Ndugu Rais nguzo imeanguka paa litashikiliwa na nani?

Ndugu Rais, Abdulrahman Kinana ametuacha! Anataka kupumzika. Mwanadamu
ana siku moja tu ya kupumzika. Siku Muumba wako atakayokwita ukasimame
mbele ya haki! Siku hiyo utakuwa umelala peke yako! Nawe utakuwa na
mapumziko ya milele kwenye nyumba yako ya milele! Hapa duniani pambana
na hali yako, Abdulrahman, mahali pa kupumzika hakuna!

Ukatibu Mkuu hukuuachia kwa nguvu zako mwenyewe. Tuaminio tunaamini kuwa Mungu
amekuitia kazi nyingine! Anataka uwatumikie waja wake wote katika umoja wao siyo katika vikundi vya kisiasa. Watazame waja wake, utaisikia sauti yake Yeye aliye juu! Wajengee watu wake, jukwaa litakalowaunganisha wote! Njoo Mwalimu Forum-MWAFO ufanye kazi Mungu
aliokuitia!
Ndugu Rais, Baba wa Taifa alikuwa na imani kubwa sana kwa vijana wake watatu- Kinana akiwemo pamoja na Jakaya Kikwete na Edward Lowassa. Kati ya hao ni Kinana tu ambaye hajautukuza utukufu! Hakuna timamu aliyemuita mheshimiwa. Kama ni uheshimiwa Kinana ulistahili kutokana na hadhi yako. Nchi ilikusikia ukiwataka viongozi wenzako wajivue
utukufu. lakini nani alikusikia? Wako waliowaendea wananchi wakitembea kwa magoti kuomba ajira ya Udiwani, Ubunge au Urais, na walipoajiriwa katika nafasi hizo wakaota mapembe. Wakiwarudia waajiri wao walewale wanajiita waheshimiwa hata kama kati yao wapo baba zao na mama zao. Tumekosa adabu!
Mwenyekiti ulihuzunika kumsikia Kinana akiaga. Baba usihuzunike. Umakini wa Katibu Mkuu hutegemea sana umakini wa Mwenyekiti wake kwa sababu wanasema samaki anapooza huanzia kichwani. Tangu Kinana aiweke madarakani Awamu ya Tano, amekuwa kimya! Kama alivyosema Nyerere, wenye akili walielewa.
Abdulrahman Kinana alinifikirisha sana kwa mara ya kwanza pale nilipompatia kama zawadi kitabu nilichoandika cha ‘Mwalimu Mkuu wa Watu’. Nilikitafsiri kwa Kiingereza, “The Peoples’ Schoolmaster”.
Taadhima au sifa aliyokitolea, ilifanana kabisa na ile aliyotoa Askofu Desmond Tutu mshindi wa tuzo ya Nobel wa Afrika Kusini baada ya kukisoma. Ilifanana sana na taadhima iliyotolewa na mshindi mwingine wa tuzo ya Nobel, mwandishi maarufu Ole Soyinka wa Afrika Magharibi
naye baada ya kukisoma. Hawa nilikutana nao kwa mazungumzo kila mtu kwa wakati wake tukiwa katika Tamasha la Vitabu la Afrika kule Cape Town, Afrika Kusini. Kabla ya hapo taadhima kama hiyo ilikuwa imetolewa na Mzee Sam Kivuitu ambaye sasa ni marehemu. Alikuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya tulipokutana kwa mazungumzo katika
Tamasha la Vitabu la Nairobi, Kenya.

