote duniani. Hapa kwetu miaka ya 50 wakati Mwalimu Nyerere na wenzake wakipigania Uhuru walikutana na watu wa aina hii. Hawakuwa wageni, bali wazawa kama ilivyo sasa. Walimwambia Mwalimu na timu yake kuwa mtashindwa. Walimwambia Mwalimu kuwa mzungu si kiumbe wa kuchezea. Walimtolea mifano ya maeneo ambako wamejaribu kupigania Uhuru na kushindwa na wapiganaji kupotezwa huku wakiacha kutoa mifano ya yale maeneo ambako wapiganaji walifanikiwa na kupata Uhuru.

Majira yale na ya sasa hayana tofauti. Utamuona Mtanzania akitoa mifano ya Zimbabwe ambako wameshindwa huku akiacha kutoa mifano ya Libya ya Gaddafi na Botswana ambako walishinda na rasimali zao kugeuka lulu kwa raia wao. Utamuona Mtanzania akipenda na kufurahia kutoa mifano mibaya kabisa kwa Taifa lake huku akiacha ile iliyo mizuri.

Miaka ya 1967 na 1970 wakati Mwalimu ameitoa Tanzania katika siasa za kibepari na kuipeleka katika siasa za ujamaa watu wa namna hii walimshambulia sana Mwalimu. Wakati akiwajibu, Mwalimu alisema katika hotuba yake moja, “Madhali nia niliyonayo ni nzuri, basi sitageuka nyuma na kuwa jiwe. Sikubali kuwa jiwe, nitaendelea mbele mpaka lengo litimie.”
Juu ya maneno ya Mwalimu nimalizie na busara za wahenga ambao walisema, mpiga ngumi ukuta huumiza mkonowe. Bila shaka hila za hawa ni ngumi za ukutani na bila shaka wanachoumiza ni mikono yao wenyewe.

EWE MWENYEZI MUNGU, IBARIKI TANZANIA YETU

By Jamhuri