Ndugu Rais, tumtangulize Muumba wetu kwa kuwashukuru wachungaji na mapadri wa Dodoma ambao kwa wakati wote wamekuwa wakiniombea uzima wawapo katika sala zao! Nimeisikia sauti yenu na baba yenu wa mbinguni anazipokea sala zenu.

Mwenyezi awabariki ili siku moja mje muishuhudie tena amani ya kweli katika nchi yenu hii mliyopewa na Muumba wenu kwa neema tu! Nchi yenye upendo, umoja na mshikamano wa kweli. Bila kumwomba, Mungu amewajalia Watanzania utajiri mwingi juu na chini ya ardhi. Mito inayotiririsha vyote; maji na samaki watamu.

Chemchemi za maji ya baridi zinazoipoza nchi huku zile za maji yachemkayo zikionyesha utukufu wake aliyezifanya ziwe. Nchi ya mlima mrefu wa pili katika dunia yote na mabonde yaliyojaa miti iliyosheheni matawi ya kijani na ndege wazuri, waimbao juu yake na wasokotao viota vyao. Akaipangilia majira yaliyo bora ya mvua za masika na za vuli na wakati wa kiangazi. Wana wa nchi, wanalima na kuvuna mazao ya nchi!

Ndugu Rais, meza ya maridhiano ni muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote. Nchi yangu kwanza! Malumbano hayajengi. Nchi ni yetu wote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu katika umoja wetu.  Achaneni na tofauti zenu za kisiasa. Vyama vya siasa huja na kupita lakini nchi inabaki, visiwagawe. Kuweni wamoja muilinde amani ya nchi yenu. Asiyetaka maridhiano kabla ya Uchaguzi Mkuu, hawafai! Awe ni mwenyekiti, diwani, mbunge au yeyote yule, amekengeuka! Muogopeni mtu huyo. Mkataeni kama mlivyoapa kumkataa shetani. Uchaguzi utakapojiri msimpatie kura zenu, Mungu wa Ibrahim atawapigania dhidi yake!

Hali tuliyomo inaamsha simanzi katika vifua vyetu na kuashiria kuwa tunaelekea katika majuto ya dhiki kuu! Furaha katika nchi imekwisha kupotea! Kuipata tena ni vigumu. Simanzi nzito itakapokuwa imeielemea mioyo yetu inaweza kutusukuma kumkufuru Muumba wetu kwa kutupatia baadhi ya wenzetu. Katika nchi hii hakuna mwenye haki zaidi ya wengine. Rais wetu, ndiye baba wa wote hata tulioona jua kabla, hivyo atende haki sawa kwa wote.

Kumekuwako na kelele nyingi kwa kila kinachofanyika eti viongozi wamevunja rekodi hata kwa miradi ambayo hawakuibuni wao bali wameikuta ikitekelezwa. Wanaoamini kuwa anaweza akatokea kiongozi mwenyeheri kama Nyerere, mawazo yao yaheshimiwe. Lakini lazima watambue kuwa utakatifu wa mtu huonekana mwishoni si sasa anapoanza.

Baba tutengenezee meza ya maridhiano. Busara ni kupatana na kamwe si kupambana. Watoweni katika hofu watu wa Mungu ili wapate kuishi kwa amani, furaha na ustawi katika nchi yao hii njema waliyojaliwa na Mola wao! Tunaweza kuwa na nia njema kwa haya tunayoyafanya lakini tuutazame utendaji kazi wetu!

Tumepanua pengo la kuasimiana kwa kiasi kikubwa na tunatengeneza kesho yetu iliyojaa visasi! Watawala wetu wengi wa sasa kuhubiri upendo kwao imekuwa ni kama mwiko. Kutisha na kutishana umekuwa ndiyo mwendo wetu wa kila siku. Wamejaa hofu na wasiwasi hata kwa hatari isiyokuwapo. Ni vema wakaelewa kuwa Watanzania hawakulelewa hivyo! Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwalea Watanzania katika upendo, umoja na mshikamano. Hivyo wamezoea undugu badala ya ubabe, kutukanana na kufokeana kwa kila jambo! Watanzania wanachokihitaji sasa ni kiongozi wa kuwaunganisha ili kwa pamoja waijenge nchi yao! Tofauti na hilo tunajenga nyumba yetu juu ya mchanga!

