Ndugu Rais wananchi wanataka maziwa na asali

Ndugu Rais hii ni sauti ya mtu aliaye jangwani. Wahurumieni masikini
na wanyonge wa nchi hii. Wahurumieni watu wa Mungu hawa.

Baba, Watanzania wameteseka vya kutosha. Kwanini masikini wateseke katika nchi yao ambayo Mwenyezi Mungu aliipendelea kwa kuikirimu kila aina ya utajiri na rasilimali kupita nchi nyingine zote duniani?

Wananchi wanataka maziwa na asali walivyovifaidi kabla yetu. Kiburi chao baadhi ya viongozi wachache kitaendelea hadi lini? Wananchi watafarijika
zaidi kufanyiwa sherehe ya mchicha, bamia na matembele iliyojaa amani
na upendo kuliko kufanyiwa sherehe ya vitu vikubwa, mbuzi, hata kondoo
wa kubanikwa, lakini iliyojaa vinyongo na visasi.
Ndugu Rais, kila mtu anaweza kufanywa kuwa kiongozi, lakini si kila mtu
ana uwezo wa kuongoza watu. Uwezo wa kuongoza watu ni karama itokayo kwa Mungu mwenyewe. Na apewaye hupewa tangu akingali tumboni mwa mama yake. Wako waliopata kuonekana kuwa viongozi bora huku wakiwa hawana karama, lakini wakafanikiwa tena hata sana. Hawa ni wale tu waliyoyatumia vema zaidi na kila mara masikio yao yote mawili kusikia zaidi badala ya kutumia zaidi kusema kwa mdomo wao mmoja. Mwenyezi Mungu alipotuumba na masikio mawili, lakini akatuwekea mdomo mmoja tu, hakufanya hivyo kwa bahati mbaya. Alikuwa na makusudi yake.

Baba tumeumbwa tusikie zaidi na tuseme kwa kiasi. Wenye busara wametushauri kuwa kabla hatujasema, tuyapime kwanza maneno yetu. Wakale walisema, “Fikiri kwanza kabla ya kusema”.
Ndugu Rais, Watanzania nchi waitakayo ni ile ya Baba wa Taifa. Tanzania
ya viwanda halisi vilivyokuwa vinazalisha siyo hii ambayo masikini wake wanazidi kukata tamaa! Tanzania ambayo ilikuwa na amani, upendo,
umoja na mshikamano, iliyowapa wao kama jamii moja, matumaini mapya na ustawi. Kamwe, wananchi hawaitaki harufu ya damu inayonuka katika
nchi yao. Yaonekana tuna mipango na miradi mingi mikubwa sawa, lakini
isiwe ni mipango na miradi mikubwa ambayo inazidi kuwatenga masikini
na kuufanya umasikini wao kuwa ni wa kudumu. Baba nchi ni watu. Ni
kweli imeandikwa asiyefanya kazi na asile, lakini ni kweli pia kuwa
mwanadamu anapoletwa hapa duniani na mama yake kwa mara ya kwanza,
huanza kula kwanza kabla hajaanza kufanya kazi. Hivyo, tunapowataka
kufanya kazi tukumbuke pia kuwa ni wajibu wetu kuhakikisha wanakula.
Hapa Kazi Tu halafu kula, ‘no’ hapana Baba. Hiyo si sahihi. Watanzania
walio wengi wanafanya kazi sana, lakini wakati mwingine kipato chao
kinanyonywa na mipango mibovu nyongefu ya baadhi ya viongozi wao.
Kama tulidhani kulizima Bunge lisionyeshwe ‘live’ kutatusaidia kuwaficha wananchi wasijue maovu tunayowafanyia bungeni hatukuamua
sawa sawa. Mwenye nia njema na moyo safi kila siku hana cha kuficha.
Bali muovu na mharibifu ana siri nyingi hata zilizo wazi kwake bado ni
siri.

