Ndugu Rais nionyeshe hata ukurasa mmoja usio na makosa…

Ndugu Rais Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi alitupiwa kitabu cha Kingereza kilichochapwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) mezani pake kisha akaulizwa; “Nionyeshe hata ukurasa mmoja tu ambao hauna makosa katika kitabu hiki”.
Kitabu hicho na vingine ambavyo sasa vinafananishwa na sumu wanayolishwa watoto wa masikini huko shuleni baada ya kusambazwa na Wizara ya Elimu, vimechapwa na TET, badala ya kuchapishwa!
Kitabu kilijaa makosa ya kila aina! Ilichofanya  TET, kwa vitabu hivi ni kuvichapa badala ya kuvichapisha!


Ndugu Rais uchapishaji kama ulivyo uandishi wa vitabu ni sanaa. Ni kipaji ambacho mhusika huzaliwa nacho. Akienda shule au katika mafunzo, huenda kuboresha tu kile ambacho tayari kipo ndani yake.
Inasikitisha kutambua kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Katibu Mkuu wake wameifanya wizara ionekane ni maamuma kiasi cha kushindwa kupambanua na kutofautisha kati ya viambata vya elimu na elimu yenyewe. Waziri na Katibu Mkuu wake wanashindwa kujua kuwa wako watu wengi sana ambao wanaweza wakajenga madarasa mazuri sana, wakatengeneza madawati mazuri sana hata wakazijaza shule zetu na chaki, madaftari na hata vifaa vya maabara na vya kufundishia. Hivyo vyote vinamsaidia mtoto kupata elimu angalau katika mazingira bora.
Lakini hivyo vyote siyo elimu. Elimu yenyewe iko kitabuni! Waziri wa Elimu na Katibu Mkuu wake wanapaswa kuelewa kuwa ni watu wachache sana wenye kipaji cha kuandika vitabu vinavyotoa elimu.
Ndugu Rais ni jambo la kusikitisha sana kuona wizara ya elimu inakusanya watu tu wa hivi hivi na kuwagharimia kuanzia katika hoteli, warsha, semina na malipo ya marupurupu mengine eti waandike vitabu. Wanawataka waandike vitabu vya watoto wakati kuna vitabu vingi sana vya watoto kwa wachapishaji ambavyo vimeidhinishwa na wizara hiyo hiyo!


Baba, kinachotawala hapa ni ubinafsi na tamaa ya fedhanyingi. Ndivyo vilivyosababisha mpaka kukamilika kwa dhambi hii kubwa!
Wizara ya Elimu kwa kuitumia Taasisi ya Elimu Tanzania wameng’ang’ania kazi ya uchapishaji ambayo hawana ujuzi nayo! Vigezo vilivyotumika kuwateua waandishi hao eti baadhi yao ni walimu au wana digrii wengine mpaka PhD. Matokeo yake wanaishia kuandika yanayofanana na yale walioandika ili kupata digrii zao (dissertation au thesis) na siyo maandiko ya kumsaidia mtoto kupata elimu kutoka katika vitabu hivyo kwani mwishowe vilichapwa tu. Havikuchapishwa! Kwa kusukumwa na maslahi binafsi watu dhaifu wako tayari kuliangamiza Taifa hili kwa kuifuta elimu!
Naibu Katibu Mkuu alikiri udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na TET katika kuandika hadi kuchapa vitabu hivyo na kwa unyofu aliwaambia wachapishaji wa vitabu akasema;  “Nitawaiteni, niwaunganishe na TET walioandaa vitabu hivi ili tuongee kwa pamoja. Hawa (Taasisi ya Elimu Tanzania) wameitia aibu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi!”


