Ndugu Rais, kwa kuwapenda watu wako, uliwatahadharisha viongozi wao kuwa watambue ya kwamba Watanzania si wajinga. Wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ na kuchambua mambo. Wakinyamazia jambo kubwa wajue mioyo yao haiko, ‘clear’. Ndugu yetu Harrison Mwakyembe Waziri wetu aliwahi kuliambia Bunge kuwa wananchi siyo mabwege. Kwa sasa katika mitandao ya kijamii na hasa kule bungeni kauli hizi zimetamalaki. Haijulikani wanaozitamka wanathibitisha vipi kuwa na wao si wajinga! Wanapotenda kazi zao wanachukua tahadhari zipi ili wananchi nao wasije wakawadhania kuwa ni mabwege?

Wananchi wanakumbuka jinsi Spika alivyolitukuza kidhaifu neno udhaifu.

Akaagiza kutofanya kazi na CAG. Lilipotumbuka akasema hatutafanya kazi na Mussa Assad. Akawa tayari amepoteza mwelekeo. Aibu kubwa ikalifunika Bunge. Wabunge watiifu wakapoteza heshima zao katika jamii. Alipozusha la Steven Masele, wakamwambia akae pembeni ili haki itendeke, akawa mbogo. Mtoa utaratibu ana bahati, bungeni hakuna magongo. Masele akamsoma mzee amepindia wapi, akampelekea mpira huko huko akimghilibu kuwa anataka kuomba radhi. Jamaa kusikia ataombwa radhi, akavunja utaratibu na akaingia, Masele hakukosea!

Akapiga pale pale utosini. Aliposhtuka, oh, alisema anaomba radhi mbona anasema na mengine? Masele anatoka kuokota mpira kwenye nyavu! Huyu ni Naibu Rais wa Bunge la Afrika. Haukupita muda ikasikika yowe kubwa, “Acha, acha kabisa. Mnamzeesha Rais, Rais ana kazi nyingi sana’’. Kwakuwa si mabwege, wananchi wakawa wameishajua ukweli. Ndugu Bashiru Ally mpike huyu kijana aje awe spika wetu bora ajaye!

Spika Ndugai aliwahi kuliambia Bunge kuwa baadhi ya maprofesa wanatuona tusio maprofesa kama mbuzi tu. Baadhi ya maprofesa wameamua kutuonyesha umbuzi wetu. Wameshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge kutumia muda wa Bunge la bajeti kushughulika na watu badala ya mambo ya msingi. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala aliliambia gazeti moja ya kwamba, hamuelewi na anamshangaa Spika Ndugai kwa sababu anaonekana ni mtu mwenye jazba kila mara…“Nasema Spika wetu wa sasa nadhani tuna matatizo naye. Mara nyingi yuko kwenye malumbano, aidha na wabunge wenzake au na watu wa serikali. Jazba, jazba, jazba mimi sielewi’’. Wabunge watiifu Profesa anawauliza, “Vifungo vya Lema na Mdee waliounga mkono kauli njema ya CAG, hivi sasa vina uhalali gani?’’ Nyerere alisema, ‘mnaonekana wote, ni wale wale!’.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, Askofu Dk. Fredrick Shoo akimuonya Spika katika ibada ya misa kumzika mzee Regnald Mengi alisema, “Ndugai, leo uko hapa, nasema mnapokaa bungeni na kuamua mambo mtende haki na mfanye maamuzi [uamuzi] yenye maslahi kwa wananchi.’’ Wale waliposhangilia Bunge kutiwa aibu, Masele naye alishangilia japo kwa dhamira tofauti.

Nape Mnauye anapozililia korosho na jimbo lake, bungeni wananchi wa kawaida ambao ndiyo wangelia pamoja naye, hawawezi tena. Aliwadhulumu haki yao ya kuliona ‘Bunge live’. Aache kulia awaombe kwanza wananchi radhi. Wabunge watiifu wajiulize Nape alikuwa nani? Hakujua kama kuna kesho. Analia kilio cha samaki, machozi yake yanaenda na maji.

Baba, kupasua kioo hakuondoi matongotongo tuliyonayo usoni. Kazi ya kioo ni kutuonyesha matongotongo tuliyonayo usoni. Wapinzani ndiyo kioo chetu. Kuwadhibiti kwa kila hali ni sawa na kukipasua kioo bila kujua kuwa tunafanya hivyo kwa hasara yetu wenyewe! Walitushauri tusiende Mtwara mikono mitupu. Hadi leo katika vyama 11 peke yake kuna wakulima 1,281 ambao korosho zao zilichukuliwa na kuhakikiwa na serikali, lakini sasa inapoelekea miezi minane wapo ambao hawajalipwa. Simanzi tulioliachia Taifa kule Mtwara ni nzito mno nayo itatugharimu pa kubwa huko tuendako! Wahusika wangewajibishwa, lakini hata kukemewa tu hawajakemewa. Jenerali Ulimwengu amekaririwa akisema aliyeivuruga biashara ya korosho ni mhujumu uchumi.

Wakashauri tusiende Mbeya bila kuwa na nyongeza ya mshahara mfukoni.

Tukaenda. Majeraha ya kisiasa tuliyoyatengeneza Mbeya ni kwa nchi nzima. Taifa lilipopatwa na msiba mkubwa wa kuwapoteza watoto wake kwa makumi katika ajali ya shule ya Lucky Vincent, wakati wa maziko yao

kule Arusha wengine eti hawakukuona. Ulimtuma mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan Makamu Rais aliyekuwakilisha vema. Kwanini hatukumtuma Mbeya? Mshereheshaji akiona kabisa umati ulivyosinyaa baada ya kukosa nyongeza ya mishahara bado akawataka wafanyakazi na wananchi wengine wanyanyue mikono yao juu, waipunge kumuaga Rais wao. Alisahau kauli kuwa wananchi siyo mabwege. Nani anyanyue mkono wake!

Msitu wa mikono tuliokuwa tunauona katika hotuba nzima ulififia.

Ndugu Bashiru Ally aliwahi kusema kuwa kama tumejipanga vizuri hatuwezi kuogopa uchaguzi wa mwaka 2020. Kama tumejenga shule bora za kutosha zinazoonekana, zenye vitabu bora na walimu waliohamasika, tumejenga zahanati na hospitali za kutosha zinazoonekana zenye dawa, vifaa-tiba na huduma zinazoridhisha hatuna cha kuhofia. Wananchi watatuchagua. Akakumbusha tumaini jema ambalo Waziri Mkuu Ndugu Edward Ngoyayi Lowassa aliwaahidi wananchi wakati awamu ya nne inaiingia madarakani mwaka 2005. Alisema, “Tutaanza na kujenga shule za sekondari kwa kila kata. Tukishamaliza tutajenga zahanati kwa kila kata’’. Wabaya wakayakatisha maendeleo ya kweli ya wananchi kwa ripoti yao ya Richmond. Leo maisha ya wananchi pengine yasingekuwa kama hivi! Kazi ya wabaya sasa ni kuwashambulia wanachama ambao wao wanadhani wana dhamira ya kuchukua fomu kugombea urais mwaka 2020. Kinachowaumiza wanao baba, ni hawa kukufanya uonekane kama usiyejiweza. Kwamba mwenyewe huwezi kupambana na wanachama wenzako ndani ya chama ambacho wewe ni mwenyekiti na ukawashinda. Baba ameifanyia nchi hii mengi na makubwa. Kama hayo yamewagusa wananchi wa kawaida ambao ndiyo wapiga kura ndiyo yatambeba.

By Jamhuri