Ndugu Rais siku ya kumuaga Akwilina ilikuwa nzito

Ndugu Rais, sijui niilaumu nafsi yangu au nimlaumu Mwenyezi Mungu aliyenifanya niishuhudie
siku ya Alhamisi tarehe 22/2/2018 pale Chuo cha Usafirishaji, siku ambayo mwili wa Akwilina
ulipokuwa unaagwa.
Yaliyonigusa moyoni naapa hayatakuja kunitoka katika kifua changu siku zote zilizobakia katika
maisha yangu, baba nchi imepinda! Ni nani asimame ainyooshe? Hakika siku hiyo ilikuwa ni
siku ya kihoro!
Nilishindwa kwenda kumwangalia pale alipolala katika jeneza lake kuogopa ningemwangukia!
Ndugu Rais, siku alipofariki mama yangu mzazi mbele ya macho yangu nilidhani ndiyo ilikuwa
siku yangu ya mwisho kushuhudia maumivu makali katika moyo wangu kwa siku zangu hizi
chache nilizobakisha kabla ya kurudi kwa Baba. Kumbe haikuwa hivyo.
Alhamisi ya tarehe 21/2/2018 mambo yalikuwa magumu sana kwangu. Siku hiyo nilikwenda
kushiriki katika ibada ya kuuaga mwili wa Akwilina Akwilini iliyofanyika pale Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji.
Laiti baba ungekuwapo siku hiyo, nina hakika kwa huruma yako ungewaza mara mbilimbili jinsi
unavyowatumikia watu wako. Kilichoshangaza wengi msiba ule uligeuzwa na kuwa wa kitaifa.
Kila gari lilipekuliwa, ulinzi ulikuwa mkali.
Baba, umati nilioukuta ulikuwa mkubwa kama ule tuliozoea kuuona Karimjee kwenye misiba ya
kitaifa. Huu haukuwa msiba wa kitaifa lakini walikuwako mawaziri na viongozi wengine wa
kitaifa. Ni wangapi katika ule umati mkubwa walimjua Akwilina kabla ya kifo chake? Mtoto
mdogo yule alifanya kitu gani kikubwa mpaka azikwe na viongozi wa kitaifa?
Ala! Kumbe! Kilichovuta ule umati ni jinsi alivyouawa kinyama. Risasi ilipigwa ndani ya daladala
na kumuua binti mwema ambaye hakuwa na hatia yoyote masikini!
Katibu mmoja alisikika akisema; “Tulipata habari kuwa wengine walikuwa wamepakiwa ndani ya
madaladala!” Je, ni kwamba ilipangwa?
Kama maneno ya mzee Mwinyi, Rais mstaafu, kuwa tuishivyo ni sawa na kitabu
kinachoandikwa ni sawasawa, basi kitabu cha awamu ya tano kitawatoa machozi wasomaji
wengi!
Ndugu Rais, baada ya viongozi mbalimbali kutoa salamu zao alisimama Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia. Alipoanza tu kuzungumza kiliibuka kikundi cha vijana tisa kikiwa na
mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Mojawapo lilisomeka; ‘Tumechoshwa kuuliwa,’ Jingine
likasomeka, ‘Mwigulu na Siro kwa mauaji haya bado mpo ofisini?’ Jingine lilikuwa na mantiki
kubwa zaidi lilisomeka, ‘Wauaji hawawezi
kujichunguza’.
Nikamkumbuka mwanamwema Waziri wetu Mkuu, Kassim
Majaliwa, kwa busara zake kuamuru wenye mabango wasibughudhiwe.
Nilitegemea Ndalichako angeiga mfano mwema wa bosi wake, Waziri Mkuu, ayachukue aende

