Ndoto ya ‘Simba Mo Arena’ imeyeyuka? 

DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

“Ukiona mtu mzimaaa mamaa! Analia, mbele za watu ujue kuna jambo.” Sehemu ya kiitikio cha wimbo wa Msondo uitwao ‘Kilio cha Mtu Mzima.’

Tangu alipochukua jukumu la uenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amekuwa mzungumzaji mzuri na vyombo vya habari, lakini hali ilikuwa tofauti hivi karibuni alipoamua kutoa jibu moja kwa maswali yote!

Hicho ndicho unachoweza kusema wakati Mangungu alipozungumza na kipindi cha ‘Sports Court’ cha Wasafi FM kuhusu hatua zilizofikiwa na klabu katika ujenzi wa uwanja wake.

Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa hivi: 

Mtangazaji: Wapenzi na mashabiki wa Simba wanataka kujua suala la ujenzi (wa uwanja) limefikia wapi?

Mangungu: Subirini taarifa rasmi. Tutawaambia.

Mtangazaji: Ni kiasi gani cha fedha mlichokusanya hadi sasa kwa ajili ya ujenzi?

Mangungu: Subirini taarifa rasmi. Tutawaambia.

Mtangazaji: Lini sasa tutegemee uwanja wa Simba utaanza kujengwa?

Mangungu: Subirini taarifa rasmi. Tutawaambia.

Ukimsikiliza Mangungu na kinachoendelea sasa ndani ya Simba, ni wazi vitu havipo sawa tena. Waingereza wana msemo: ‘honeymoon is over’.

Miaka minne ya fungate inaelekea mwisho. Ile amani, shangwe iliyotawala imeanza kuyeyuka na watu wameanza kunyoosheana vidole katika kila jambo.

Wanachama, mashabiki na makundi hasimu ambayo hayakuwa na nafasi, sasa wameanza kupata nguvu kwa sababu ile nguvu ya fedha na mafanikio ya timu uwanjani vimeanza kutoweka.

Wadau wanataka kujua fedha walizochangishwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja zimetumika vipi, maana viongozi wamekuwa kimya.

Baada ya kumaliza kudai taarifa za matumizi ya fedha za uwanja, hawataishia hapo. Watageuka kuuliza na kutaka kujua matumizi ya Sh bilioni 20 zilizowekwa na mdhamini Mohamed Dewji.

Mangungu, katika maswali haya magumu, yeye anakuja na jibu moja tu rahisi ‘subirini taarifa kamili tutawaambia’. 

Bila shaka kusubiri taarifa kamili ni jambo jema, lakini anatakiwa kujua namna ya kuzungumza hasa katika kipindi ambacho tayari yameanza kuibuka maswali mengi juu ya matumizi ya fedha.

Majibu ya aina hii yangekubalika kwa wepesi miaka minne iliyopita wakati Simba ilikuwa bora uwanjani kwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu mara nne; huku misimu miwili, 2019/20 na 2020/21 ikitwaa taji la ligi na Kombe la ASFC.

Simba inapofanya vizuri uwanjani hakuna mtu wa kuuliza chochote kinachofanywa na viongozi kwa wakati huo zaidi ya kufurahia ushindi.

Hali ni tofauti kwa sasa, kwa kuwa Simba inaelekea kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu mbele ya watani wao, Yanga, wakiongoza kwa tofauti ya pointi 13.

Hivi karibuni, kiongozi wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage, aliweka bayana kwamba mwaka huu Simba wasahau kuhusu ubingwa.

Rage anasema: “Hatuwezi kutwaa ubingwa labda itokee miujiza. Wapinzani wetu wana nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa baada ya kusubiri kwa miaka minne.”

Baada ya sare dhidi ya Namungo, Mbunge wa Njombe na shabiki mkubwa wa Simba, Festo Sanga, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Nimekubali, Yanga Bingwa msimu 2021/22. Simba tujipange msimu ujao.”

Uongozi wa Simba unapaswa kujitokeza mapema na kueleza nini kinachoendelea kuhusu ujenzi wa uwanja, kuliko kukaa kimya. Kufanya hivyo ni kukaribisha matatizo zaidi siku za usoni.

