Nchi inavyoliwa

Yaliyoandikwa kwenye mtandao
Tanga ni mkoa wa pili kuwa na bandari kubwa nchini Tanzania na ndiyo makao makuu ya raia huyo wa Uswisi anayemiliki Amboni Sisal Properties Ltd (ASPL).

ASPL inamiliki mashamba matatu ya katani ya Kigombe, Pongwe na Magoroto ambayo yanajishughulisha na kilimo na utalii. Shamba la Kigombe huzalisha tani 2,000 za katani kwa mwaka na ni moja ya mashamba makubwa nchini Tanzania. Linauza nusu ya mkonge safi ya daraja la 3L na 3S katika  maeneo 20 tofauti duniani.

Katika wavuti wa kampuni hiyo, anajinadi kuwa anamiliki kiwanja cha ekari 360 za uwanja wa gofu wa kwanza Tanzania kwa uzuri na wenye makazi. Eneo hilo linafikika kirahisi kwa gari kutoka Tanga kwani muda wa dakika 40 kufika Pangani.

Anaendelea kujinadi kuwa barabara za Tanzania Bara kwenda Kenya ni nzuri na unaweza kuendesha gari kwa saa 10 kutoka Pangani hadi Nairobi na Mombasa hadi Pangani ni saa tatu.

Anasema kutoka Moshi hadi Pangani hutumia saa 4 na Pangani kwenda Arusha saa 5 na kutoka Dar es Salaam hadi Pangani ni saa tano na kujinadi kupitia mtandao huo kuwa ni karibu mno kutoka katika uwanja wa ndege wa Tanga, Kilimanjaro na Dar es Salaam. Anasema katika eneo hilo atajenga uwanja wa ndege kwa kiwango cha moramu na utaruhusu ndege ndogo kutua.

Kusini mwa shamba la Kigombe kutaendelezwa wastani wa mashimo 71, na viwanja 18 vya kuchezea gofu ambavyo vyote vitabuniwa na Tommy Fjastad. Uwanja wa gofu ndiyo utakaokuwa pekee wenye nyumba zilizojengwa katika viwanja vya nusu au ekari moja zitakazokuwa zinatazamana na Bahari ya Hindi.

Katika tovuti hiyo, Dk. Hess amsema kutakuwa na huduma za hoteli, uwanja wa ndege binafsi, viwanja vya tenisi, maduka makubwa, klabu za usiku, bwawa la kuogelea na mengineyo.

“Nchi imebarikiwa kuwa na wanyamapori wengi, ina jiolojia ya ajabu: kreta, volcano,” anajinadi.