Ndugu Rais watoto wasiandaliwe vitabu-sumu vingine

Ndugu Rais, Watanzania wanapaswa kumshukuru Mungu kumpata rais anayethubutu. Katika kipindi kifupi umegusa mambo mengi yenye uzito mkubwa ambao wenzako wasingethubutu! Hata kama hutafanikisha, lakini historia itasema huyu alithubutu! Kwa makaburi uliokwishafukua mpaka sasa, nani mwingine angeweza?
Wakati unaendelea na hayo mengine huku waliowema wakikuombea, kumbuka usemi wa wazee wetu, kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Tusingoje tukifikiri kuwa tutakuja kuwatibu watoto wetu, watakapokuwa wamekwishaathiriwa na sumu iliyomo ndani ya vitabu walivyopelekewa! Tutakuwa tunajidanganya kwa sababu hiyo haitawezekana!

Wakinge watoto wa masikini wanaoendelea kunyweshwa sumu ya vitabu-sumu ambavyo bado viko shuleni.
Tulisema tangu mwanzo kuwa busara inamtaka aliyeumwa na nyoka kupanua kwanza jereha lake ili kuitoa sumu kwanza kupitia damu nyingi itakayomwagika. Kisha kama panafungika funga upande unaoelekea uliko moyo ili damu isipande kuelekea huko. Kuchelewa kufanya hivyo ni kuruhusu sumu ya nyoka kuendelea kusambaa mwilini. Itakapoufikia moyo aliyeumwa na nyoka atakufa! Hili ndilo linalongojewa kuwapata kielimu watoto wa masikini na wanyonge wa nchi hii baada ya kumwagiwa vitabu-sumu shuleni na kugoma kuviondoa!

Waliowamwagia vitabu-sumu hivi hawataki kuviondoa haraka ili sumu isiendelee kusambaa! Wanangoja mpaka watoto hawa watakapokuwa wamekufa kabisa kielimu! Baba, kama wewe mwenyewe hutaingilia kati kuwaokoa masikini na watoto wao wa Taifa hili ni nani mwingine atakuwa mkombozi wao? Baba waamuru wote, iwe ni kwa tamaa ya mali au vinginevyo, waviondoe haraka vitabu-sumu vyao kutoka shuleni.
Sasa zinaanza kusambazwa porojo zisizo na mashiko kuwa hao wenye vitabu-sumu watashirikiana na PATA- Chama cha Wachapishaji- kuvirekebisha ambavyo tayari viko shuleni. Kwakuwa waliotajwa hawajakanusha. Siwezi kuwasemea. Kila mtu anajua anavyoganga njaa yake.

Lakini baba nakupa ukweli; kitabu kikishatoka katika mitambo ya kuchapia, hakiwezi kurekebishika na mwanadamu yeyote aliyeko duniani.
Haya ni maneno ya kutaka kupooza mambo na labda kupoozana!
Ndugu Rais, waliovisambaza vitabu hivi ni wasomi hivyo siyo kwamba ni bahati mbaya. Atakayesema tamaa ya fedha nyingi ilitawala, hawezi kupuuzwa na timamu yeyote! Tamaa na uroho wa fedha nyingi kuingia katika elimu ya nchi, Taifa limeangamia! Unahitaji kusafisha uozo huu kwani umekaa sehemu mbaya. Mafisadi wasambae, lakini waliohusika na ufisadi huu usipowahukumu sasa, iko siku Mwenyezi Mungu atakuja kukuuliza! Wabarikiwe sana wanawema wa Mlimanitivi ambao sala yao kuu kila siku ni ‘elimu kwanza’.

Ndugu Rais wakati tunapambana na vitabu-sumu ambavyo viko tayari shuleni kutaka viondolewe, viko vitabu vingine vinaandikwa kwa ajili ya watoto. Hatujui kama navyo ni vitabu-sumu au la, lakini vinapikwa kwa staili ileile ya vitabu sumu. Lazima ichukuliwe tahadhari kubwa kwa watu wako kuvipitia kabla havijafika shuleni. Mbaya zaidi hivi ni vya ngazi ya chini zaidi kule, watoto wanakoanzia!

