Ndugu Rais, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa muadilifu wa hali ya juu, mwenye hofu ya Mungu na tena kionambali.

Wanasema bahati haiji mara mbili, hivyo tukubali tumepoteza kito cha thamani kubwa sasa ndiyo fahamu zinatujia! Tumekuwa ‘yamleka zipita

nga masala yawazana.’ Watu wanaopata akili baada ya mambo kuharibika.

Baba wa Taifa alisema, “Paolo, Paolo, Paolo, na nyinyi wengine, mkilifuta kabisa kabisa Azimio la Arusha mtakuja kupata taabu sana baadaye!” Baadaye yetu aliyoiona Baba wa Taifa itakapofika, itakuwa chungu tena ya kutisha.

Tutachukiana wenyewe kwa wenyewe, tutatekana na kutesana lakini huo hautakuwa mwisho! Wakongo, Wanyarwanda, Warundi na wengine hawakuzaliwa wakipigana. Walisukumwa na viongozi wao waliokosa busara wakaendekeza ubinafsi.

Isipochukuliwa tahadhari sasa haitashangaza na sisi siku moja tukajikuta tunapigana ‘masasi’ (risasi) wenyewe kwa wenyewe kama wanavyopigana wenzetu hao!

Ndugu Rais, ukweli ni kwamba Katiba mpya siyo mwarobaini wa matatizo yaliyopo. Wapinzani wanaodai Katiba mpya huku na wenyewe wakiwa wamejivika utukufu na kujiita waheshimiwa, wanatofauti gani na hawa waliopo? Mheshimiwa hawezi kuwa mtetezi wa masikini hata siku moja.

Hawa hawamlilii mwananchi yeyote, wanalilia utukufu zaidi na wala siyo maslahi ya nchi wala wananchi. Kudai Katiba mpya wakati huu wa watu wasiojulikana huku akina Grace wakitamba kwa kupewa jeuri zaidi, ni sawa na kuitakia nchi majanga makubwa zaidi.

Mnaweza mkajikuta mnaibuka na Katiba inayohalalisha uongozi wa maisha!

Ndugu Rais, siasa ni kazi sawa na kazi nyingine. Mwanasiasa halisi lazima atakuwa na malengo ya kuwa mwanasiasa mkubwa kabisa katika nchi. Akigombea udiwani akapata atataka ubunge, akipata ubunge lazima atataka urais. Yote hayo, hayafanyi kwa ajili ya watu wengine bali kwa faida yake mwenyewe!

Hakuna timamu anayetafuta udiwani au ubunge ili awasaidie wananchi. Vivyo hivyo kila anayeusaka urais, anausaka kwa faida yake mwenyewe. Huyu ndiye mwanasiasa aliyekamilika. Mwanasiasa aliyekomaa akishindwa kupata udiwani, ubunge au urais katika chama chake akihamia chama kingine anatafuta nafasi ileile aliyoikosa kwenye chama alichohama.

Wanaojiuzulu udiwani au ubunge katika vyama vyao na kujiunga na vyama vingine na kisha kugombea nafasi zilezile walizojiuzulu, hao ni chupa zinazofanana na almasi. Wanaowapokea Baba wa Taifa aliwafananisha na mazuzu.

Alisema bila kujua kama wameachiwa chupa, wanabaki wanachekelea kama zuzu!” Hawa ni mabati yaliyoshika kutu ambayo timamu hawezi kuezekea nyumba yake hata kama atapewa bure. Ukiona mtu ananunua bati lenye kutu jua yeye mwenyewe ni kutu zaidi.

Ndugu Rais, Baba wa Taifa alipoasisi makao makuu ya nchi yahamie Dodoma alitangulia kuliasisi Azimio la Arusha. Nawe kama uliyetumwa na Mungu umechomoza kutaka kutimiliza matakwa ya Mwalimu Nyerere lakini kipi kianze?

Tumwongezee damu majeruhi aliyeishiwa damu au tumtibu kwanza mguu wake uliovunjika?  Ukombozi wa masikini mnyonge wa Tanzania uko katika ujenzi wa Dodoma au katika kulirejesha Azimio la Arusha?

Alah, kumbe! Azimio lingewainua masikini walioinama na kuwainamisha waliojiinua kwa kupanda migongo ya wanyonge. Tukisema kama kweli tunawahurumia masikini lakini tunatenda tofauti.