Ndugu Rais, tuliokulia vijijini tukitumia muda mwingi porini machungani, tukichunga ng’ombe au mbuzi, tulisisitiziwa na wazazi wetu kuwa mara tu unapogongwa (kuumwa) na nyoka, kitu cha kwanza ni kuchana zaidi jeraha aliloliacha ili damu nyingi itoke kwa maana itakuwa inatoka pamoja na sumu iliyoachwa na nyoka. Hatua ya kwanza na ya muhimu sana ni kuitoa sumu mwilini haraka iwezekanavyo! Kama uchunguzi ni baadaye! Ikiachwa iendelee kusambaa katika mwili na itakapoufikia moyo muathirika anapoteza maisha.
Ndugu Rais masikini na wanyonge wa nchi hii wanakuomba kwanza kabisa, uwaondolee watoto wao sumu hii iliyo katika mfano wa vitabu kule shuleni. Hivi tuandikavyo, watoto shuleni wanazidi kuathiriwa na sumu iliyomo katika vitabu hivi! Ikiachwa iendelee kusambaa Taifa kielimu litaangamia! Ondoa vitabu hivi shuleni kwanza baba! Tambua kuwa hakuna namna unaweza kuvihifadhi vitabu hivi. Ni sumu, jambo moja tu na moja pekee unaweza kuvifanya ni KUVICHOMA MOTO!
Ilisikitisha kumsikia Naibu Katibu Mkuu akisema watavisahihisha. Pole sana! Viko shuleni unavisahihishaje? Huku ni kukiri umaamuma katika taaluma ya uchapishaji! Baba, dakika ya mwisho ambayo mchapishaji anaweza kuitumia kusahihisha chochote katika kitabu ni ile anayoitumia kumkabidhi kazi hiyo, mchapaji. Na hapo hicho hakijawa kitabu.


Wanaita ‘camera ready copies’. Zikishapita katika mitambo ya mchapaji (printer) zinakuwa kitabu. Hapo hakuna kinachoweza kuongezwa, kupunguzwa au kusahihishwa katika kitabu hicho! Baba, yeyote atakayekwambia watavisahihisha ni maamuma ambaye hajui asemalo. Hakuna mwanadamu chini ya mbingu hii anayeweza kusahihisha kitabu kilichokwishachapwa! Anaweza kuandika kitabu kingine akiyakwepa makosa yaliyo katika kitabu kibovu. Lakini huko ni kuandika kitabu kipya.
Watakuja maamuma wengine, watakwambia sasa tukiviondoa watoto watakaa hivi hivi? Hao usiwajibu kwa maana maandiko yanasema; “Usimjibu mpumbavu kulingana na upumbavu wake, usije ukafanana naye!” Waulize, wakiwa hawana chakula cha kuwapa watoto wao, je, wao wako tayari kuwapa sumu?
Baba, kuna vitabu vingi ambavyo wachapishaji binafsi wanavyo. Vitabu ambavyo vimethibitishwa na wizara hiyo hiyo ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuwa vinafaa kutumika shuleni. Kama lengo ni maslahi ya Taifa, wanashindwa nini kuvitumia vitabu hivi?
Ndugu Rais, waziri amesema hawezi kuomba radhi kwa makosa ya watu wengine. Kama jina lake linaonyesha kuwa ni mkristu, basi si muumini wa kweli! Mbona Yesu Kristu aliteswa mpaka akasulubiwa kwa kifo cha msalaba kwa sababu ya dhambi za watu wengine? Waziri aelewe kuwa hao anaowaita wengine ndiyo hao baba uliompa ili awaongoze na kuhakikisha hawatendi uovu kama huu ambao wameutenda. Amethibitisha kuwa alishindwa kuwasimamia na kama kuwaongoza amewaongoza kuutenda uovu huu!
Ndugu Rais, katika hali kama hii hakuna mwingine anayeweza kuviondoa vitabu-sumu hivi shuleni, isipokuwa wewe! Waziri hawezi na hata Katibu Mkuu wake. Hawawezi kwa sababu ni mamlaka zao ulizowapa ndizo walizitumia vibaya na wao ndiyo waliovipeleka vitabu-sumu hivi katika shule zetu vikawaathiri watoto wa masikini kwa manufaa yao! Baba waite viongozi wa wachapishaji watakujuza mengi zaidi!