Ahadi hewa ya uwanja

Ahadi za ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Simba hazijaanza leo na mara zote kumekuwa na mwanzo mzuri, lakini katikati viongozi wa klabu hiyo wamekuwa hawana mwendelezo wa wanachokianzisha.

Mwaka 2014, Simba iliingia mkataba na Kampuni ya uchoraji ramani ya Envirolink kuwapatia michoro ya hosteli na viwanja viwili katika kuendeleza mradi wa Bunju utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 2.5.

Awali, uongozi wa Rage ulitangaza ujenzi wa uwanja huo kwa gharama za Sh bilioni 74; uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000 kwamba ungesimamiwa na Kampuni ya Uturuki, GIDS, na baadaye wakatangaza kutiliana saini na Kampuni ya Petroland ya Uturuki kutafuta fedha za ujenzi mwaka 2011.

Lakini kilichofanyika Bunju hadi sasa ni ujenzi wa uwanja wa mazoezi kabla ya Desemba 2021, uongozi kuwataka mashabiki kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi.

Mangungu alitangaza ujenzi wa uwanja wa ‘Mo Simba Arena’ kuwa unatarajiwa kugharimu takriban Sh bilioni 30 ukiingiza mashabiki 30,000.

Akasema tayari Mo ameshachangia Sh bilioni 2, lakini hazihusiani na zile za uwekezaji, pia kwamba kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki kuchangia kupitia benki na simu.

Kigamboni Complex nako mmh…

Machi 25, 2020, uongozi wa Yanga uliahidi kuanza kwa ujenzi wa mradi uliopewa jina la ‘Kigamboni Sports Complex Home of Champions’ ifikapo Juni mwaka huo, hasa baada ya kipindi cha mvua kumalizika ili kuepuka usumbufu. 

Katibu Mkuu wa Kamati ya Ujenzi na Miundombinu wa Yanga, Said Mrisho alisema: “Tunataka Yanga iwe klabu ya mfano ambao unaendana na hadhi ya jina lake. Ni klabu ambayo ina historia kubwa sana nchini, kwa hiyo hata wageni wakija kuitembelea, wakutane na kitu cha kihistoria na kwenda kusimulia huko waendako.”

Alifafanua kuwa uongozi wa Yanga umejipanga kuhakikisha mradi unaanza na kuwa na kasi kubwa ili ukamilike na kwamba: “Masuala ya bajeti na wapi klabu itapata fedha, hayana tatizo.” 

Leo ni miaka miwili tangu uongozi wa Yanga ulipotoa ahadi hiyo, lakini hakuna kitu chochote kilichokamilika huko Kigamboni.

Ila sasa ni vigumu kwa mwanachama au shabiki wa Yanga kuhoji kuhusu maendeleo ya uwanja huo kwa sababu timu inafanya vizuri na kipaumbele chao ni ubingwa.

Viongozi wa Yanga wanajua timu ikifanya vibaya au wakati wa uchaguzi, basi wataulizwa kuhusu uwanja, ila timu ikifanya vizuri ni rahisi kuwa na majibu mepesi. 

Mwisho

Ramos hayupo, Salah anataka kisasi

LONDON

Uingereza

Liverpool itakuwa na kibarua kizito mbele ya Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa itakayochezwa jijini Paris mwisho wa mwezi huu.

Fainali ya Mei 28, 2022 ni marudio ya ile ya mwaka 2018, wakati Real Madrid iliposhinda 3-1 dhidi ya Liverpool na kumfanya Kocha Zinedine Zidane kuandika historia mpya ya kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Kisasi kwa Ramos asiyekuwapo

Fainali ya mwaka 2018, kwa Mohamed Salah ilimalizika mapema sana. Katika dakika 25, nyota huyo wa Misri aliwania mpira wa juu na Sergio Ramos na wawili hao walipodondoka chini kwenye nyasi za Kyiv, mkono wa Salah ulipata maumivu baada ya kuvutwa na Ramos. 