Baba tuambie, kama siyo wewe, masikini wa nchi hii wamngojee nani mwingine wa kuja kuwarudishia ukombozi wao Azimio la Arusha? 

Kama Azimio la Arusha lingekuwapo mpaka leo mapito wanayopitia Watanzania leo yasingekuwa machungu kiasi hiki. Tutafanya mengi sana, lakini hata tukiisawazisha milima yote ya nchi hii na nchi yote ikawa tambarare kama kiwanja cha kuchezea mpira, nchi haitanyooka, bali itakuwa ni kuwapa fursa ya kusikilizwa wale ambao kwa muda wote wamekuwa wakisema tunapuyanga tu! Ni kipi rahisi kutamka; kuwa tuhamie Dodoma au tunalirejesha Azimio la Arusha?

 

Ndugu Rais, nafasi tulizoachiwa za kusemea ni ndogo hivyo inatubidi yote tunayotaka kusema tuyasemee hapahapa. Ndugu Edward Ngoyai Lowassa kuonekana akicheka na Rais wake Ikulu imekuwa nongwa. Baba amesema ni Edward ndiye aliyeomba faragha ya kukutana naye.

Wote tunajua anachotafuta Edward katika nchi hii ni urais siyo kitu kingine. Asingeweza kwenda Ikulu kumwomba baba amwachie urais. Sasa tujiulize, aliomba kukutana na Rais ili amwombe nini? Ndipo nikayakumbuka maneno ya busara ya mzee Madiba Nelson Mandela aliposema, “Ukitaka kumshinda adui yako mfanye awe rafiki yako.”

Alah, kumbe! Edward alienda Ikulu kuomba urafiki na mkuu wa nchi, kuna ubaya gani? Zipo njia mbili za kupambana. Kutumia mtutu wa bunduki au kujadiliana. Chuki, hasira na woga kamwe haviwezi kuinyoosha nchi.

Viongozi wetu hawa wawili kukutana na kuzungumza, huku wakicheka, wametuonesha busara kubwa sana. Mapigano yanayoendelea katika nchi mbalimbali hasa za Afrika ni kutokana na viongozi kukosa busara.

Wanaodhani bunduki inaweza kulinda amani wana upeo mdogo!

Sasa wamejitengenezea visasi vya kudumu!

Edward ameamua kuitafuta amani ya kweli kwa njia ya mazungumzo. Amefungua njia ya majadiliano. Wanaojiona ni viongozi wetu wa kweli ni busara wakaitumia njia hiyo.

Hekima na busara si kila mtu anavyo. Kumwona mpinzani wako kisiasa ni adui au kusema haikupendeza kwa sababu tunauguza, ni mawazo ya mtu aliyekwishachoka kifikra. Alichokifanya Edward hakiwezi kumchanganya timamu yeyote. Kuwa alitakiwa amwambie kwanza Mwenyekiti wake ni upofu tu katika kufikiri.

Edward kama Edward ni sawa na Mtanzania mwingine yeyote mwenye haki ya kuonana na rais wake kila anapojaaliwa! Maneno waliyoyatoa wote wawili yalihaririwa na wahariri wa Ikulu.

Baba amesema Edward alimwambia mengi. Na mimi nitakapojaaliwa kukutana na baba nitamwambia mengi zaidi. Unategemea hakumuuliza kwanini amemzuia asifanye mikutano ya kuwashukuru mamilioni ya wananchi waliompa kura wakati yeye baba anafanya?

Hakumuuliza kwanini wananchi wanatekwa na kuteswa kinyama wakati Serikali ipo? Kwanini watu wanapotea na wengine kushambuliwa kwa bunduki? Mlitegemea majibu aliyompa yatangazwe? Edward ameenda kuitafuta amani hasa kwa watu wake wanaoonekana kuwa wahanga wa uovu huu!

Kumwambia elimu bure kunahitaji ujasiri gani? Hata hivyo, Edward hakuna elimu bure. Pesa zinazotumika ni kodi ya wazazi wao! Tusiwapotoshe wananchi! Wanasema umenunuliwa, kama wanawema wanavyoambiwa umewanunua kila wanapotaja jina lako kwa nia njema!

PASCHALLY MAYEGA

SIMU:    0713334239

By Jamhuri