Baba, pale Wizara ya Elimu kuna mradi unaitwa LANES (Literacy and Numeracy Education Support). Mradi huu unatumia mabilioni ya fedha ili kufanikisha upatikanaji wa vitabu vya watoto vya kujisomea. Kitu ambacho wananchi wako baba wanataka uwaambie ni kwa vipi waliaamua kutafuta watu wanaowajua wao eti waandike vitabu vya watoto? Hawa nao ni wasomi. Wanajua kuwa uandishi, na hasa uandishi wa vitabu vya watoto ni kipaji ambacho mwandishi anazaliwa nacho. Kipaji hakisomewi shuleni. Kuwa na digrii yoyote au kuwa mwalimu hakumfanyi mtu kuwa mwandishi mahiri wa vitabu vya watoto. Aliyewateua hao alifuata kigezo gani? Akitokea hata aliyethibitika kuwa ni mlevi tu, akasema huu ni mpango uliopangwa na watu wanaojuana wakatengeneza mazingira ya kufanya ufisadi, ni timamu gani atakayempuuza mtu huyu?

Ndugu Rais, wachapishaji Watanzania, wazawa na wageni, wana vitabu makini na vizuri sana vya watoto. Ni vitabu vingi sana ambavyo vimetayarishwa kwa weledi mkubwa. Vitabu hivi vimeidhinishwa na Wizara ya Elimu yenyewe kuwa vinafaa kusomwa na watoto shuleni. Vingine vimethibitishwa hata na taasisi za elimu za nchi nyingine kama Kenya, Uganda, Rwanda hata taasisi za kielimu za kimataifa kuwa vinawafaa watoto shuleni.
Baba waulize watu wa mradi huu, ni kwanini walivikwepa vitabu hivi ambavyo kwanza vilikuwa tayari vipo? Kwanini waliamua kutafuta waandishi wanaowajua wao? Hata kama ilikuwa ni lazima
viandikwe vitabu vingine, kwanini hawakuwachukua waandishi ambao tayari waliishathibitika kuwa ni waandishi bora kwa kuwa wana vitabu mkononi walivyoviandika vikapitishwa na Wizara ya Elimu? Ni kwanini waliwakwepa waandishi wanaojulikana? Baba kuna kila dalili kuwa watoto wa masikini wanaweza kuwa wanatayarishiwa sumu nyingine! Tujifunze kutokana na kosa kubwa la vitabu-sumu! Tusingoje mpaka vifike shuleni!
Baba, vichunguze vitabu hivi kabla havijawafikia watoto.

Ukishajiridhisha uwapatie masikini wako majibu sahihi kwa maswali haya wanapohangaika na hatima ya elimu ya watoto wao!
Ndugu Rais, majanga haya yamelikumba Taifa hili baada ya miiko na maadili vilivyokuwamo katika Azimio la Arusha kutupwa pamoja na Azimio lenyewe!
Moyo safi wa uadilifu wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiyo uliyomsukuma aachie urais bila kusukumwa na mtu. Mtawala yeyote duniani hutamani atawale milele! Lakini kiongozi mwema kwa watu wake hutamani muda wake umalizike haraka. Wanaokutakia utawale milele wanadhani hutayafikia makaburi yao. Ah! Augustino Lyatonga Mrema si uwaambie watu wa Mungu! Uliona nini njiani ulipokamata vya kukamata Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere? Lilikuwa ni kaburi la nani ili lifukuliwe? Mrema utakumbukwa na watu wema ukisema na Chavda lilikuwa ni kaburi la nani.

Ndugu Rais, hawa ndiyo wanaoifanya kazi yako njema unayoifanya iwe ngumu zaidi. Kama wasingeliua Azimio la Arusha kazi yako leo isingekuwa ngumu kiasi hiki! Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kama aliwalaani watu hawa! Akiwa amesimama chini ya mkungu nyumbani kwake Msasani, Mwalimu kwa kilio alisema, “…Paolo, Paolo, Paolo na nyinyi wengine, mkilifuta kabisa Azimio la Arusha, mtakuja kupata taabu sana baadaye…! Ningekuwa na uwezo wa kumlaani mtu ningewalaani watu hawa!” Baba, warudishie watu wa Mungu urithi wao, AZIMIO LA ARUSHA!