Taarifa ya kusikitisha ilifuatia baada ya madaktari kuthibisha bega lake limeteguka, hivyo nyota huyo wa Liverpool hataweza kuendelea na mchezo huo.

Katika tukio hilo wengine waliona ni ajali ya kawaida ya mchezo, lakini kwa wengine waliamini ni makusudi. Ramos aliamua kutumia ‘judo’ kutegua bega la Salah kwa lengo la kuimaliza nguvu Liverpool.

Kama ni kweli au si kweli, Liverpool ilishindwa kurudi mchezoni. Benzema akafunga bao la kwanza kwa Madrid akitumia vizuri uzembe wa kipa wa Liverpool, Loris Karius. 

Sadio Mane akasawazisha, lakini dakika nane kabla ya mchezo kumalizika, Gareth Bale alifunga bao la pili kwa Madrid kabla ya kupachika bao la tatu kutokana na uzembe mwingine wa Karius na mechi kwisha hivyo.

Lakini Liverpool bado wanakumbuka na hawajasahau. Muda mfupi baada ya kuisaidia Liverpool kufuzu fainali za mwaka huu, Salah aliulizwa na BT Sport angependa kukutana na timu gani kati ya Manchester City na Real Madrid.

Akajibu: “Kama utaniuliza mimi binafsi, ningependa kucheza dhidi ya Madrid, kwa sababu tulipoteza katika fainali tuliyocheza dhidi yao. Kwa hiyo nataka kucheza dhidi yao. Ni matumaini yangu na sisi tutashinda pia.”

Klopp, Ancelotti wasaka rekodi

Makocha Jurgen Klopp na Carlo Ancelotti wamekutana mara 10 katika mashindano mbalimbali, katika Ligi ya Mabingwa mara sita, Ligi Kuu England (3) na mara moja Kombe la FA. 

Mwitaliano akishinda michezo minne dhidi ya mitatu ya Mjerumani; wakitoka sare mara tatu.

Hii ni fainali ya nne kwa Klopp. Mara ya kwanza alifuzu akiwa na Borussia Dortmund (2013), kabla ya 2018, 2019 akiwa na  Liverpool na kumfanya kuifikia rekodi ya makocha Alex Ferguson na Marcello Lippi.

Klopp msimu huu anasaka rekodi ya kutwaa mataji manne. Tayari ameshatwaa Kombe la Carabao, kikosi chake kipo nyuma kwa pointi moja kwa vinara wa Ligi Kuu, Man City, ameshafuzu kwa fainali ya Kombe la FA pamoja na Ligi ya Mabingwa, kama watafanikiwa kutwaa mataji yote manne, itakuwa timu ya kwanza England kufanya hivyo.

Wakati Klopp akikaribia mafanikio hayo akiwa kocha, mpinzani wake Carlo Ancelotti atakuwa anasaka kuweka rekodi yake nyingine.

Mtaliano huyo anakuwa kocha wa kwanza kufuzu kwa fainali ya tano ya Ligi ya Mabingwa, endapo atashinda anaweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa mataji manne ya Ulaya akiwa mchezaji na sasa kocha.

Ancelotti tayari ameshanyakua taji la La Liga. Hili ni taji la 35 kwa Real Madrid akiwa amemuacha mbali mpinzani wake mkubwa, Barcelona, kwa tofauti ya makombe tisa.

Kocha huyo wa zamani wa Everton anakuwa kocha wa kwanza kutwaa ubingwa katika ligi tano kubwa barani Ulaya. 

Aliianza kwa kutwaa ubingwa wa Italia ‘Serie A’ akiwa na AC Milan (2004), Ufaransa  ‘Ligue 1’ akiwa Paris Saint-Germain (2013), Ligi Kuu England akiwa na Chelsea (2010), Ujerumani ‘Bundesliga’ akiwa na Bayern Munich (2017) na sasa Hispania ‘La Liga’ akiwa na Real Madrid (2022).

Ancelotti alitwaa taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa mwaka 2003, 2007 akiwa na AC Milan. Mwaka 2014, aliiongoza Real Madrid kuichapa Atletico Madrid 4-1 na kunyakua ubingwa huo.