Tumepokea wageni wengi lakini Rais wa DR Congo, Felix Tshisekedi, alituletea ujumbe muhimu wa kipekee. Alisema: “Januari 24, mwaka huu, kulitokea jambo kubwa sana katika nchi yetu. Mimi nikiwa mpinzani tulipokezana madaraka ya kuongoza nchi yetu na Rais Joseph Kabila aliyekuwa madarakani, kwa amani kabisa.”

Watanzania wengi walitarajia ujio wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ungekuwa ni mfano wa kulisisitiza hilo, kuwa angekueleza mbinu alizotumia katika meza yake ya maridhiano kufikia amani ya kweli na aliyekuwa hasimu wake mkubwa, Raila Odinga. Wakadhani amekuja kutupa somo na sisi tubadilike. Mwanafalsafa wa kale anayeheshimika sana hapa duniani, Plato, alisema: “Kuna watu wawili tu wasioweza kubadili mawazo yao. Mpumbavu kuliko wote na mwenye hekima kuliko wote.” Tusione aibu kufikiri mara mbili.

Tunaendelea kusisitiza; Ole wake mtu yule aliyeliua Azimio la Arusha. Hukumu yake itabaki juu ya kichwa chake katika siku zake zote. Ndani ya Azimio la Arusha tuliishi kwa amani, upendo, umoja na mshikamano. Huyu ndiye chanzo cha magumu yote yanayowasibu Watanzania leo. Nani angeihitaji meza ya maridhiano leo?

Mzee wetu, Ali Hassan Mwinyi, apumzike kwa amani. Hana tena wakati wa kuchekelea. Aliposema maendeleo yanayofanyika nchini hivi sasa ni maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu, Watanzania wengi walidhani anayakiri maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliyesema: “Wakati tumechukua uongozi wa nchi hii, tulifanya ujinga. Tuliitazama ‘Europe’ Ulaya, tukaona inameremeta kwa madege yao. Tulipoitazama ‘North’ Amerika na matreni yao tukaona ina -‘glitter’, inawaka! Tukadhani yale ndiyo maendeleo. Kumbe yalikuwa maendeleo ya vitu. Maendeleo ya kweli yanapaswa kuwa ya watu.”

Ndugu Rais, Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi hii, ndiye muasisi wa taifa hili la Tanganyika na baadaye Tanzania. Ndiye Baba yetu wa Taifa. Leo Ulimwengu unamtambua kuwa ni Mwenyeheri. Kwa kutambua hekima na busara zake kuu, na hasa uchaji wake wa kweli kwa Mwenyezi Mungu, Kanisa Katoliki na ulimwengu kwa jumla wanafanya mchakato Baba Mtakatifu amtangaze kuwa ni ‘Mtakatifu’. Mtu huyu wa Mungu anawatangazia Watanzania na dunia yote kuwa walipoanza kuiongoza nchi na kuhusudu maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu, walifanya ujinga!

Tuyarejee maandiko katika kitabu cha The People’s Schoolmaster kuwa: “Kupanda mlima mkali kunahitaji kuanza na hatua za polepole. Njia yetu ya maisha sasa ni mwinuko mkali. Tukilielekezea jua macho yetu kamwe hatutaona kivuli. Hivyo lazima tuweke fikra zetu katika urari. Jana yetu imekwisha kupita, hivyo ni kesho yetu ndiyo inatuita kwa ishara. Hatuwezi kuibadili jana yetu lakini tunaweza kuiboresha kesho yetu. Tuiangalie kesho yetu kwa sababu huko ndiko tutakapomalizia maisha yetu.’’

By Jamhuri