Kinana aliniambia, “Nimekisoma mara ya kwanza. Nikarudia kwa mara ya pili. Nikakisoma tena kwa mara ya tatu. Hiki ni kitabu makini!”
Nilipompatia tasinifu (wazo linalotolewa kimantiki) ya Mwalimu Forum-
MWAFO- Jukwaa la kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali tofauti zao
hasa zinazotokana na itikadi ya vyama vyao vya siasa na badala yake
wawe na kaulimbiu moja tu, ‘Nchi yangu kwanza,’ aliiunga mkono na
akanunua kadi yake hapo hapo. Tumezungumza mengi ya nchi hii na hasa
kuhusu umuhimu wa uwepo wa Azimio la Arusha. Yawezekana huyu ni
kiongozi wa mwisho aliyebaki katika kuwatanguliza wananchi mbele kwa
nyakati hizi!
Ndugu Rais, kama walivyo tumbusi Watanzania wanatishwa kuwa watawagalagaza, watawapiga hata kuwaua na kuwafunga jela kama watawapinga kutimiza matakwa yao! Kinana usijeshangaa kusikia tumbusi wanataka kujenga pyramid kubwa kuliko za Misri ili kuongeza mapato katika utalii!  Katika kitabu cha nukuu za Kiswahili za Mwalimu
Nyerere Uk. 128-129 Nyerere alisema, “Wananchi wanapoonyesha uamuzi wa
kipumbavu, wanatumia haki yao ya kiraia. Wanaponung’unika kwa uamuzi
ambao si wa kipumbavu wanaweza wakaelekezwa mpaka wakaelewa kwanini
uamuzi ule ulifanyika, na faida zake ni nini” Na katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania uk. 65 anasema, “Kuogopwa ni sifa na ada ya madikteta, viongozi halisi hawapendi kuishiriki. Kujenga mazoea ya kutii viongozi hata katika mambo haramu, ni dalili ya woga, ni
kukaribisha udikteta.” Nenda Kinana nenda, ukatembee juu ya ardhi, uizunguke tena nchi yote ukawaondolee watu wa Mungu hofu iliojazwa katika vifua vyao. Kwanini iwe dhambi kuhoji wanaohangaika kuwashushia wananchi mbingu badala ya kuwatatulia kero zao za msingi zinazohusu elimu, afya na ustawi! Wakati kuna habari kuwa zaidi ya wanafunzi 600
wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kumkambati, Kata ya Nyamidaho, Kasulu mkoani Kigoma, wanaolazimika kusoma katika chumba kimoja kutokana na uhaba wa madarasa; huku wanasikia zaidi ya Sh bilioni 700 zimepelekwa kwenye mradi wa kutaka kuwashushia wananchi
mbingu! Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na miradi yake mizuri, lakini imekuwa ikitoza kodi mpaka kwenye vifaa vya mama zetu kujihifadhi!
Mkurugenzi Mtendaji wa Human Cherish Paids- shirika linalojishughulisha na utengenezaji wa padi, Selina Letara anasema maeneo mengi nchini wanawake wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali vya kujihifadhia ambavyo havina ubora pindi wanapokuwa katika hedhi.

Anasema, “Kuna maeneo tuliyatembelea wanawake wanatumia ugali au kinyesi cha mifugo
wengine hadi magunzi kujisitiri. Hali hii ni hatari kwa usalama wa afya zao. Hivyo padi zikiondolewa kodi zitapatikana kwa gharama ya chini na hata wale wa vijijini watazipata.”
Nenda Abdulrahman Kinana nenda, lakini ujue utakumbukwa na wengi wakiwamo mawaziri mizigo! Uliuacha mkate wa siagi nyumbani kwako, ukaenda kushiriki kula matembele na masikini katika vijiji vyao nchi nzima, ili ukijibie chama chako maswali kutoka kwa wananchi.
Wanaofaidi kivuli leo, cha mti uliopanda wamejipumbaza wasijue kuwa usione vyaelea, vimeundwa! Huko uendako Kinana utukumbuke na sisi wazee vikongwe wastaafu wa iliyokuwa TTCL kwa pensheni yetu ya Sh 50,000 kwa mwezi! Wanaofaidi kivuli cha mti tulioupanda wanatuona sisi sasa ni malapulapu ya nchi hii! Siku hazigandi, lakini wabarikiwe sana! Lakini ah! Kinana, nenda watu wapate njia! Wewe ndiye uliyekuwa kizingiti kikubwa katika njia ya wapinzani kila walipokuwa tayari kuingia Ikulu!