nayo akayafanyie kazi. Pamoja na yote hayo, Ndalichako aliendelea kusema; Rais
ameshtushwa sana na tukio hilo. Sikuelewa alikuwa na maana gani. Ukitupiwa nyoka wa
plastiki utashtuka tu lakini hilo haliwezi kukuumiza moyoni.
Ndugu Rais, baadaye niliambiwa kuwa Waziri Ndalichako alikuwa anaiwakilisha Serikali.
Alikuwa anaiwakilisha Serikali kwa sababu Akwilina alikuwa ni mwanafunzi? Tangu Serikali hii
imekuwa madarakani Akwilina ndiye mwanafunzi wa kwanza kufa?
Ni mara ngapi Waziri Ndalichako ameiwakilisha Serikali kwenye msiba wa mwanafunzi? Mara
ya kwanza nilisikia amepeleka ubani wa shilingi milioni moja kwenye msiba. Lakini kwanini
Serikali igharamie msiba wa Akwilina?
Ala! Kumbe! Shida hapa siyo kifo cha Akwilina, ni namna kifo hicho kilivyotokea! Kama Akwilina
angekufa kutokana na kuanguka kutoka juu ya mti Serikali ingegharamia mazishi hayo? Ala!
Kumbe ilikuwa ni namna fulani ya kupulizia kama panya afanyavyo!
Wanaotuhumiwa kwa mauaji haya ni polisi. Polisi ni mkono wa Serikali. Chochote
kinachotendwa na mkono wa mtu, kinatendwa na mtu mwenyewe mwenye mkono. Iweje sasa
watuhumiwa wa mauaji wakabidhiwe jukumu la kujichunguza?
Hii hata kwa mtu asiyejua mambo hawezi kukubaliana nalo. Sasa tunaanza kusikia labda
kulikuwa na gobore. Marehemu mama yangu aliniambia, “Mwizi hujishika mwenyewe.”
Ndugu Rais, ni vema na haki tena ni vizuri sana tumshukuru Mungu kwa kumtuma mtumishi
wake Padri Raymond Manyanga, Paroko msaidizi katika Parokia ya Yohane Mbatizaji iliyoko
Kigogo Luhanga, kuja kuendesha misa ya mwisho ya Akwilina.
Mahubiri yake hayakuwa na chembe ya unafiki. Aliongea bila kumung’unya maneno ili
kumfanya kila mwenye masikio ya kusikia asikie. “Kama tusipopatana tutakubali kwamba sisi
wote ni watoto wa Mungu tutamalizana. Hakuna namna tutakavyoweza kuishi pamoja bila
kupatana. Naomba tuwe wapatanishi na si wagombanishi. Mtu wa kutuunganisha ni Serikali
pekee.”
Alisema, “Mimi si hakimu na sitaki kuhukumu, wale wenye nafasi na hasa vyombo
vinavyohusika vifanye uchunguzi; vikimaliza taratibu zake kama ni kupitia televisheni ama nini,
huyu mtu aliombe Taifa msamaha vinginevyo hatutafika mbali. Leo ni Akwilina, huenda kesho ni
mwingine.”
Padri Raymond anasema amesikia na kuona kwenye vyombo vya habari kuwa Akwilina aliuawa
kwa kupigwa risasi huku akiona taarifa za namna ukweli wa tukio hilo unavyopindishwa.
Alisema, “Wote tumesikia na hata mimi nimesikia kuwa Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi,
mimi sitaki kuhukumu lakini nimeona kama kuna namna ya kutaka kulipindisha jambo hili
naviomba vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi kwa kina, kwani kama ni risasi haiwezi
kuwa imekwenda yenyewe kwa mtu, yupo aliyepiga na aliyefanya hivyo atakuwa na akili
timamu, hivyo tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na mambo kama haya.”
Alisema mauaji hayo ni dalili kwamba mambo hayajakaa sawa hapa nchini, hivyo Watanzania
wanapaswa kumwomba Mungu ili amani iliyopo isivurugwe.
Akaendelea kusema, “Tena hapa naomba kusema bila kupepesa macho, wenye jukumu la
kufuatilia jambo hili ni Serikali nawaomba watusaidie kwani ndiyo waliopewa dhamana ya
kutulinda. Pia Serikali itambue kuwa watu wake wapo kama vidole vitano vilivyopo mkononi,
havilingani, ndivyo hivyo kwa raia wake, wapo wembamba, wanene, wafupi lakini wote ni watu
wao.”
Ndugu Rais, kilichoonesha hasira kubwa iliyowajaa Watanzania katika vifua vyao, ni pale
ambapo kila neno alilolisema Baba Padri lilishangiliwa sana na umati wote! Sasa maaskofu

wote waliungana pamoja na wametoa kauli nzito. Nayo yaonekana imepamia mwamba!
Wanaokemea sasa ni Wakatoliki. Madhehebu mengine na dini nyingine mbona wamekaa
kimya? Waumini wao wanatetewa na nani? Mwogopeni anayeweza kuua roho!
PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713 33 42 39