Wananchi walifuatilia kwa uchungu mkubwa mjadala wa korosho bungeni. Nasema kama alivyosema yule mwingine, hili la korosho namwachia Mungu, lakini Baba, Mungu alituzidishia sikio moja, yakawa mawili ili linapokuja jambo kama hili la korosho, tusikie zaidi, lakini tuseme kwa kiasi.
Mwanamwema Masako aliniandikia ujumbe akiniuliza ni kazi gani
ningependa kuifanya. Ya kulima mbaazi zinazouzwa kilo moja Sh 150 au
kuokota makopo barabarani ambayo kilo moja inanunuliwa kwa Sh 450?
Nikamwambia kuokota makopo. Haitashangaza kuona huko tuendako wakulima wa korosho nao wakalazimika kuona maslahi sasa ni kuokota makopo barabarani badala ya kulima mikorosho. Madhara makubwa ya maendeleo ya vitu ni kujenga au kununua mitambo ghali huku tukiwafukarisha zaidi wananchi wetu. Walisema, “Chuma huliwa na kutu, lakini cha mtu huliwa na mtu!”
Ndugu Rais, mwasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwaambia Watanzania kuwa maadui wetu wakuu ni
watatu – ujinga, maradhi na umasikini. Lakini mimi nawaambia masikini
wenzangu kuwa adui wetu mkuu ni mmoja tu naye ni UJINGA. Siandiki
kuitengua torati, bali kuitimiliza. Kumshinda adui mjinga wale wawili
watashindwa wenyewe. Elimu katika nchi hii imepuuzwa kwa muda mrefu na sasa imefikia kiwango cha mwisho. Wenye uelewa finyu waliposikia elimu bure walidhani ni kusoma, kuandika na kuhesabu bila kulipa. Hii haipo popote duniani. Malipo lazima yafanyike. Au kwa msomi mwenyewe kulipa ada anakosoma au serikali kukusanya malipo hayo kama sehemu ya kodi inayokusanya. Anayekuambia kuna elimu bure mhurumie, hajui alisemalo.
Naibu Waziri wa Elimu, William ole Nasha alipoulizwa kuhusu kitabu kinachoendelea kupotosha wanafunzi alijibu, “Siwezi kuzungumzia kitabu
hicho, lakini suala la vitabu vyenye makosa limeishajadiliwa na Serikali imechukua hatua kuviondoa kwenye mzunguko.”

Hawa ndiyo viongozi wetu. Hili ni suala la kujadiliwa? Baba kunani Wizara ya Elimu? Hivi ninavyokuandikia watoto wa masikini wanamaliza zaidi ya
mwaka hawana vitabu vya kusoma! Watoto hawana vitabu shuleni, lakini
wachapishaji wana vitabu vimejaa katika maghala yao hawana kwa kuvipeleka – vitabu ambavyo wizara yenyewe imeishavithibitisha kuwa ni
vitabu bora kutumika shuleni. Nchi moja, serikali ziko ngapi?
Kwanini wizara haiwapelekei watoto vitabu hivi na hasa wakati huu
wanapoendelea kuvutana kuhusu vitabu-sumu vyao? Baadhi ya walimu
wanasema kufeli kwa watoto tatizo kubwa liko kwenye vitabu. Mwingine
anasema, “Vitabu vyote vya hisabati kutoka kidato cha kwanza hadi cha
nne vina makosa.”

Kutokana na makosa hayo wamelazimika kutumia vitabu vya zamani vilivyochapishwa na wachapishaji binafsi. Baba mwambie waziri wa elimu majadiliano baadaye. Awapelekee watoto vitabu walivyonavyo wachapishaji.
Ndugu Rais, ujumbe, “Tunapenda sana uandishi wako ndugu Mayega kwenye gazeti la JAMHURI. Sisi wahanga tuliostaafu tangu mwaka jana
hatujalipwa mafao. Wengi tumepanga uraiani. Kupitia Fikra za Mwalimu
Mkuu, tunakuomba umwandikie Mheshimiwa Rais wetu ili afahamu shida
tunazozipata.” Simfahamu amejiita Infomers Mhanga.

Baba haya na mengine yawezekana ndiyo yanawafanya baadhi ya Watanzania wenzetu wasishangilie ujio wa ndege mpya wala ujenzi wa treni. Basi, si kwa kiburi chao! Wanatafakari kipi kianze. Uhai wao au ufahari wao!
Tusikimbilie kuwahukumu na kuwaona chizi. Kama uchizi tuutafute kwanza kwetu. Baba wanachokitaka ni maziwa na asali, siyo harufu ya damu!

905 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons